Baada ya kuonesha kiwango kizuri kwenye msimu uliomalizika wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2017/18, mchezaji wa Yanga, Emmanuel Martin, inaelezwa anahitaji katika klabu ya Waasland Beveren inayoshiriki Ligi Kuu Ubelgiji.
Taarifa zilizo chini ya kapeti zinaeleza kuwa mabosi wa Beveren tayari wameshatuma watu wao waliopo ndani ya Afrika Mashariki kusaka vipaji ukanda huu huku ikielezwa pia wanafanya mazungumzo na Yanga kumnasa mshambuliaji huyo.
Martin ambaye amekuwa sehemu muhimu ya kikosi cha Yanga haswa katika safu ya ushambuliaji ya timu hiyo, ameingia kwenye rada za Wabelgiji hao ikiwa ni wiki kadhaa zimesalia kuelekea mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika.
Mpaka sasa wachezaji wote wa Yanga wapo likizo na mapema pindi watakaporejea wataanza kujiandaa kukipiga na Gor Mahia ya Kenya ambapo mechi itachezwa Julai 18 huko Nairobi.
Endapo mipango ya Wabelgiji hao itafanikiwa kumnyakua nyota huyo itabidi Yanga wajipange upya kujaza nafasi yake haswa katika wakati huu wachezaji wengi wa kikosi hicho kutokuwa na mikataba.
Ikumbukwe kuwa Mtanzania, Mbwana Samatta naye anakipiga nchini humo katika klabu ya KRC Genk, hivyo endapo dili la Martin kuelekea huko litatiki atakuwa anaungana na Samatta kuendeleza soka lake nchini humo.
0 COMMENTS:
Post a Comment