June 22, 2018








Na Mwandishi Wetu
TAMASHA la Majimaji Selebuka limekuwa likifanyika kila mwaka katika Mkoa wa Ruvuma na kushirikisha mambo mbalimbali yanayokwenda kwa mzunguko.

Tamasha hilo linahusisha shughuli mbalimbali za michezo, sanaa, biashara na elimu, jambo ambalo linalifanya tamasha hilo kuwa kubwa zaidi kuliko mengine yote ambayo yanafanyika kwenye Ukanda wa Nyanda za Juu Kusini.

Huu ni mwaka wa nne tamasha hilo linafanyika. Mwaka huu lilianza Juni 14 na litafikia tamati Julai 21. Ndani yake kuna mambo ambayo inawezekana si rahisi kuyapata katika matamasha mengine.


Huenda wahusika wamekuwa hawalitangazi sana, lakini ni tamasha ambalo Watanzania wengi wangependa kulisikia na ikiwezekana kuhudhuria kwa ajili ya kujifunza.

Inawezekana kabisa kwa serikali nayo kutia nguvu katika tamasha hilo ambalo linawezesha vitu mbalimbali kufanyika kwa wakati mmoja na faida kubwa ipo kwa jamii ya Watanzania.

Angalia hivi; Kwa upande wa michezo, awali kulikuwa na riadha na mashindano ya baiskeli jambo ambalo limegeuka kuwa burudani kuu kwa Wanaruvuma au Wanasongea.

Awali, halikuwa jambo rahisi kuona kuna mashindano ya baiskeli au riadha. Sasa kuna vipaji vimeibuliwa mkoani humo lakini hata nje ya mikoa hiyo na imefanya watu wengi kufika mkoani humo.

Hii ni pamoja na mashindano hayo ya baiskeli ambayo wapo wanaopenda kuendelea baada ya kushiriki kwa mara ya kwanza katika mashindano ya Majimaji Selebuka. Inawezekana ukawa mwanzo wa kutaka kuendeleza na kuzifikia ndoto zao.

Safari hii, mchezo wa soka umeongezwa, mambo yanaanzia kutokea kwenye kata kwenda juu. Inawezekana kabisa timu kama Majimaji au JKT Mlale zinaweza kupata vipaji vitakavyowasaidia.

Vipaji hivyo vitaonekana katika mashindano ya msimu huu ambayo yameanzia chini kabisa “mavumbini” ambako awali kusingepewa heshima au nafasi ya kuonekana, jambo ambalo pia linaonyesha tamasha hilo linatengeneza njia kwa wale waliokuwa wamekata tamaa wakati wana uwezo wao.

Wataweza kuonekana kwa timu za mkoa huo na kama watajiendeleza wana nafasi ya kufanya vizuri mbele na katika timu kubwa zaidi. Sote tunajua Ruvuma ni kati ya mkoa wenye vipaji katika michezo, soka ukiwa mmoja wao.

Katika sanaa, Majimaji Selebuka imetoa nafasi kubwa na kuutangaza mkoa huo kitalii na utamaduni pia. Awali ilionekana ngoma za asili za makabila ya mkoa huo ni jambo la kawaida sana.

Lakini sasa vikundi mbalimbali vinashindanishwa na mwisho wanapatikana washindi wanaopewa zawadi. Washiriki wanataka kushinda zawadi mwishoni, hivyo kila upande unatoa burudani ya uhakika ili kuweza kushinda mwishoni.

Ukipata nafasi ya kuhudhuria tamasha hilo, sasa kuna masupa staa wa tamasha hilo kwa maana ya watumbuizaji, jambo ambalo linaleta raha.

Hii inasaidia kuliko kuwaacha watumbuizaji hao wakitumbuiza kwenye harusi pekee bila ya kupewa thamani ambayo itawaonyesha wakifanyacho ni kitu kizuri na tayari wamekuwa wakipewa sapoti.

Ruvuma ni mkoa wa kina mama wachapakazi. Wengi ni wakulima, wachuuzi na wafanyakazi. Wengi hasa wafanyakazi wamekuwa na uhakika wa mshahara, lakini wachuuzi hawawezi kuwa na uhakika sana.

Majimaji Selebuka inawatengenezea sehemu ya kuuza na kutangaza biashara zao. Hili jambo jema kabisa ambalo linapaswa kuungwa mkono.

Ukifuatilia utagundua wajasiriamali wengi ambao wanauza bidhaa zao baada ya kuzitengeneza ni akina mama ambao wanahitaji kuungwa mkono kwa kiwango cha juu kabisa.


Mwendo wa Majimaji Selebuka unaonekana kupaa na kuwa msaada kwa Mkoa wa Ruvuma ukianzia Songea mjini na kuunganisha na vijijini.

Waandaaji wanaweza wasiwe na nguvu sana kutokana na ukubwa wa tamasha. Maana yake wanahitaji msaada wa kuungwa mkono kuanzia serikalini hadi katika sekta binafsi.

Tamasha lao linahusisha watu, hivyo linatengeneza faida kwa wananchi ambao ni rafiki wa serikali na sekta binafsi. Maana yake, waandaaji wanapaswa kuungwa mkono ili wafanikishe lengo la yale ambayo wameyapanga.



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic