August 8, 2017Na Saleh Ally
GWIJI na beki kisiki wa zamani wa Arsenal, Sulzeer Jeremiah Campbell maarufu kama Sol Campbell yuko nchini kwa ziara maalum kupitia mwaliko wa SportPesa Tanzania.

Campbell amewasili na kufanya shughuli kadhaa za kijamii kama kuitembelea timu ya walemavu ya Muungano na kukabidhi vifaa vya michezo, pia jana alishuhudia mechi ya Ngao ya Jamii kati ya Chelsea dhidi ya Arsenal mubasharaa kutoka London, akiwa na mashabiki wa soka nchini.

Kati ya vyombo vichache vya habari vilivyofanya naye mahojiano ya ana kwa ana SALEHJEMBE.

SALEHJEMBE: Katika maisha yako ya timu ya taifa ya England, ulicheza kwa miaka 11. Si jambo dogo, nini hasa kilikufanya ufanikiwe katika hili wanaloshindwa wengi?
Campbell: Kweli ni jambo gumu sana, lakini lazima uwe mtu unayejitolea. Hauwezi kufanikiwa kwa kuyafanya mambo yaende tu kawaida, lazima utoke pale na kupambana kuhakikisha yanafanikiwa.

SALEHJEMBE: Kujitolea namna gani?
Campbell: Mfano unatakiwa kufanya mambo kwa ziada. Mfano kufanya mazoezi ya ziada baada ya yale ya kawaida. Tukimaliza, mimi nilikuwa nikienda tena peke yangu kufanya mazoezi ya ziada na wakati mwingine hata saa mbili zaidi.

SALEHJEMBE: Ukiwa katika mazoezi ya ziada unafanya kipi hasa?
Campbell:  Mazoezi ya ziada ni kuangalia mapungufu binafsi. Mfano stamina, kasi au kuna kosa ulilofanya katika mechi iliyopita. Utaona katika mechi inayofuata, pia linaweza kutokea kosa jingine na hii ni kawaida katika soka. Nalo unalifanyia kazi kwa mfumo huohuo.

SALEHJEMBE: Lakini mazoezi ya pamoja yanaweza kutosha kukubadilisha, ninamaanisha mazoezi ya ziada si lazima sana?
Campbell: Hapana, mazoezi ya pamoja yanaweza kukuimarisha lakini kila mmoja anakuwa na makosa yake binafsi ambayo yatajengwa na mazoezi au juhudi binafsi. Tena uvumilivu wa marekebisho ndiyo jambo bora zaidi.

SALEHJEMBE: England kwa upande wa klabu na hata timu ya taifa inaonekana imepoteza mabeki wa aina yako, tatizo ni nini?
Campbell: Kweli kunaweza kuwa na utofauti wa wakati. Aina ile haipo lakini kiasi unaweza kuwapata watu kama Gary Cahill ambaye amekuja mwishoni. Lakini ni kweli, kama utazungumzia mabeki imaraimara kweli tena manahodha, kwa sasa hakuna tena.

SALEHJEMBE: Kwanini hakuna?
Campbell: Ni kama mzunguko hivi, mambo hutokea. Watu wa aina hii wanakuwepo lakini baadaye wanapotea na huenda baada ya miaka minne au mitano ijayo wanaweza kupatikana tena watu wa namna hiyo.

SALEHJEMBE: Nini cha kufanya kwa England?
Campbell: Ni kutengeneza watu imara kwa kila sehemu, kuanzia kwa kipa, mabeki viungo na washambulizi. Inatakiwa sasa, kuanza na wale watoto, vijana waendelezwe na baada ya hapo utaona mambo yanabadilika tena kwa kuwa mtafanya jambo kwa kufanyia kazi tatizo husika.SALEHJEMBE: Hili lililenga kwenye timu za taifa za vijana?
Campbell: Kabisa, kwa kuwa kama mtakuwa na vijana bora watawasukuma hata wale waliokuwa katika timu kubwa kufanya vizuri zaidi wakijua hakuna utani kuna vijana wanakuja. Hii pia itasaidia kuongeza umoja wenye ushirikiano uliolenga kufanya vema zaidi.

SALEHJEMBE: Kuwa na timu bora ya taifa ili kufanya vizuri kimataifa, kipi kinatakiwa kufanyika?
Campbell: Kuna mengi kama ligi bora na kadhalika. Lakini kikubwa kabisa ili kufanya vizuri kimataifa lakini ni lazima timu kuwa angalau na wachezaji nane bora wa ngazi ya ushindani kimataifa katika kila nafasi. Kama ni namba sita, ajue kuna wengine saba wana uwezo kama wake au zaidi wanaweza kucheza nafasi hiyo. Hapa lazima kikosi chenu kitakuwa bora chenye uwezo wa  kutawala na kufanya vizuri katika michuano mbalimbali mikubwa kama Kombe la Dunia, tena kwa muda mrefu kabisa na kwa uhakika.

SALEHJEMBE: Mikono yako ni kati ya ile ya mwisho kushika kombe la ubingwa wa Ligi Kuu England. Baada ya hapo, kwisha kazi. Unafikiri Arsenal wanastahili kufanya kipi kurudisha uwezo wa kushinda tena ubingwa huo?
Campbell: Kwanza tusiichukulie Arsenal kama haijawahi kushinda kabisa vikombe, hata msimu uliopita walichukua ubingwa wa Kombe la FA, ambao si haba na imewafanya kuwa wanaoshikilia rekodi ya kubeba Kombe la FA najivunia wao katika hilo. Pia ni jambo zuri kwa wachezaji kwa kuwa kila msimu wanataka kuondoka na jambo ubingwa fulani kuliko mikono mitupu na makombe ni machache hivyo ni jambo bora kabisa kwa Arsenal na wachezaji wao.SALEHJEMBE: Pamoja na yote hayo, bado Arsenal wanaonekana kutotulia kwa kuwa ubingwa wa Premier League ni zaidi ya miaka kumi sasa?
Campbell: Ni kweli, ingawa ni kawaida kwa timu kupitia mambo mbalimbali ya furaha na magumu.

SALEHJEMBE: Sawa, nini kifanyike labda ili Kocha Arsene Wenger aweze kuzima kelele hizo za ubingwa?
Campbell: Anajitahidi sana, Wenger anatakiwa kuendelea kubakiza wachezaji, kutengeneza timu na kuifanya iwe imara na hili jambo linaweza kutokea au la lakini inategemea na kinachofanyika. Arsenal wanajaribu kwakweli.

SALEHJEMBE: Kama wanajaribu, unafikiri kuna mwanga unaonyesha watafanikiwa kupata wanachotaka, labda msimu ujao?
Campbell: Lolote linawezekana lakini itakuwa ni rahisi kuanza kujua wanaweza au la baada ya mechi kumi na tano za mwanzo.

SALEHJEMBE: Ila Arsenal wamekuwa na mwisho mbaya mara nyingi.
Campbell: Majeruhi yanaweza pia kuchangia, si kitu unaweza kuwa na uhakika nacho. Mfano, msimu Leicester waliochukua ubingwa, nafikiri walikuwa na majeruhi mmoja au wawili. Tena wakikaa sana ni wiki moja au mbili na huenda isiwe wale wanaotegemewa sana. Wengine wote walikuwa fiti, sasa Arsenal pia wanapaswa kuwa na hali hii.SALEHJEMBE: Unaona kikosi cha Arsenal ni bora kubeba ubingwa?
Campbell: Ndiyo, inawezekana lakini wakiweza kuwa fiti hadi mwishoni. Tena pia kama watabaki na kikosi chao na watu wao muhimu.

SALEHJEMBE: Karibu sana Tanzania, labda kabla ya kuja, ulisikia nini hasa kuhusiana na nchi hii nzuri?
Campbell: Tanzania ni nchi nzuri sana ingawa sijakaa kwa muda mrefu, watu ni wacheshi, hali nzuri ya hewa na kweli nimefurahi sana kuwa hapa na ningependa nafasi zaidi ya kuona mengi.

Kabla sikuwahi kuisikia sana Tanzania kuhusiana na mpira ni kidogo tu. Lakini zaidi ni masuala ya utalii, kwenda mbugani, pia kuhusiana na ufukwe mzuri wa kuvutia na kadhalika.

SportPesa pia imefanifanya nijue zaidi kuhusiana na Tanzania. Udhamini wao na Arsenal na klabu nyingine za England ni kitu ambacho kinakulazimisha kuwafuatilia na kujua mengi.


SALEHJEMBE: Umesema umewahi kusikia kuhusiana na Tanzania lakini si soka. Je, hukuwahi kusikia lolote kuhusiana na Simba na Yanga?
Campbell: Ndiyo, kwamba moja ina mashabiki kama milioni tisa hivi, nyingine inaizidi nyingine kwa mashabiki kama milioni moja hivi. Lakini pia zimeigawanya nchi ya Tanzania kwa ushabiki. Kwamba bila kujali mtu anatokea wapi, au mkoa upi lazima atakuwa shabiki wa moja wa hizi timu. Hivyo sijasikia mengi sana, zaidi ni hayo mazungumzo kuhusiana na masuala hayo, basi.

Mafanikio yake ya makombe
Tottenham Hotspur
Kombe la Ligi: 1998–99
Arsenal
Ligi Kuu England: 2001–02, 2003–04
Kombe la FA: 2001–02, 2004–05
Portsmouth

Kombe la FA : 2007–08

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV