March 3, 2018




LEIPZIG, Ujerumani
UHONDO wa Ligi Kuu ya Ujerumani, Bundesliga unaendelea wikiendi hii ambapo leo Jumamosi mechi kadhaa zitachezwa ila mchezo mkali ni kati ya RB Leipzig na Borussia Dortmund.

Leipzig watakuwa nyumbani kuwakaribisha Dortmund kwenye Uwanja wa Red Bull na mshindi anaweza kujiweka katika nafasi nzuri ya kushika nafasi ya pili katika Bundesliga.

Uhondo wa Bundesliga ambayo mechi zake zinaonyeshwa live na StarTime hapa nchini, umefikia patamu hasa katika kuwania nafasi ya pili kwani nafasi ya kwanza ipo kwa Bayern Munich yenye pointi 60.

Leipzig na Dortmund zote zinapambana kuwania nafasi ya pili kwa sasa na mechi ya leo inaweza kutoa mwanga wa nini kitatokea katika ligi hiyo kama mwenendo wake utabaki kuwa kama huu wa sasa.

Wakati Bayern ikiwa na pointi 60 kileleni, Dortmund ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi 41 wakati Leipzig ikiwa na pointi 38 katika nafasi ya sita na pointi 38. 

Kuanzia nafasi ya pili hadi ya sita, timu zimepishana pointi tatu tu na timu itakayoshinda inaweza kupaa hadi nafasi ya tatu, hivyo leo Leipzig ikishinda itafikia pointi 41 za Dortmund lakini haiwezi kuishusha.

Hiyo imekuja kutokana na ukweli kwamba, Dortmund ina mabao 49 ya kufunga huku ikiwa imeruhusu mabao 30 wakati Leipzig ikiwa na mabao 37 na ikiruhusu mabao 33.

Chini ya Kocha Ralph Hasenhüttl, Leipzig inajivunia baadhi ya nyota wake katika kuleta madhara kwa Dortmund wakiwemo Timo Werner mwenye mabao kumi na Dayot Upamecano, Ibrahima Konaté, Marcel Sabitzer, Naby Keita, Yussuf Poulsen na Emil Forsberg.

Kiungo Keita ni yule ambaye ameshasajiliwa na Liverpool na kilichobaki ni kusubiri Julai mwaka huu ili aweze kujiunga na timu hiyo ya England.

Huyo Yussuf Poulsen ni yule mtoto aliyezaliwa na baba Mtanzania na mama raia wa Denmark na kijana amechukua uraia wa Denmark, hawa ndiyo watu tegemeo wa Leipzig.

Ila Dortmund chini ya Kocha Peter Stoger, wao huwezi kuwabeza kwani wana nyota kama Mario Götze, Marco Reus, André Schürrle, Shinji Kagawa, Sokratis Papastathopoulos na Michy Batshuayi anayecheza kwa mkopo kutoka Chelsea.

Wakati Leipzig ikicheza nyumbani na Dortmund leo, katika mechi nyingine za Bundesliga leo, Hamburger SV itacheza na Mainz 05 kwenye Uwanja wa Volksparkstadion, Augsburg itaivaa Hoffenheim kwenye Uwanja wa WWK Arena.

Eintracht Frankfurt itacheza na Hannover 96 kwenye Uwanja wa Commerzbank-Arena huku Schalke 04 ikiivaa Hertha BSC kwenye Uwanja wa Veltins-Arena huku Wolfsburg ikicheza na Bayer Leverkusen pale Volkswagen Arena.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic