Uongozi wa Klabu ya Yanga, umekiri kwamba kuna wachezaji wengi wa timu yao bado wanaidai klabu hiyo fedha za usajili akiwemo Mzambia, Obrey Chirwa ambaye hivi sasa yupo kwao.
Imeelezwa kuwa, Chirwa aliyejiunga na Yanga msimu uliopita, amegoma kurejea kikosini hapo ambapo hivi sasa yupo akifanya shughuli zake binafsi huku akishinikiza kulipwa stahiki zake ili arejee kuitumikia timu hiyo.
Licha ya kutowekwa hadharani Chirwa na wenzake wanaidai Yanga kiasi gani cha fedha, lakini Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Mkwasa amemuomba Mzambia huyo kurejea kuendelea kuitumikia timu huku taratibu za kulipwa zikiendelea.
“Ni kweli kuna wachezaji wengi wanaidai klabu fedha za usajili akiwemo Chirwa, lakini kugoma kurudi si suluhisho, anatakiwa arejee aweze kuitumikia timu huku tukiangalia namna ya kumlipa stahiki zake.
“Ni fedha za usajili tu lakini masuala mengine wanapatiwa kila kitu kama bonsai za mechi na mishahara, lakini anapokaa nje ya timu anaiathiri timu, unaweza kuona kama mechi iliyopita dhidi ya Mbao tumepoteza pointi kitu ambacho hatuwezi tena kufanya kuzirudisha.
“Hali ya uchumi hivi sasa imebadilika, alitakiwa awepo kikosini stahiki zake atapata tu hatuwezi kumnyima,” alisema Mkwasa.
0 COMMENTS:
Post a Comment