July 9, 2017
Taifa Stars inatarajia kuivaa Rwanda katika mechi ya kuwania kupata nafasi ya kufuzu kucheza Fainali za Kombe la Mataifa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (Chan).

Julai 15, mwaka huu, Taifa Stars itaikaribisha Rwanda kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza ukiwa ni mchezo wa kusaka tiketi ya kushiriki Fainali za Chan zitakazofanyika mwakani nchini Kenya.

Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Salum Mayanga ana imani kubwa na kikosi cha kuwa kimepata mabadiliko kupitia michuano ya Cosafa ambayo Stars imeshika nafasi ya tatu.

"Kwa kuwa tulikuwa ndani ya michuano, nina imani kubwa hii itatusaidia katika mechi dhidi ya Rwanda," alisema.

"Wao walikuwa katika maandalizi mazuri kwa kuwa wamenuia kufanya vizuri katika mechi hii. Lakini kuwa kwetu pamoja na mechi zaidi ya tatu tulizocheza, imetusaidia sana na tunataka kuitumia nafasi hiyo."

Taifa Stars ambayo ilikuwa ikishiriki michuano ya Cosafa ikiwa mgeni mwalikwa, mbio zao ziliishia hatua ya nusu fainali baada ya kufungwa na Zambia mabao 4-2.

Katika michuano hiyo, katika mechi za awali, Stars ilionyesha soka safi ikicheza na kupata matokeo yafuatayo:

Tanzania 2-0 Malawi
Tanzania 0-0 Angola
Tanzania 1-1 Mauritius
Tanzania 4-2 Lesotho (mikwaju ya penalti)

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV