Na George Mganga
Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) limefungua rasmi dirisha la usajili kwa msimu wa 2018/19 huku awamu hii ukija na mfumo tofauti ukilinganisha na ilivyokuwa mwanzo.
Usajili wa awamu hii utakuwa wa kitofauti ambapo utatumia mfumo mpya ujulikao kwa jina la TFF FIFA CONNECT.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa TFF, Clifford Mario Ndimbo, amesema mfumo huu utafafanuliwa kinagaubaga kupitia semina ambazo zitafanywa mbele ya viongozi wa klabu zote za Ligi Daraja la Kwanza, Pili na Ligi Kuu.
Ndimbo ameeleza kuwa semina hizo zitaanza mapema kabla ya kuanza kutumika ili kutoa uelewa juu ya namna unavyopaswa kutumika kwa timu zote husika ambapo semina hizo zitaanza na timu zinazoshiriki Ligi Kuu Bara Jumatatu ya ya Juni 25 2018.
Baada ya timu za Ligi Kuu, semina hiyo itaendelea tena kesho yake itakayokuwa Jumanne kwa zile za Daraja la Kwanza na keshokutwa yake Jumatano, zinazoshiriki Ligi Daraja la Pili zitahusika kwenye semina.
Kufuatia mabadiliko hayo ya mfumo wa usajili, Ndimbo amesema baada ya usajili huo, kutakuwa na wiki moja ya mapingamizi endapo yatakuwepo ambapo klabu zinatawasilisha kupitia kamati maalum itakayosimamia suala la usajili.
Mbali na hayo, Ndimbo amewaomba viongzozi wa klabu zote kuzingatia muda wa mafunzo juu ya mfumo huo mpya ili kuepusha matatizo ambayo yanaweza yakajitokeza baadaye.
Ikumbukwe dirisha la usajili tayari lilishafunguliwa tangu Juni 15 2018, saa 6 na dakika 1 usiku na klabu zote zinaruhusiwa kufanya usajili wa wachezaji.
0 COMMENTS:
Post a Comment