June 22, 2018


NA SALEH ALLY

BEKI wa zamani wa Yanga, Shadrack Nsajigwa amemaliza mkataba wake na klabu ya Yanga na mwisho ameamua kuondoka zake.

Nsajigwa ameondoka si kwamba alikuwa amepanga au alikuwa anapenda kuondoka na kuachana kabisa na klabu hiyo kama alivyofanya.

Inawezekana anaweza kusema aliamua kufanya hivyo, lakini ukweli wa mambo unaonyesha angekuwa tayari kuendelea hasa kama kungekuwa na upendo na uungwana.

Mfululizo kwa zaidi ya miezi mitatu, mashabiki wa Yanga walikuwa wakimsakama Nsajigwa akionekana kama alikuwa ni tatizo na wengi walipaza sauti aondoke.

Waliopaza sauti, wengi walikuwa ni fuata mkumbo, si wachunguzi wa mambo na wasio na subira ya kutafakari. Mwisho ameshindwa, Nsajigwa ameondoka na hakika binafsi bila ya kona niseme alichofanyiwa si sahihi lakini ni mafunzo makubwa sana katika maisha yake kama kocha wa mpira, nitakuambia kwa nini.

Nsajigwa hakuwa ameiva katika kiwango cha kutosha, lakini alipata nafasi nzuri kuwa chini ya makocha wa kimataifa wa Yanga kwa kuwa aliaminika na anakuwa pale kama mwakilishi wa klabu.

Yanga wanakuwa na kila sababu ya kumtumia mtu kama yeye, nahodha wa klabu kwa zaidi ya misimu sita, mtu aliyejituma na kupambana kwa ajili ya klabu yake.

Ingawa amepata mafunzo kama kocha, lakini angeweza kujifunza zaidi akiwa anafanya kazi katika klabu kubwa kama Yanga na chini ya makocha wakubwa mfano wanaotokea Ulaya au nchi za Afrika zilizopiga hatua kuliko nyumbani Tanzania.

Halikuwa wazo baya kumpa Nsajigwa nafasi hiyo, lakini kelele zisizo na mashiko zimemuondoa. Nafikiri kwake ni faida kubwa kwa kuwa kama anataka kuendelea kuwa kocha mwenye mafanikio hapo baadaye basi ni lazima ajue anatakiwa kujifunza zaidi ya hapo alipofikia.

Kujifunza na kuwa bora kunataka mambo mengi lakini mawili makubwa ambayo ni kufanya mambo kwa vitendo lakini kuendelea kufanya tena na tena, yaani kupata uzoefu ambao baadaye unakuwa msingi wa juu unapozungumzia suala la utendaji.

Kama Nsajigwa atakuwa anata kujiendeleza zaidi huu sasa ni wakati mwafaka na sahihi kwake. Wakati mwingine napenda watu wanidharau ili niwe na hamu ya kujifunza na kujua vitu zaidi ili siku nyingine nije nifanye kwa usajili mkubwa kabisa na kuwaonyesha hawakuwa sahihi kunidharau.

Waliomdharau Nsajigwa hawakuwa na hoja za msingi zaidi ya lawama pofu ambazo hazikuwa hata na maana. Najua atakuwa ameumia kama mwanadamu kwa kuwa wakati wakipiga kelele, hakuna aliyelilia apewe madai yake, mfano hakulipwa zaidi ya miezi kadhaa na akaendelea kufanya kazi kwa juhudi kila kukicha.

Kikubwa ni kujifunza zaidi na ikiwezekana kwa kipindi hiki Nsajigwa anapaswa kufundisha timu ambayo anaamini ataiongoza vizuri na kupata mafanikio.

Bila ya kujali ligi daraja la kwanza au la pili, Nsajigwa anapaswa kuonyesha mafanikio kama ambavyo leo tumeona kwa makocha kadhaa kama Fred Felix Minziro, ambaye pia aliwahi kuwa kocha msaidizi Yanga na mwisho akaonekana hafai.

Unapokuwa na mlima wa changamoto na ukachukulia chanya, basi ni rahisi kubadilika wakati ukifunza na kuwa bora zaidi. Nsajigwa ana nafasi hiyo na ilikuwa lazima aondoke Yanga ili kupata nafasi ya kuonyesha alichonacho.

Sasa ndiyo wakati mwafaka wa yeye kuanza kuinuka akiwa nje ya Yanga na siku nyingine ikiwezekana Yanga wamuite tena na safari ya pili watakuwa wamejifunza kuhusiana na thamani ya utu wake.

Kama ikifikia siku anarejea Yanga, basi Nsajigwa atakwenda kama mtaalamu anayekubalika na ataweza kufanya kazi yake vizuri bila ya hofu.

Kwa Nsajigwa, huu ndiyo wakati mwafaka na anapaswa kuutumia haswa ili kujifunza zaidi. Waliomzodoa wasimkatishe tamaa, waliomlaumu awatumie kama changamoto na chachu na siku moja ataweza kuwashangaza.





0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic