November 27, 2017

Na Saleh Ally, Dortmund
UKISEMA unawaonea huruma bado utakuwa haujakosea, lakini kuna jambo linatakiwa lifanyike ili msimu ujao Borussia Dortmund iweze kurejea katika ile hali yake iliyozoeleka.

Kwa sasa unaweza ukadhani ni miujiza lakini ukweli ni kwamba Dortmund, timu iliyoshika namba moja mara mbili katika misimu minne kwa kuingiza mashabiki wengi zaidi Ulaya, sasa inasuasua katika hali ya kushangaza.

Dortmund hawako vizuri na Watanzania ambao wamekuwa wakishuhudia utamu wa Bundesliga kupitia King’amuzi cha StarTimes, wanaweza kuwa mashuhuda wa hili.

Kama unashuhudia mechi za Bundesliga katika StarTimes, waangalie mashabiki wa Dortmund, nao wanaonekana kupoteza matumaini kama vile hawaelewi kinachoendelea.

Baada ya mechi 13 za Ligi Kuu Ujerumani maarufu kama Bundesliga, Dortmund iko katika nafasi ya tano ikiwa imeshinda mechi sita, sare tatu na kupoteza nne. Hii si kawaida na unaona Bayern Munich iko kileleni ikiwa na pointi 29.

Wanaoifuatia Dortmund ni RB Leipzig, timu ambayo misimu mitatu sasa inaonekana kuivuruga Dortmund na kuitisha Bayern Munich kutokana na mwendo wake. Hata hivyo, Bayern maarufu kama Bavarians hapa Ujerumani haraka walijipanga kuanzia misimu miwili iliyopita.

Hata msimu huu walipoona mambo yanayumba, haraka walimng’oa kocha maarufu Carlo Ancelloti na kumrudisha babu yao, Jupp Heynckes. Sasa mambo yanaimarika na utaona bado wako juu.

Katika Ligi ya Mabingwa Ulaya, huko nako Dortmund imepoteza mvuto na inaonekana haina nafasi ya kufanya vizuri kusema nafasi imeshaota mbawa.

Matumaini yako nyumbani hapa Ujerumani, lakini unaona kama maajabu hasa katika mechi ya juzi ambayo huenda ni kengere ya hatari kwa kikosi hicho cha Dortmund.

Wakiwa nyumbani dhidi ya Schalke 04, hadi dakika ya 60, unaona Dortmund wakiwa wanaongoza kwa mabao 4-0. Lakini ajabu kabisa hadi dakika ya 90, mwamuzi anapuliza kipenga cha mwisho, matokeo yanakuwa 4-4.

Kwa timu kama Dortmund, kama wanaongoza mabao manne hadi dakika ya 60, kawaida matarajio yanakuwa ni kufikisha hadi 7-0 au zaidi hadi mwisho wa dakika 90. Lakini haikuwa hivyo na inaonekana kama kila kitu kimeshindikana.

Unaweza ukasema kisingizio ni kutolewa kwa Emeric-Pierre Aubameyang aliyelambwa kadi nyekundu. Lakini jiulize, kwa dakika hizo 30 zilizobaki, Dortmund haina uwezo wa kulinda mabao manne tena ikiwa nyumbani?

Kwa hapa Ujerumani, Dortmund inajulikana kama BVB, timu yenye mashabiki wenye upenzi wa damu, upenzi wa hali ya juu na unaona namna ambavyo wanaumia kwa kiasi kikubwa kutokana na timu hiyo kupoteza mvuto tena kwa haraka sana.

Mvuto wa Dortmund unaonekana kuporomoka kwa kasi ya kimondo kama pale unapoelezwa mzigo umemshinda Mnyamwezi. Hivyo kinachofanyika ni punda afe mzigo ufike lakini anayefanya hivyo anashindwa kukumbuka punda akifa, siku nyingine hakutakuwa na wa kubeba mzigo.

Kikosi cha Dortmund kinahitaji mambo mawili makuu ambayo yasipofanyika hadi mwishoni mwa msimu huu, basi nafasi ya Dortmund katika Bundesliga rasmi itakuwa mali ya RB Leipzig ambao wanaonekana kuendelea kwenda mwendo uleule na wanathibitisha si watu wa kubahatisha.

Lazima suala la usajili kuimarisha ushambulizi hasa kwa mshambulizi ambaye si anakwenda kujifunza badala yake kufanya kazi ya kufunga, aongezwe na kupunguza utegemezi kwa Aubameyang pekee.

Katika usajili huohuo, Dortmund pia wanatakiwa kusajili viungo, maana viungo wa timu hiyo wanaonekana wamechoka au hawana hofu ya ushindani wa namba, pia wasajili beki maana tangu alipoondoka Mats Hummels kwenda Bayern, wanayumba sana. 


Pili ni suala la kisaikolojia, wachezaji wa Dortmund ni kama watu waliojawa na mawazo au msongo wa mawazo. Kama vile hawaelewi wanalofanya au kuna shida inawasumbua. Na kama Kocha Mkuu, Peter Bosz ameshindwa, basi haraka anaweza “akaishia zake”.

Kwa Ligi Kuu Bara nyumbani Tanzania, Simba ilipoteza mvuto na kukosa ubingwa misimu minne mfululizo. Kipindi hicho, Yanga na Azam FC wakagawana nafasi ya kwanza na ya pili.

Yanga ilikuwa bingwa mara tatu na Azam FC mara moja. Simba haikuwa na nafasi tena, lakini utaona mwanzo ilionekana ni kama utani na hakuna aliyelichukulia suala hilo kwa ukubwa wa juu.

Utaona namna Simba ilivyopambana kurejea angalau katika ile heshima yake hadi kufikia kuchukua Kombe la Shirikisho na sasa itashiriki tena michuano ya kimataifa.

Huenda Dortmund wanaona kama suala hilo litakwisha taratibu au si la kuwasumbua. Lakini kwa namna inavyokwenda, itafikia nafasi yao waliyokuwa wakichuana na Bayern katika ubingwa wa Bundesliga au Kombe la Ujerumani maarufu kama Germany Polka, itakuwa ni mali ya RB Liepzig.

Hii haiwezi kuwa utani, mechi sita Dortmund haijashinda hata moja! Ina sare mbili na kupoteza nne, hii si kawaida na si jambo la kuliona ni la kupita.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic