March 3, 2018




Na Saleh Ally
HAKUNA anayeweza kukataa kwamba kati ya wachezaji wenye vipaji sahihi au bora ambavyo Watanzania wamebahatika kuwa navyo ni kiungo mwenye kasi wa Simba, Mohamed Ibrahim.

Ibrahim anajulikana kwa mashabiki wengi wa soka kama Mo Ibrahim. Hakika ni sehemu ya hazina ya Watanzania katika mchezo wa soka na anahitaji kukuzwa na kujikuza yeye mwenyewe.

Ntasema kwa nini nasema kujikuza na kukuzwa. Kwanza kujikuza anatakiwa kuwa mchezaji anayejitambua kuwa anataka nini, malengo au ndoto zake ni zipi na anakwenda wapi.

Huyu atakuwa anajikuza kwa kuwa atajitunza na atafanya mambo kwa juhudi na maarifa akiwa anajua anapoelekea. Kama atakuwa hajitambui, basi hata akishikwa mkono basi itakuwa ni vigumu sana kufanikiwa.

Pili nimesema kujikuza, ninaeleza hili kwa wadau nikianzia klabu anayoichezea kwa maana ya viongozi, wenzake na mashabiki lakini hata jamii inayimzunguka. Kuwa wazi kwake na mchango usi na unafiki kumsaidia kukua au kuendelea zaidi.

Unajua kuwa wengi wa wapenda soka wanaendeshwa na ushabiki zaidi badala ya hali halisi. Wengi huogopa kuwaambia watu ukweli kwa kuhofia kuwaudhi au kwa kuendekeza tu tabia za kinafiki za kutaka kuwafurahisha tena na tena hata kama wanaharibu.

Nimeshangazwa sana na kusikia Kocha Mkuu wa Simba, Pierre Lechantre akilalamika kuhusiana na Mo Ibrahim huku akisisitiza hatapewa nafasi ya kuifanya Simba ni sehemu ya kupumzikia, yaani holiday.

Kocha huyo ametumia neno hilo ambalo kwa kawaida lina maana mbaya kwa mtu ambaye ni mfanyakazi kama utaambiwa unapafanya ofisini kwake ni sehemu ya holiday au picnic.

Tofauti ya mapumziko na kazi inajulikana, baada ya kazi huwa kuna mapumziko na hata ukifanya kazi wakati wa mapumziko unaweza kusema ni jambo la ghafla au lazima.

Lakini kama utafanya mapumziko wakati wa kazi, yaani kuifanya kazi kama sehemu tu ili mradi maana yake hujitambui.

Wenzetu Wazungu ukweli ni jambo la maisha ya kawaida. Unakosea, “anakuchana” anasonga mbele. Ukiweka kinyongo wewe ndiye utakayepata shida na ikiwezekana itakuwa bora kuzichukulia kasoro zako chanya.

Kwangu inanishangaza baada ya kuona MO Ibrahim ameibuka na kuanza kufanya vema lakini taratibu amekwenda anapotea hadi sasa amepotea kabisa.

Huenda atakuwa anasubiri ile tabia ya wachezaji wa Kitanzania, kwamba anasubiri ahamie timu nyingine, aanze kufanya kazi kwa juhudi ili kuwaonyesha Simba halafu baada ya muda fulani pia anakwama tena!
Kama alionyesha ana uwezo kabla hata ya Nicholas Gyan vipi leo tena ashindwe kupata nafasi? Maana alikuwa ni kocha Joseph Omog ambaye alimuweka benchi, akawa anaingia na baadaye kumpa nafasi.

Baada ya kuondoka kwake, Mo Ibrahim hajawahi kupata nafasi ya kutosha kwa kocha Masoud Djuma aliyeshika timu kwa muda.
Wakati huo, Mo Ibrahim alipata matatizo ya kifamilia ikiwa ni pamoja na kupoteza mwanaye. Lakini sasa kuna utawala mpya ambao nao unahitaji kuona kazi kwa maana ya uwezo alionao.

Lechantre hawezi kuwa na urafiki na asiyefanya kazi yake vizuri. Atakayemsaidia kazi yake iende vizuri ndiyo atakuwa rafiki yake. Kama Mo Ibrahim atakuwa leo kazini kesho hayupo basi nafasi ya urafiki haitakuwepo na maelewano yatakuwa madogo.
Inawezekana ana matatizo hasa yaliyomtokea lakini anatambua kwamba matatizo ni yetu wanadamu, yakitokea hupita na yakitokea hayazuii kila kitu kwenda? Kama yeye hatambui kuna mtu wa karibu anaweza kujadili naye na kumsaidia?

Wachezaji wengi wa Kitanzania hawajawahi kukwamishwa na vipaji vyao. Wamekuwa wakikwamisha na tabia zao na mnajua na mnawajua kama akina Haruna Moshi Boban, Mrisho Ngassa, Athumani Iddi ‘Chuji’ na wengine wengi ambao leo wanaonekana ni watu wa kawaida wakati walistahili kuwa mbali sana.

Nani angewaambia wakati wote mnawahofia, mnahofia wasikasirike, mnawajaza ujinga zaidi kwa kuwa kabla ya kuwaambia hamtafakari! Sasa wako wapi? Angalia vipaji vyao wangapi wanavyo?
Kuna haja ya kuacha unafikiri, kuwa wazi, wakweli kwa nia ya kurekebisha. Wakati mwingine mfikie unayeamini anaharibu, mueleze hata kama kikuchukia na kuvunja urafiki na wewe, kila mwanadamu ameumbwa na “nafsi kweli”, siku itafika na itamweleza ukweli.
Mo Ibrahim badilika, kipaji ulichonacho, ukiendelea kukifunika na magugu ya tabia mbovu, mwisho kitadumaa na utaangukia walipo wengine.



1 COMMENTS:

  1. Maneno yako swadkta...tatizo lingingine ni hawa viongozi wa klabu kubwa na mawakala wa kutowaeleza ukweli.Nakufagilia ndugu Saleh pamoja Edo Kumwembe, na Hans Pope kwa kuwa wakweli wakati wote.Unakuta mchezaji anaambiwa asijutume aonekane ni mzigo kwa timu yake simply asajaliwe na timu pinzani baada ya kuhaidiwa pesa ndefu lkn hata akienda huko bila ya malengo itakusaidia nini zaidi ya kuishia maisha ya kupiga mizinga na kulalamika kuwa wachezaji wa zamani hatuthaminiwi...Inasikitisha na hasa nikifikiria Mrisho Ngassa alivyodanganywa asiende El Mirekh na leo anapigana kupandisha kiwango ili asajiliwe tena na Yanga.Tatizo la wachezaji wetu kama ulivyosema ni malezi , kutokuwa na malengo/vision.Huwa inachekesha pale unapomsikia mchezaji anahojiwa kuwa malengo yake ya baadaye ni yapi?...jibu lao rahisi ni "mie hapa napita kwani malengo yangu ni kucheza mpira Ulaya na siku ya mwisho unakuta anapigania kusajiliwa Friend Rangers,Dodoma FC,KMC etc.
    Alikoanzia Samatta na alipo sasa si issue ya kubahatisha...waangalie kina Ulimwengu, Msuva baada ya kuongezewa vitu na Hans Plujim.
    Walezi,viongozi wa Simba na wakala wake MO mwambieni ili ajitambue.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic