July 3, 2017Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi, leo Jumatatu anatarajia kupandishwa tena kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar akiwa na wenzake wawili kufuatia kushtakiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru) kwa makosa 28 yakiwemo ya utakatishaji fedha.

Awali, Malinzi alipandishwa kizimbani katika mahakama hiyo Alhamisi iliyopita akiwa na washtakiwa wenzake ambao ni Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa Selestine na Mkurugenzi wa Fedha wa TFF, Nsiande Isawafo Mwanga ambao walisomewa mashitaka hayo 28 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbord Mashauri.

Katika kesi hiyo namba 213 ambayo baada ya kutajwa watuhumiwa walipelekwa rumande na kutarajiwa kupandishwa kizimbani leo, inadaiwa Malinzi akiwa na Mwesigwa, walihusika kughushi waraka wa kamati ya utendaji ulioonyesha kuwa  kamati hiyo imeridhia kubadilishwa kwa ‘Signatories wa Bank’ yaani mwenye mamlaka ya kutia saini ili kutoa fedha benki, kutoka kwa Edgar Leonard Masoud kwenda kwa Nsiande Isawafo Mwanga.

Malinzi alisomewa mashitaka hayo na mwendesha mashitaka wa upande wa serikali, Leonard Swai akiwa na mawakili wenzake, Christopher Msigwa, Pius Hila na Nassor Katuga. Mbali na kughushi waraka huo, pia Malinzi anatuhumiwa kwa kufoji risiti mbalimbali zinazoonyesha akilidai na kulikopesha shirikisho hilo huku akijua kuwa ni kinyume cha sheria.

Mbali ya mashitaka hayo, Malinzi, Mwesigwa na Nsiande walikutwa na kosa la kula njama ya kutenda kosa la utakatishaji wa fedha dola za Kimarekani 375, 418 (zaidi ya Sh milioni 822) wakati wakijua fedha hizo ni matokeo ya mapato ya kughushi.
Shitaka lingine ambalo liliwahusisha Malinzi na Mwesigwa ni kutoa fedha hizo kwa njia ya kughushi katika Tawi la Benki ya Stanbic iliyopo Kinondoni ikiwa ni kinyume cha sheria wakati kwa upande wa Nsiande alikutwa na kosa la kushirikiana viongozi hao kujipatia kiasi cha fedha hizo huku wakitambua ni mapato ya kughushi.


Katika kesi hiyo, watuhumiwa hao wanatetewa na mawakili Jerome Msemwa, Aloyce Komba, Sostern Mbedule, James Bwana na Asia Chali.

SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV