Kamati ya Usajili ya Yanga ambayo inasimamiwa na mwenyekiti wake wa muda, Abass Tarimba, imepindua meza kibabe baada ya kumfuata kiungo Feisal Salum ‘Fei Toto’ wa JKU na kumwambia aachane na mpango wa kutua Singida United kisha ajiunge na wao.
Fei Toto amekuwa akifuatiliwa kwa ukaribu na timu hizo mbili ambazo zinapigana vikumbo kuwania saini yake huku taarifa zikiweka wazi kwamba Singida United wapo katika hatua nzuri ya kumalizana na kiungo huyo.
Chanzo makini kutoka Yanga kimeliambia Championi Jumatatu, kuwa viongozi wa timu hiyo walimfuata Feisal baada ya kutua Dar es Salaam na kikosi chake kwa ajili ya Kombe la Kagame ambapo walizungumza naye kwa ajili ya kumsajili huku wakimwambia aachane na Singida United ambao walikuwa tayari wameshampa mkataba wa awali.
“Yanga kwa sasa wameonyesha wapo siriaz juu ya Feisal baada ya Ijumaa iliyopita kumuibukia mazoezini katika Uwanja wa Karume, Dar na kuzungumza naye kwa kutaka kumsajili na kuna kigogo mmoja (anamtaja jina) ndiye aliyeenda mazoezini hapo na kuzungumza naye kwa muda mrefu.
“Yanga wanataka kumsainisha kiungo huyo, kwani wamesikia kwamba Singida United tayari wameshampa mkataba wa awali lakini wao wanataka kuuvunja na watatoa milioni 40 ambazo zitatumika kwa yeye Feisal kuwarudishia Singida fedha zao walizompa awali.
“Kuna uwezekano mkubwa wa dili hilo kufanikiwa kwani Yanga wanaongea na Mwigulu Nchemba ambaye ndiye aliyehusika na usajili wake Singida kwa ajili ya kumalizana na kisha msimu ujao kiungo huyo avae jezi za Yanga,” kilisema chanzo hicho.
Championi Jumatatu, lilimtafuta Feisal ambapo alipopatikana alisema: “Kweli kuna kiongozi wa usajili Yanga alikuja uwanjani na akazungumza na mimi juu ya usajili wangu.
“Mimi sijajua wapi nitacheza kwa msimu ujao kwani kweli nimesaini mkataba wa awali Singida United lakini Yanga wanataka kuwarudishia fedha, kama suala hilo watakubaliana wenyewe mimi nipo tayari kwa ajili ya kwenda Yanga.”
Pia Championi lilimtafuta Katibu wa JKU, Sadu Hujud Maalim ambapo alisema: “Sisi hatujaiona timu yoyote ile ambayo imemfuata Feisal kati ya hao Singida au Yanga, tunachojua sisi bado ana mkataba wa miaka miwili wa kututumikia na kama timu itakuwa inamtaka basi lazima ije kuonana na sisi.”
CHANZO: CHAMPIONI
Huu ni uongo....wanataka kuuza gazeti tu
ReplyDeleteHuyu mjinga anaaendika uongo kama huu. Yanga wanaweza kuwa na akili mbovu kama hizo kweli. Kama mtu ameshapewa mkataba Yanga watawaingiliaje Singida. Acha ujinga umesema mengi ya kipuuzi ili uuze tu habari.
ReplyDelete