August 5, 2017




Na Saleh Ally
UNAWEZA kusema leo itakuwa siku ya burudani kwa mashabiki wa soka duniani kote wakati msimu mpya wa soka nchini Ujerumani ukiwa ndiyo unaanza.

Msimu unaanza kwa kuwa vigogo wawili wa muongo mmoja nchini humo, Bayern Munich na Borussia Dortmund wanakutana katika mechi ya DFL-Supercup.

Mechi hiyo itakayoonyeshwa mubashara na StarTimes inachezwa kwenye Uwanja wa Signal Iduna Park mjini Dortmund na kawaida hilo ndiyo huwa kombe la kwanza kutolewa kila mwanzo wa msimu katika mechi inayowakutanisha mabingwa wa Bundesliga dhidi ya wale wa Kombe la Ujerumani au Germany Poka.

Bayern na Dortmund kila upande umebeba kombe hilo mara tano, ndiyo mara nyingi zaidi na timu nyingine iliyojitutumua kushindana na vigogo hao ni Werder Bremen iliyobeba mara tatu, wengine hakuna anayesogea hata kidogo.

Presha ni kubwa kwa mashabiki kwa kuwa kila mmoja ana hofu, hana uhakika sana kama usajili mpya waliofanya unaweza kubadili mambo na wao wakanywa bia za kutosha baada ya mechi hiyo. Maana furaha ya Wajerumani haiwezi kukamilika bila “kinywaji”.



Hofu kubwa iko kwa makocha, kila mmoja angependa kubeba kombe hilo kwa mara ya sita na kumzidi mwingine lakini uzuri limekuwa likisaidia kufanya mambo yatulie kwa yule ambaye anashinda mechi hiyo ya mwanzo kuukaribisha msimu.

Dortmund waliwatwanga Bayern katika fainali ya 2013 na 2014, nao wakakubali kupokea kipigo katika fainali ya 2012 na 2016. Nani atakuwa mbabe leo kuchukua kwa mara ya sita lakini kumshinda mwenzake zaidi katika siku husika na rekodi? Hofu inazidi kupanda.

Kila timu imetoka katika maandalizi ya msimu mpya barani Asia. Maandalizi mazuri ya upande wowote yatatoa majibu leo upande mmoja.

Kocha wa Bayern, Carlo Ancelotti anaweza kuwa na hofu ya kumkosa beki Mhispania, Juan Bernat, ambaye alilazimika kurudishwa Ujerumani wakati timu hiyo ikiwa barani Asia kwa maandalizi ya msimu baada ya kuumia.

Uhakika wa uimara wa beki mwingine Mhispania, Javi Martinez, unaweza kupunguza presha ya kocha huyo mkongwe.

Hiyo haitoshi, utaona kuna presha nyingine kubwa, hii inawajumuisha washambuliaji tegemeo wa timu zote mbili na mmoja akiwa amewahi kucheza pande zote mbili.

Robert Lewandowski upande wa Bayern alikuwa mfungaji bora wa msimu wa 2015/2016 baada ya kufunga mabao 30, msimu uliofuata wa 2016/17, raia wa Gabon, Pierre Emerick Aubameyang akapiga mabao 31 na kuwa mfungaji bora.

Wanaume hawa mmoja kutoka Poland na mwingine Gabon barani Afrika kila mmoja atataka kuonyesha ameanza vizuri kwa kuipa timu yake kombe.


Kwa mashabiki, tegemea kuona idadi kubwa ya mashabiki wenye jezi za rangi ya njano na nyeusi na hawa ndiyo mashabiki maarufu zaidi barani Ulaya kwa kuwa BVB wanaongoza kuingia uwanjani kuisapoti timu yao ya Dortmund.

Wale Bavarians wakiwa na jezi za rangi nyekundu, nyeupe na bluu kwa mbali, lazima watajazana kwa wingi pia kuhakikisha wanatoa sapoti ya kutosha kwa kikosi chao ili kishinde nao waingie mtaani kupiga “kinywaji” cha furaha.

Wakati mtu anaangalia mechi hii leo kupitia StarTimes ambao wana haki ya kuionyesha kwa upande wa nchi zilizo chini ya ukanda wa Jangwa la Sahara ikiwemo Tanzania, atagundua mambo mengi sana kupitia mechi hiyo.


StarTimes wanatumia mfumo wa HD ambayo hukupa hisia kuhisi kama uko uwanjani. Itakuwa pia rahisi kuona namna wachezaji hao wanavyotaka kutimiza malengo ya ushindi na kutanguliza mguu mzuri kwa maana ya kuanza vizuri.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic