August 7, 2017Mgombea wa Urais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia amezindua kampeni zake leo na kueleza anachotaka kufanya ikiwa ni pamoja na kubadilisha mambo kadhaa pale atakaposhinda.

Karia ambaye pia ni kaimu rais wa TFF, amezindua kampeni hizo leo Jumatatu na kutangaza vipaumbele 11 ambavyo ndiyo mambo muhimu amepanga kuyafanyia kazi atakapoibuka na ushindi.

Uchaguzi mkuu wa TFF, umepangwa kufanyika Agosti 12 mjini Dodoma huku kampeni zikianza leo rasmi.


Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Karia alivitaja vipaumbele hivyo, kuwa ni nidhamu ya muundo na mfumo wa TFF, pili maendeleo ya soka la vijana, wanawake na ufukweni, tatu mafunzo na ujenzi wa uwezo, nne mapato na nidhamu ya fedha, huku tano ikiwa miundombinu na vifaa.

“Kipaumbele cha sita ni maboresho ya Bodi ya Ligi, saba ushirikiano na wadau, nane udhamini na masoko, tisa maboresho ya mashindano, kumi uimarishaji wa mifumo ya kumbukumbu na kumi na moja tiba ya changamoto za waamuzi na uamuzi,” alisema Karia.

Karia ambaye hivi karibuni alikumbwa na kashfa ya uraia kabla ya Mamlaka ya Uhamiaji kumsafisha, mbali na kuanika vipaumbele hivyo, pia amekuja na kauli mbiu yake inayofahamika kama Uwazi, Uadilifu, Uwajibikaji na Maendeleo.

Karia alisisitiza kuwa, vipaumbele hivyo ndivyo atavifanyia kazi pindi atakapopata ridhaa ya kuwa Rais wa TFF katika kipindi kijacho cha miaka minne.


Aliongeza kuwa, uzoefu alioupata wa kuwa ndani ya shirikisho hilo tangu kipindi cha rais Leodger Tenga mpaka sasa Malinzi ambapo yeye ni makamu wa rais, anaamini utamsaidia sana kulisogeza mbele gurudumu la soka letu.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV