June 16, 2018




Na Saleh Ally
KWA sasa mashabiki wa soka wameelekeza nguvu zao katika Kombe la Dunia linaloendelea huko Urusi. Kila mmoja anajaribu kufurahia, kufanya biashara na kadhalika.

Kocha Mkuu wa Arsenal, Unai Emery ni raia wa Hispania, bila shaka atakuwa katika harakati za kuhakikisha anaishangilia nchi yake ifanye vizuri na raha zaidi ilianza kampeni za kuwania ubingwa dhidi ya Ureno, jana.

Pamoja na kwamba Emery lazima aangalie na kufurahia Kombe la Dunia, lakini atakuwa kazini akiendelea na mambo mengine kuangalia anaoweza kuwapata kwa ajili ya msaada katika kikosi chake kwa msimu ujao wa Ligi Kuu England.



Msimu wa 2018/19 unaanza Agosti 11 na Emery tayari presha imekuwa juu kwake kuzidi mara mbili. Inakuwa kuzidi mara mbili kwa kuwa tayari alikuwa na presha mara tu baada ya kusaini mkataba wa kuinoa Arsenal.

Kuinoa Arsenal baada ya Arsene Wenger aliyekaa miaka 22, si jambo la kawaida. Vita ya kumuondoa Wenger ilikuwa kubwa, mlima wa lawama na anayechukua maana yake ni tumaini jipya.


Atafanya kipi aonekane ni tofauti na Wenger na mashabiki wanaweza kumpa muda wa kumvumilia? Wakati swali hilo halijajibiwa, Premier League wameamka na kitu chao, nacho ni ratiba.

Ratiba mpya ya Ligi Kuu England msimu mpya wa 2018/19 imetangazwa. Wakati ratiba inatangazwa inaonekana wiki mbili za mwanzo za ligi hiyo, zitakuwa ni kama kiama kwa Emery.
Watoto wa mjini wanasema, “mtamtoa roho”. Maana wakati inaanza mechi ya kwanza Arsenal imepata bahati ya kuwa nyumbani Emirates lakini msala inaonekana ni timu itakayoanza nayo.

Inaanza na mabingwa watetezi Manchester City, katika mechi ambayo itakuwa ni ya kwanza ya EPL, Emery akikaa katika benchi.



Angalia, Man City wanajulikana kwa ukali wao, kikosi chao na walivyofanya msimu uliopita. Tena wataingia dimbani wakiwa wamejiboresha. Emery atakuwa anataka kuwafunga Manchester City lakini akiwa na presha kubwa kwa kuwa mechi itakuwa nyumbani.

Mashabiki wangependa kumuona anashinda kwa mara ya kwanza akiwa Emirates. Wangependa kujenga imani naye kama atafanikiwa kushinda mechi hiyo ya kwanza.

Lakini pia, yeye angependa kuwaonyesha mashabiki anaweza ili kupunguza moto katika kiti chake pale Emirates na kwingine atakapokuwa akiiwakilisha Arsenal.

Mechi ya kwanza itakuwa dhidi ya mabingwa watetezi Manchester City na hapa itakuwa ni kushinda na ikishindikana angalau kutafuta sare au kuwa makini kuzuia kipigo kikubwa kinachoweza kuondoa morali ya wachezaji wake.

Wiki inayofuata, siku saba baadaye watabaki jijini London lakini watasafiri takriban kilomita 10 kwenda upande mwingine wa jijini hilo katika Uwanja wa Stamford Brigde.

Utaona hapa, ndani ya siku 14, Emery atakuwa ameshakutana na timu mbili zenye uwezo wa kuwania au kubaki katika Top 4.
Haitakuwa kazi rahisi kwake ingawa bado mambo yanaweza yakawa tofauti na wengi tunavyofikiria maana kunaweza kuwa na faida.

 FAIDA:
Kama Arsenal chini ya Emery itapoteza mechi hizo mbili, basi ujue atalazimika kufanya kazi kubwa na ya ziada kuhakikisha anairudisha timu katika mwendo sahihi katika mechi yake dhidi ya West Ham ambayo pia haitakuwa nyepesi kutokana na upinzani wa Jiji la London.

Lakini ikitokea Emery akashinda mechi zote mbili dhidi ya Man City halafu Chelsea, maana yake atatengeneza mambo mawili makubwa ndani ya kikosi chake.

Kwanza ni hali ya kujiamini kwa wachezaji wake kwamba wamemtandika bingwa mtetezi wa msimu uliopita ambaye ni Man City halafu wakamtandika bingwa aliyepita kabla ya Man City. Maana yake wao ndiyo wanastahili kuwa mabingwa.

Pili, ni suala la hali ya kujiamini kwa wachezaji wake, kwamba wamewafunga mabingwa wa misimu miwili, sasa nani watamshindwa!

Hivyo pamoja na kuonekana ni kama jambo gumu sana kwa Emery, upande wa pili EPL wanaweza wakawa wamemtengenezea ulaini ambao utamfanya akae sawa na kufanikiwa.

Inategemea atazicheza vipi karata zake. Akizicheza vizuri katika mechi hizo mbili, maana yake ana nafasi ya kuwa mfalme mpya wa Ligi Kuu England.

MECHI:
JUMAMOSI AGOSTI 11,2018
Arsenal v Man City

JUMAMOSI AGOSTI 18, 2018
Chelsea v Arsenal

JUMAMOSI AGOSTI 25, 2018
Arsenal v West Ham
JUMAMOSI SEPT MOSI 2018
Cardiff City v Arsenal

KLABU ALIZOCHEZEA
MSIMU    KLABU  MECHI  MABAO
1990–1995 Real Sociedad B 89 (7)
1995–1996 Real Sociedad 5 (1)
1996–2000 Toledo 126 (2)
2000–2002 Racing Ferrol 61 (7)
2002–2003 Leganés 28 (0)
2003–2004 Lorca Deportiva 30 (1)
JUMLA 339 (18)

MATAJI ALIYOCHUKUA
Sevilla:  Europa League 3: 2013–14, 2014–15, 2015–16

Paris Saint-Germain
Ligue 1: 2017–18
Coupe de France : 2016–17, 2017–18
Coupe de la Ligue: 2016–17, 2017–18
Trophée des Champions: 2016, 2017


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic