August 9, 2017MWANARIADHA Mtanzania, Alphonce Felix Simbu, wikiendi iliyopita alifanikiwa kushinda medali ya shaba katika mashindano ya Mbio za Dunia kwa upande wa Marathoni zinazoendelea London, England. 

Simbu mwaka jana katika mashindano ya Olimpiki jijini Rio De Janeiro, Brazili alishika nafasi ya tano, kabla ya Januari, mwaka huu kushinda medali ya dhahabu katika mbio za Standard Chartered Marathon zilizofanyika India kwa kushika nafasi ya kwanza baada ya kutumia saa 2:09: 32. 

Mfukuza upepo huyo ambaye ni nahodha wa timu ya taifa iliyoshiriki mashindano hayo ikiwa na wawakilishi nane, amefanikiwa kushinda medali hiyo baada ya miaka 12. 
Simbu ameshinda medali kwa kushika nafasi ya tatu baada ya kutumia muda wa saa 2:09:51, akiwa nyuma ya mshindi wa kwanza, Mkenya Geofrey Kirui, aliyetumia muda wa saa 
 2:08:27, huku mshindi wa pili, Muethiopia, Tamirat Tola akitumia muda wa saa 2:09:47. 

Licha ya ushindi huo wa mwanariadha huyo lakini ameshindwa kuvunja rekodi ya muda wa saa 2:09:21, iliyowekwa na Mtanzania, Christopher Isegwe mwaka 2005, katika mashindano hayo yaliyofanyika jijini Helsink, Finland. 
Championi Jumatano, limefanya mahojiano maalum na mfukuza upepo huyo ambaye alianza kwa 
 kuwashukuru Watanzania kwa kuweza kumuombea mpaka akashinda medali hiyo ambayo ilikuwa ikimpa wakati mgumu kwa muda mrefu. 

“Kwanza Watanzania wanatakiwa kujua ni kwa kipindi kirefu tumeyumba katika mchezo wa riadha na michezo mingine lakini sasa riadha ni kama imeshaanza kufunguka. 
“Lakini hatuwezi kupata mafanikio kwa kasi na ndiyo maana unaona kuanzia mwaka juzi, mwaka jana imeonekana kuna unafuu na leo tumeweza kupata medali, siyo jambo ambalo linaweza kufanyika kwa wepesi. 

“Zaidi inahitajika subira na ndiyo maana nikajitahidi kwa hali na mali mpaka tukaweza kupata medali, kwetu sio kitu cha kushangaza, wenzetu wamejipanga siku nyingi sana ila sisi tunafanya sasa hivi hivyo lazima kutakuwa na utofauti mkubwa. 
CHANGAMOTO GANI UMEKUTANA NAZO KABLA YA KUSHINDA? 

“Unajua changamoto katika mashindano ilikuwa kubwa hasa kwa wachezaji wenzangu ambao nilikuwa nashindana nao kwa sababu nilikuwa napambana kuwaacha nao walikuwa wakipambana kuniacha. 
“Ni moja ya changamoto ambayo tunakutana nayo kwenye mashindano, nimesapoti wenzangu, tulikuwa wote maana hata kabla ya kukimbia tulikuwa tumeambiana tujitoe muhanga hata kama hatutopata medali wote basi apate mmoja kati yetu. 
“Tunashukuru tumejitahidi, tukajitoa muhanga na tumefanikiwa kuchukua medali moja ambayo ni ya Shaba lakini sapoti ya wenzangu imechochea kuweza kushinda medali hii kwa kuwa tulikuwa tukihamasishana. 

UNAZUNGUMZIAJE USHINDI HUO? 
“Wakati wa kushangilia furaha yangu ilikuwa kubwa sana kwa sababu hili jambo lilikuwa linaninyima usingizi siku zote kwamba ni lini Tanzania na sisi tutapata medali katika mashindano makubwa ili kuweza kuondoa kasumba ya muda mrefu ambayo ipo vichwani mwa watu wengi. 

WAKATI UMEMALIZA MBIO ULIONEKANA UKITAFUTA BENDERA LAKINI UKAIKOSA, KWA NINI ILIKUWA VILE? 
“Wakati namalizia mbio ni kweli nilikuwa natafuta bendera ya nchi yangu ila haikuwepo lakini baadaye nikakumbuka kuwa viongozi walikuwa katika vituo wakiendelea kutoa huduma ya maji kwa wenzangu ambao walikuwa hawajamaliza. 

“Unajua vituo vilikuwa viwili, sasa kama kimoja kipo wazi walikuwa wengine walikuwa wakihamia kingine kuendelea kutoa huduma kwa wenzangu ambao bado walikuwa wakikimbia, naomba jambo hilo lisilete mitazamo tofauti kwa sababu viongozi bado walikuwa wakipambana kuwasaidia wengine kuwapa huduma. 
“Angalia hata ushindi ambao tumeweza kupata umetokana na mafanikio yao ya huduma ambazo tulikuwa tunazipata kule barabarani, ikizingatiwa walikuwa wachache hivyo hawakuweza kutosha ila nashukuru bendera ilipepea. 

UNAZUNGUMZIAJE KUCHUKUA MEDALI BAADA YA MIAKA 12? 
“Kiukweli hata mimi mwenyewe binafsi nimefurahi sana kwa medali hii maana ni muda mrefu umepita bila ya sisi kuweza kufanya hivi, naamini itaniongezea juhudi na maarifa makubwa katika mashindano yajayo. 

“Kikubwa ambacho kipo ni kumuomba Mungu azidi kunijaalia ili niweze kuendelea kufanya makubwa katika medani ya mchezo wa riadha maana hii ni zawadi kwa Watanzania ambao naamini leo hii wanafura kubwa.

CHANZO: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV