November 20, 2017




Na Saleh Ally
NILIJARIBU kuweka maoni yangu kidogo mtandaoni nikiwaeleza wadau wa mpira nchini namna ambavyo nilikuwa nimefikiria kuhusiana na wachezaji wa kigeni wanaokuja kucheza nchini.

 Asilimia kubwa niliona waliungana na mimi na walikuwa wanapendelea mambo yatokee kama ambavyo nilikuwa nikitamani yawe.

Wako wachache ambao nilikuwa ninawaza wapo, kweli walikuwepo na mawazo yao hasi ambayo yamekuwa mawazo ya viongozi wengi wa mpira wanaozidi kutukwamisha kwa kuwa hawana uamuzi wa kusimama bila ya hofu.

Labda nirejee nyuma kidogo. Kama unakumbuka kuliwahi kuwa na mjadala mkubwa wa kuhusiana na kupunguza wachezaji wa kigeni katika ligi zetu na wako walitaka hata wasiwepo kabisa. Mimi nilikuwa katika kundi la wanaoamini wageni ni muhimu lakini kuwapunguza si vibaya.

 Nilikuwa katika kundi wanaotaka wawe watano katika kila, awali ilipitishwa hivyo lakini uongozi wa TFF chini ya Jamal Malinzi ukabanwa mbavu na Yanga, Simba na Azam FC ambao mwisho walikubali kuongeza wawili wawe saba badala ya ule msimamo wa awali wa watano.

 Mjadala nilioweka mtandaoni ni kuhusiana na suala la kuwepo kwa wachezaji wengi wa kigeni, wako wenye viwango sawa au wanazidiwa na wachezaji wa hapa nyumbani lakini wanapewa thamani kubwa.

 Pamoja na kupewa thamani kubwa, bado wanaonekana wao hawajali lolote kuhusiana na thamani wanayopewa mishahara yao hadi zaidi ya mara nne kwa wachezaji wazawa. Nyumba nzuri na wakati mwingine magari.

 Wako wachezaji wachache kutoka nje ndani ya Yanga, Simba ambao angalau unaweza kuwatumia kama mfano kutokana wanavyofanya kazi yao vizuri. Angalia Emmanuel Okwi, James Kotei au Method Mwanjale kwa Simba, au Amissi Tambwe,Youthe Rostande, Thamani Kamusoko, sasa Obrey Chirwa na wale wa Azam FC. Lakini wengine wanaonekana kutojali na viongozi wanalazimika kuwapapatikia kwa hofu ya kuwaudhi mashabiki wao.

 Si jambo jema kuwa na kiongozi anayesumbuliwa na wachezaji na akawa na hofu ya kuchukua uamuzi kwa kuwa mashabiki watakasirishwa.

 Juuko Murshid aliyekwenda Uganda, kila mara akirejea kwao kurudi kazini imekuwa ni mbinde na viongozi hulazimika kumbembeleza arejee. Sasa anawasumbua, wao wanajua lakini hofu ya mashabiki akiachwa, atakwenda Yanga.

Ujinga wa kuamini akiachwa atakwenda Yanga au akiachwa atakwenda Simba ndiyo umekuwa kichaka cha wachezaji wengi kuutumia kufanya mambo yao ya kijinga dhidi ya uongozi.

 Wangapi walikwenda Simba na Yanga inaendelea, au wangapi unawahia walihamia Yanga na Simba inazidi kupeta? Sasa kuna sababu gani ya kuingia hofu na kuwavimbisha vichwa waendelee kuwatesa kwa sababu za kijinga?

 Juuko hayupo,Yusuph Mlipili wa Simba ambaye amesajiliwa kutoka timu ya Toto African iliyotelemka daraja ameonyesha kiwango cha juu kabisa. Jiulize huyo anatokea timu kama Toto, kwangu naona ana kiwango kizuri hata kuliko huyo Juuko?

Kama kweli alicheza michuano ya Kombe la Mataifa Afrika, basi anapaswa kuwa mfano wa utendaji na nidhamu pia. Mambo ya kucheza kwa kutumia majina ni ulimbukeni na kuwafanya Watanzania wajinga huku tukiziba nafasi za vijana wetu wa Kitanzania kupata nafasi za kucheza na kuonekana.

Angalia Yanga wanavyohangaika na Donald Ngoma, ni kitu cha ajabu kabisa. Kama akichukuliwa hatua utaona watu watalalamika. Najua, Ngoma hakutakiwa Yanga na Simba walishamalizana naye ilibakia kusaini tu lakini wanachama wa Yanga wakatia presha kubwa hadi kumfuata uwanja wa ndege na Yanga ikamsainisha kwa presha kubwa huku ikimpa fedha zake zote za usajili dola 40,000, utafikiri ilikuwa ikinunua mchezaji mpya!

Leo anafanya anavyotaka, Yanga inalalama kila kukicha. utovu wake wa nidhamu ni wazi na hakuna hatua zinazochukuliwa kwa hofu ya kuwadhi mashabiki. Hili nijambo baya kabisa, tena linaonyesha kiasi gani viongozi wamekubali kuwa dhaifu na klabu zinakuwa zinaongozwa na mashabiki na si viongozi tena.

Ushabiki wa Yanga na Simba hauwabadilishi mashabiki wake kubaki Watanzania au wazalendo. Hauwageuzi kusahau umuhimu wa utaifa kwa maana ya kuona vijana wa Kitanzania wanaendelea.

Wangapi walio Yanga leo wanamfurahia Samatta? Au wangapi mashabiki wa Simba wanaofurahishwa na alipofikia Saimon Msuva? Hawa wameonekana baada ya kupewa fursa kuliko ingetolewa kwa wageni wanaoleta nyodo na upuuzi bila ya kutusaidia.

Nimesikia kuna timu moja ina wachezaji wa kigeni waliopangiwa nyumba nzuri huku wachezaji wazalendo wanalazwa kwenye nyumba za kulala wageni zenye kiwango duni, tena chumba kimoja watu wawili na kuna wakati timu ikisafiri, wageni wanalala hoteli yao na wazawa yao? Hili ni jambo baya kabisa, nafikiri vema wakalifanyia kazi kabla hatujaingia.

Leo yanga hawajalipwa mishahara, uongozi unahaha. Wachezaji wazalendo wanavumilia huku wale “wazungu” ndiyo wakiwaendesha. Kwani wao ni kina nani hasa? Wanacheza wao timu yote? Sasa kwa nini waonyesha dharau wazi na inaonekana ni sawa?

Viongozi acheni kuendelea kuamini mashabiki wote hawaelewi, simameni imara, mchezaji anayetaka kuwa mkubwa kuliko timu aende zake na nafasi hizo tuwape wazawa, muwaamini nao wajiamini tutengeneze taifa letu ili baadaye nalo litegemewe na mataifa mengine kwa ubora wa wachezaji na mwisho iwe msaada kwa timu yetu ya taifa. Amkeni, simameni, wametuchezea sana hawa, imetosha.



3 COMMENTS:

  1. Yooote uliosema nikweli lakini mi sikubaliani na swala la wachezaji hata saba mi nilitaka wasajiliwe kulingana na timu inavtoweza maana ligi ya bongo ungekua nawachezaji wengi wakigeni Leo tusingeona msuva kapiga hatua maana angekua kwenye ligi bora lands kuliko halipo lakini kwann wachezaji wetu nawao wasitoke?wanakua wengi kwao Tu watu wanakuja wanawaletea ufadha kwann nawao wasiende kwao huko acheni kuwatetea wachezaji wetu wamejibweteka wakati wanauwezo mkubwa tena saana msuva yupo moroco kila mtanzania anafurahi anavyowakimbiza huko kwann wasiende wakina nsuva wengi nje kama wakina ngoma wanavyokuja bongo?

    ReplyDelete
  2. Yooote uliosema nikweli lakini mi sikubaliani na swala la wachezaji hata saba mi nilitaka wasajiliwe kulingana na timu inavtoweza maana ligi ya bongo ungekua nawachezaji wengi wakigeni Leo tusingeona msuva kapiga hatua maana angekua kwenye ligi bora lands kuliko halipo lakini kwann wachezaji wetu nawao wasitoke?wanakua wengi kwao Tu watu wanakuja wanawaletea ufadha kwann nawao wasiende kwao huko acheni kuwatetea wachezaji wetu wamejibweteka wakati wanauwezo mkubwa tena saana msuva yupo moroco kila mtanzania anafurahi anavyowakimbiza huko kwann wasiende wakina nsuva wengi nje kama wakina ngoma wanavyokuja bongo?

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic