May 4, 2018






NA SALEH ALLY
MABINGWA wa soka Tanzania, Yanga hakika wanatia huruma hasa kutokana na hali yao ya kimaisha kwa maana ya kifedha.


Yanga wameondoka nchini jana kwenda Algeria kuivaa USM Alger katika mechi ya Kombe la Shirikisho. Lakini ukiangalia nyuso za wachezaji wake, zinatia huruma na si vibaya kusema mambo si mazuri.


Binafsi ninaona Yanga kwenda kuiwakilisha nchi, wakiwa ni timu kubwa kwa namna walivyokwenda si sahihi hata kidogo na ningependa nikumbushe masuala kadhaa kabla ya kuendelea kusonga.


Yanga ilianza kuyumba baada ya kutoa fedha zake zaidi ya Sh milioni 100 kwa ajili ya usajili wa Donald Ngoma ambaye leo hana faida hata kidogo. Acha viongozi waendelee kumpa moyo, lakini hesabu za haraka, kutaka kuridhisha mashabiki, zilichangia wao kuingia katika uamuzi ambao haukuwa sahihi.


Sasa mashabiki walifurahi kwa muda kwa kuwa Yanga ililazimika kukopa, lakini mwisho leo wanaumia zaidi kwa kuwa kukopa fedha za mishahara kulipia usajili na kisicho sahihi, kinawaumiza wao leo. Hapa lazima mjifunze kufanya mambo kwa malengo na si kufurahisha watu tu.  



Pili ninajiuliza, labda ikiwezekana na mashabiki wengine wa Yanga kama wanaweza kutoa jibu, kwamba kama timu iko katika wakati mgumu kama sasa. Vipi hatujaona wanajitokeza wachangiaji?


Swali nauliza kwa kuwa ni rahisi sana kuona wachangiaji kama timu inakwenda kucheza mechi dhidi ya watani wake wa jadi, Simba tu! Mechi ya Kombe la Shirikisho, tena dhidi ya timu kama ya Algeria, Yanga wanakwenda utafikiri yatima, nanyi mnakubali, mkiwa mmekaa kando mnasubiri kulaumu tu?


Unaipenda Yanga, umefanya nini kusaidia katika hili? Angalau uliwahi hata kutoa ushauri ili kuchangia jambo fulani? Au mko kando Yanga ikifungwa mabao matano, muanze kulalama na kuonyesha mnaipenda timu kwa dhati mnataka kulia au ‘kufa’ kwa kuwa imefanya vibaya?


Waungwana jifunzeni, onyesheni uungwana na mbadilike na acheni kabisa kuamini Yanga inapokutana na Simba pekee ndiyo muhimu. Mnafanya hivyo kufurahisha nafsi zenu tu ili muwe na amani mitaani.


Si waungwana ambao mnaweza kuwa mashabiki mnaotambua usahihi na ubora wa timu yenu na kile inachoshiriki. Acheni kuipenda Yanga kwa maneno na mbwembwe huku mkiwa mmejaa unafiki wa maneno ambao hauisaidii yenyewe.



Nikiachana na mashabiki wa soka, naingia kwenye Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ambalo ndilo baba wa soka Tanzania. Yanga ni wawakilishi wa Tanzania tena pekee katika michuano ya kimataifa.


Wameondoka kama yatima, wasio na ndugu wala mtu wa kuwalilia. Ubaba wa TFF ni upi sasa?


Vipi angalau hata TFF isitoe kiasi cha fedha kuikopesha Yanga, ilipe hata mishahara ya miezi miwili na yenyewe ingeweza kutoa taratibu au kukata katika mechi hata zile za Kombe la Shirikisho?


TFF haiwezi kushiriki michuano, Yanga ni mwakilishi wao na hata kuingia hatua hiyo tu, shirikisho hilo litafaidika. Sasa vipi haliwezi kujitolea angalau mchango kidogo au mkopo ili kuokoa hali?


Kila mechi TFF itapata fedha, lazima Yanga ifanye vizuri zaidi ili iingize fedha zaidi na ikumbuke kama hakuna Yanga na timu nyingine, basi hakuna TFF.


Hii si sawa, Yanga imeondoka utafikiri ilipokuwa inaishi kuna wanyama na si wanadamu, maana msaada wake umekuwa ni kutazamwa na waliofanikiwa kuisaidia ni wachache sana.



Wanaoipenda wengi si wenye upendo wa dhati, wana upendo wa kinafiki, kizandiki na wazabizabina ndiyo maana wameshindwa kuonyesha wanaweza kuisaidia.


Safari ya Yanga inanikumbusha maisha ya uswahilini kwetu katika lile suala la ndugu lawama. Wao wanasubiri kulaumu tu na katika shida hawana msaada wowote.


Yanga wamekwenda Algeria lakini mkumbuke, hatujawatendea haki. Wakifungwa, msilielie tena.
Fin.




19 COMMENTS:

  1. Hongera kaka umewaambia ukweli

    ReplyDelete
  2. Hata nyie waandishi ni wanafiki. Niliwahi kuomba nipatiwe namba za mawasiliano za klabu ya yanga hata viongozi wake au hata e mail ya klabu. Nilikuwa na ushauri mzuri ambao ungeweza kuikwamua klabu kiuchumi na ni taarifa ndefu yenye mpango mkakati mzuri lakini hukutoa ushirikiano. Na pia viongozi wa Yanga wawe wa wazi na wakubali kupokea ushauri na hata kuutekeleza. Umeongea vizuri kuhusu ngoma, kumsajili mchezaji kwa gharama kubwa halafu pesa zenyewe unakopa ili tu kuridhisha mashabiki ni upungufu wa fikra. Nipeni namba ama e mail za klabu ya Yanga. Nina ushauri mzuri sana kwao.

    ReplyDelete
    Replies
    1. Phone: +255713216125

      E-mail: info@yangasc.co.tz

      Delete
  3. Wachezaj wanajisahaulisha wengi wao wametoka vitimu vidog na mshahara mdg . wako yanga mshahara mkubwa ukikosekan mwez tu wanajifanya hawajaozea. Wametoka timu wanakul nguna na maharage huku wanapiga buffer. Mshahara ni haki na hats ukija kwa kuchelew utaupata wote he we ukifungisha ukipew mshahr utarudiaha goal. Tuwe waungwana chezen daini

    ReplyDelete
  4. Yanga wasiige simba, wajaribu kufuata mfumo wao watakao amua katika utaratibu wa uendeshaji wa klabu pasipo kutegemea atatokea tajiri wa kununua hisa kama ilivyotokea kwa simba. Bado Yanga wanaweza kuanzisha mfumo wa kampuni ambapo wanachama watamiliki hisa asilimia 51 na mwekezaji atamiliki asilimia 49, uongozi wa Yanga uitishe mkutano mkuu wa wanachama na waamue kuindesha klabu katika mfumo wa kampuni ya hisa na kila mwanachama alazimike kununua hisa ambapo hisa 1 iuzwe kwa bei ya shilingi elfu 10 na hisa za wanachama zisizidi ama kupungua asilimia 51. Zoezi la uuzaji wa hisa hizi lipewe kipindi maalum hadi kumalizika na pia linaweza kuwa endelevu, utaratibu wa kununua hisa hizi, klabu iingie mkataba na makampuni ya simu ambapo shabiki au mwanachama atanunua kupitia mihamala ya simu yake ya mkononi kwa mtandao anao utumia. Klabu italazimika kutoa au kuwa na namba maalum za simu ambazo zitasajiliwa kwa ajili ya kupokea pesa hizi. Na uwekwe utaratibu kwamba shabiki au mwanachama anapofanya huduma hii anasajiliwa kwa kupewa namba maalum ya utambulisho kwa sms. Baada ya zoezi hili klabu ya Yanga ianzishe kampuni ndogo ya bahati nasibu, kampuni hii iwe ndani ya kampuni mama ya yanga, lengo la kampuni hii ya bahati nasibu ni kuanzisha shindano la bahati nasibu kwa mashabiki na wanachama wa Yanga kama ilivyo kwa kampuni za biko, mojabet, na tatumzuka lengo likiwa kuwakutanisha mashabiki na wanachama wa Yanga kushindania pesa ambazo zitatolewa kwa mshindi wa kwanza hadi wa tatu na fedha hizi zitolewe kila mwisho wa mwezi, mshiriki atapaswa kuchangia sh 1000 na zaidi kila siku au kadri awezavyo ili kujikusanyia tiketi zaidi za kuongeza bahati ya kushinda. Kupitia shindano hili klabu ya Yanga itakuwa inajiingizia pesa kila siku ambazo kwa kadirio la chini endapo watu 1000,000 watacheza kila siku kwa sh 1000 kwa tiketi, Yanga itapata milioni 100 kwa siku ambayo ni sawa na bilioni 3 kwa mwezi. Hapo ukitoa hela ya washindi kila mwezi kama milioni 150 pamoja na kodi na gharama za uhamasishaji kwenye mitandao ya simu yote, radio na television hata ukitoa milioni 850 bado Yanga itabakiwa na bilioni 2 kila mwezi. Narudi kwenye zile hisa 49 za klabu: Yanga watafute kampuni badala ya kumtafuta mtu(binadamu), mtu ni mtu tu, anaweza kupata matatizo ama kufa na msaada wake ukaisha, waingie ubia na kampuni ya ndani au ya nje waingie nayo mkataba kuwauzia hizo hisa asilimia 49 na kampuni hiyo itakuwa mmiliki mwenza wa Yanga itahusika na kuihudumia klabu kulingana na makubaliano yao na kampuni hiyo itanufaika kutangaza huduma ama bidhaa zake kwa kupitia nembo ya Yanga.

    ReplyDelete
    Replies
    1. Kaka nashukuru sana kwa ujumbe huu nimesoma kwa makini na ninakubaliana na wewe kabisa. Thank you

      Delete
    2. Nimeipenda hii na SIMBA tafakari maoni haya kwa asilimia za hisa zilizobaki kwa wanachama na zile za MO aendelee nazo.
      Japo bado kuna wazee kina Akili Mali na Hamis Kilomoni wanafikiria soka la miaka hii litaendeshwa kwa kuchangishana kama sadaka kwa aliyenacho chochote atoe.

      Delete
  5. HAPA KUNA KITU NYUMA YA PAZIA KUNA WADHAMINI WATATU WAKUBWA SASA KWANINI WANASHINDWA KULIPA MISHAHARA? WACHEZAJI MBONA HAWAPONI MAJERAHA? KWENYE MECHI MUHIMU KWANINI NDIPO UDHURU UNAIBUKA? WALE WENYE FEDHA WAKO WAPI YANGA? NIDHAMU YA WACHEZAJI MBONA IKO CHINI NANI ANAHUSIKA NA HILI? KIBALI CHA KOCHA KWANINI MCHAKATO UMECHUKUA MUDA? USHAURI YANGA IJITOE MASHINDANONI KULIKO KUTULETEA AIBU....HIVI TUKISIKIA WANAFUNGWA 8-0 KUNA KULAUMU? HII NI HATARI SANAAA....HIVI WAPENZI WA YANGA WENGI WANAUGUA NA KUFEDHEHEKA MWAKA HUU.....KWENYE MSAFARA VIONGOZI NI WENGI 11 NA TIMU ILIYOENDA NA YOSSO 17....MNAFANYA MASIHARA NYIE MNAENDA KUCHEZA NA MABINGWA WA ALGERIA WENYE MAANDALIZI NA MASHABIKI WENYE NGUVU....MBONA KILIO TUNAKITAFUTA WATANZANIA JAMANI

    ReplyDelete
  6. tff itasaidiaje kuwapa pesa yanga?bs kila timu itapeleka mahitaji yake.mbona mtibwa alipojitoa hamkuwashauri tff wawakopeshe pesa?

    ReplyDelete
  7. tff itasaidiaje kuwapa pesa yanga?bs kila timu itapeleka mahitaji yake.mbona mtibwa alipojitoa hamkuwashauri tff wawakopeshe pesa?

    ReplyDelete
  8. Maandishi acha kuidhlilisha yanga. Hawajakuambia kuwa hawana pesa tff ikiombwa kusaidia au kukopwa kwa maandishi watafanya hivyo sio hizo chokochoko na porojo zako

    ReplyDelete
  9. Mwaandishi acha kuidhlilisha yanga. Hawajakuambia kuwa hawana pesa tff ikiombwa kusaidia au kukopwa kwa maandishi watafanya hivyo sio hizo chokochoko na porojo zako

    ReplyDelete
    Replies
    1. This comment has been removed by the author.

      Delete
  10. Nimeona Serikali kwa kutumia takukuru wameiandama Club ya simba kwa kuwakamata viongozi wake kwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha nakadhalika. Licha yakuwa tumeumizwa sana wanasimba na hatua hiyo lakini hatupingani na hatua hizo za serikali hasa kutokana imani tulionao kwa serikali ya awamu ya tano katika kupambana na ufisadi ila hatuamini kuwa viongozi wa SIMBA peke yake ndiko kwenye matatizo? Ukiangalia pale Yanga utagunduwa yakuwa ile club si ya kutembeza bakuli kuomba pesa lazima kutakuwa na wizi unatendeka. Yanga wana viongozi wa hovyo wanayoiangamiza ile club. Kwa upande mwengine serikali inatakiwa kutozipa mgongo hizi club kwani kwa kufanya hivyo ni kuwabeza waasisi wetu. SIMBA na Yanga zimefanya kazi kubwa ya kuwaunganisha watanzania wa dini zote,wa makabila yote,wa rangi zote, wajinsia zote nakadhalika. Kama hayati Karume angelikuwa hai kamwe asingekubali kuona hizi timu zinakuwa nyonge. Sisi wadau wa soka bado hatujaridhishwa na jinsi mambo yanavyokwenda katika mpira wetu mpaka sasa kwani tunaimani kabisa licha ya kuleta burudani michezo ni industry na kwa kiasi kikubwa ina nafasi ya kuchangia maendeleo ya nchi na kudhalisha ajira.

    ReplyDelete
  11. Mashabiki wa Yanga hata siku timu yao ikicheza wanaenda uwanjani wachache...Mfano mzuri ni wakati timu yao inacheza na township rollers..Simba walipocheza na waarabu walienda mashabiki wengi kuishangilia...hata juzi simba na yanga..Mashabiki yanga hawakuwa wengi kama simba.. Mapato yanakuwa kidogo endapo hawaendi kushangilia uwanjani

    ReplyDelete
  12. Kwa mara ya kwanza nimeona watu wakitoa maoni yao kwa njia ya kujenga na wala si kubomoa tena wote kwa pamoja, hata kama mtu anakosoa tuheshimu mchango wake. Lazima kuwe na utatuzi wa kudumu, inasemekana Yanga ina mashabiki wangi nchini mbona hii ni rasilimali kubwa sana jamani, nembo ya yanga ni kubwa sana (yaani goodwill) tunaweza kuendesha club kwa kuanzia hapo tulipo tusinie makuu ambayo hatuwezi kuyatekeleza. Lazima viongozi watoke nje na kusema hali halisi ya club watu hawachangii kwa sababu viongozi hawatuelezi hali halisi ya club na kutupa njia ya kufanya na ndio maana kamili ya kuuitwa kiongozi. Tuanze na hapa chini tulipo, tuwalipe wachezaji wetu kwa kile kitakachopatikana na, punguza matumizi kwa kuachana na gharama za wachezaji ghali wasio na msaada. Tutumie nembo yetu kibiashara. Ina uuma sana

    ReplyDelete
  13. kuzi mechi ya simba na yanga tunaambiwa imevunja rekodi ya mapato zimepatikana milioni 376, yanga wana udhamini wa sportpesa bado azam tv, vodacom na pia tuliambiwa wameingia mkataba wwenye thamani ya bilioni mbili kwa ajili ya mauzo ya jezi
    Tatizo la kwanza yanga walibweteka kwa pesa za Manji sijui siku akiibuka na kuanza kuidai yanga itakuwaje
    Pili wapenzi na wanachama wanakosa moyo wa kuchangia kutokana na kutokuwa na uwazi wa mapato na matumizi kila siku mkutano mkuuu unaarishwa watachangiaje wakati wanaamini klabu ina mapato ila yatakuwa yanaliwa na wachache
    Pia wale wanaouza jezi za yanga mapato yanaenda wapi tuanzie hapo?

    ReplyDelete
  14. Maafa haya yamekuja huku ligi iko ukingoni lakini ingekuwa mwanzoni ingeweza hata kushuka daraja. Manaake imefika hadi hata hata viongozi wanaingia mitini na wakopigiwa simu hawapokei na Mkemi masikini ndio katupiwa kila kitu. Masikini Yanga

    ReplyDelete
  15. Tatizo lipo kwenyetimu.kwanimpaka sasa timu haina uongozi inaendeshwa kiujanjaujanja toka manji aondoke hakuna mwenyekiti kwahiyo hakuna mwenyekuleta ushawishi wa watu kuja kufanya biashara pale.viongozi walio kuwepo siwakweli kilajambo ukiuliza wanakataa mpka limesha washinda ndio wanaleta siasa

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic