Mshambuliaji mwenye rasta ambaye mbali na kipaji chake cha mpira anapenda kutupia mavazi yanayokwenda na wakati, Adam Salamba, amesema kuwa lengo lake ni kuhakikisha anaweza kuweka rekodi safi katika timu yake ya Simba.
Salamba alisema anatambua kazi kubwa iliyopo kwa sasa ni kuhakikisha anaweza kuonyesha uwezo wake kwa kusaidiana na wenzake kwa kuwa mafanikio ya mpira yanategemea timu.
“Nipo katika timu bora ambayo imekamilika katika kila idara, hivyo ni fursa kwangu kuweza kushirikiana na wenzangu ili kuweza kuweka rekodi nzuri kwa kuisaidia timu kupata matokeo mazuri kwa kuwa hiyo ni kazi kubwa ya mchezaji.
“Ushindani wa namba hilo siyo jambo la kuhofia kwa kuwa natambua kuwa timu imedhamiria kufanya mambo makubwa kwa ajili ya mashabiki hivyo ni lazima wawepo wachezaji wazuri kama ilivyo sasa, mapambano ni jambo la msingi pamoja na kuzidi kumuomba Mungu atulinde kwa kuwa yeye ndiye muweza wa yote,” alisema Salamba.
Salamba ni mshambuliaji mpya ambaye amesajiliwa na timu ya Simba akitokea Lipuli, na sasa anakuwa pamoja na washambuliaji wengine ambao ni Mohamed Rashid, Marcel Boniventure Kaheza, Meddie Kagere na kwa upande wa makipa ni Deogratius Munish ‘Dida’ ikiwa ni usajili wa awali.
CHANZO: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment