July 5, 2018




KESHOKUTWA Ijumaa huenda itakuwa siku ambayo Kombe la Dunia litazidi kunoga pale timu tatu kati ya zaidi ya tano zilizokuwa zikipewa nafasi ya kuchukua ubingwa zitakuwa dimbani tena.

Baadhi ya zile ambazo zilipewa nafasi ya kulibeba kombe hilo ni pamoja na Ujerumani ambao safari tayari imewakuta kama ilivyo kwa Hispania, Argentina na hata Ureno walionekana wangeweza kufika angalau fainali, safari pia imewakuta.
Timu chache zimebaki ambazo zilipewa nafasi hiyo na zimeendelea kuvumilia ndani ya Kombe la Dunia lenye ‘supraizi’ kibao. Leo tatu zote zitakuwa kazini.

Brazil, Ufaransa na Ubelgiji. Ufaransa iko kazini kuivaa Uruguay ambayo imewarudisha nyumbani Ureno na Ubelgiji watakuwa wakicheza dhidi ya Brazil, mechi ambayo nimelenga kuizungumzia.
Ukiangalia mechi hizo mbili, pamoja na mambo mengi, kuna suala la mabara. Mechi zote mbili zinakutanisha timu kutoka Ulaya na Amerika Kusini. Inaweza ikawa Ulaya au Amerika Kusini pekee au kukawa na mgawanyiko.
Brazil wanaingia wakiwa wamefanikiwa kuwafunga Mexico kwa mabao 2-0 katika mechi ‘super’ ya hatua ya 16 bora na wakafuatia Ubelgiji ambao walifanya maajabu na kuvunja rakodi iliyokaa tokea mwaka 1970 katika Kombe la Dunia lililofanyika Mexico.

Mwaka 1970, ilikuwa mechi ya robo fainali, Ujerumani ilikuwa nyuma kwa mabao 2-0. Ikafanikiwa kusawazisha na kufunga la ushindi hivyo kuiangusha England kwa mabao 3-2 na kutinga nusu fainali. Juzi, Ubelgiji walikuwa nyuma kwa mabao 2-0, kabla ya kusawazisha na kumaliza kazi.
Keshokutwa Ijumaa ni mambo mapya kabisa. Halitakuwa pambano la kumbukumbu sana kwa kuangalia walivyovuka tu. Lakini itategemea pia kila mmoja atafanya vipi siku hiyo.

Ubelgiji:
Inakutana na Brazil tayari ikiwa imefunga mabao 12 katika mechi zake nne kuanzia tatu za makundi na moja ya 16 bora. Maana yake ni timu inayoweza hasa kufunga.
Brazil lazima wajilinde zaidi na kuendelea kucheza ule mchezo wao wa ‘kaunta ataki’ kwa kuwa Ubelgiji wanaweza kuitoboa difensi ya aina yoyote kwa kuwa wameweza kufunga mabao matatu ndani ya dakika 30 dhidi ya Japan, timu yenye nidhamu ya hali ya juu.

Hii maana yake nini? Kama Brazil watacheza “open football” na kuwaachia Wabelgiji kuingia mara nyingi ndani ya 18 yao, au hata kuisogelea kutakuwa na madhara mengi.

Wana wachezaji wenye “akili timamu” kama Eden Hazard, Romelu Lukaku, Yannick Carrasco, Kevin De Bryune, Dries Mertens na Nacer Chadli ambao wanaweza kuamua matokeo nje ya mfumo.
Pia, madhara hayo yatatokana na mashuti kwa kuwa Ubelgiji ina zaidi ya wachezaji wanne wa mbele wenye uwezo wa kupiga mashuti wakiongozwa na Hazard na De Bruyne pia ni wazuri kulenga.
Kitu kibaya zaidi kama wataruhusu krosi na inaonekana kuwa silaha kuu ya Wabelgiji kwa kuwa waliitumia kuwamaliza Japan na hasa kwa mipira ya juu kwa kuwa wana wachezaji wenye maumbo makubwa kama Lukaku, Mertens, Fellaini na Chadli ambao wawili hawa waliingia na kuwa tatizo kubwa.

Katika kiungo hasa kuanzia nyuma, Axel Witsel anaweza kuwa Brazil wakati mgumu kwa kuwa Ubelgiji wanamtumia kupanga mashambulizi na kuitikisa timu, lazima kuanza kumvuruga yeye.

Mechi waliyoshinda 3-2 dhidi ya Japan ni tatu katika Kombe la Dunia 2018, wakishinda mabao matatu au zaidi. Katika hatua ya makundi walianza kuichapa Panama 3-0 na mechi ya pili wakaivurumisha Tunisia kwa 5-2.

Hii maana yake ni hivi. Ubelgiji inapokutana na Brazil, ina uhakika wa asilimia 90 kupata bao moja au zaidi na lazima Brazil wahakikishe nao wanafunga mabao zaidi ya moja, la sivyo watakuwa wamejitengenezea safari.

Ukiachana na hivyo, Ubelgiji imeonyesha ina moyo wa chuma. Kurejesha bao mbili na kufunga la ushindi si jambo dogo katika Kombe la Dunia, ndiyo maana rekodi ilibaki tokea mwaka 1970 na haikuvunjwa.

Kwa Brazil hiyo ni kengele, kwamba wakifunga mabao mawili bado hawako salama kwa kuwa Wabelgiji wana uwezo wa kuja kasi na kurudisha mabao hayo, jambo ambalo halitakuwa geni kwao.
Brazil:
Katika mechi zake nne hatua ya 16 bora, Brazil imetikisa nyavu mara saba, sare ya 1-1 dhidi ya Switzerland, ushindi wa 2-0 kwa Costa Rica, pia 2-0 dhidi ya timu ngumu ya Serbia kabla ya kuitwanga Mexico kwa idadi hiyo.

Kama utazungumzia kasi ya ufungaji mabao maana yake Ubelgiji wako juu zaidi lakini Brazil wanaonekana kuwa na safu ngumu zaidi kwa kuwa wamefungwa bao moja tu katika mechi nne. Wakati Ubelgiji wao wameruhusu nyavu zao kuguswa mara nne.

Safu ya ulinzi ya Brazil inaonekana kuwa makini lakini inakutana na Ubelgiji ambayo ni kiwembe. Kitaalamu hapa ni suala la umakini na makosa ndiyo litatawala. Beki ikifanya uzembe, ushambulizi ukawa makini basi wameumia. Lakini walinzi wakiwa makini, wanaweza kuwa waokozi na hapa kikubwa ni suala la kupunguza makosa kwa zaidi ya asilimia 85.

Hata hivyo, safu ya ulinzi ya Brazil inaweza ikawa presha kubwa kwa upande wa Ubelgiji ambao wana wachezaji wazoefu na wengi wao wanacheza zaidi kwa mfumo wa Ulaya.

Mfumo wa Ulaya ni nguvu na ubora katika kupiga kichwa mipira ya juu. Watakutana na samba ya Kibrazil kwa kuwa wanacheza zaidi chini, wana mbwembwe, wepesi kuanguka na wana ufundi mwingi.
Kuwakaba wachezaji aina ya Gabriel Jesus, Willian, Neymar, Coutinho na Firmino, unalazimika kuwa makini sana kwa kuwa wahusika kama hawajasababisha madhara, ni rahisi kusababisha penalti.

Uchezaji wa nguvu wa Ulaya na kuwa na miili isiyonyumbulika sana ni nafasi nzuri kwa Brazil kuwa na faida ya mambo mawili. Kupata nafasi ya kufunga au kusababisha faulo.
Brazil wakipata mkwaju wa adhabu nje ya 18, wana wapigaji zaidi ya wawili ambao wanaweza kuwa na uhakika wa kufunga angalau kwa asilimia 80.

Safu ya ulinzi ya Ubelgiji nayo ina wachezaji wakongwe lakini inaonekana watasumbuliwa na kasi ya Brazil yenye wachezaji wengi vijana wana uwezo wa kufanya mambo mengi kama kufunga, kutoa pasi ya bao au mashuti ya kushitukiza.

Haitakuwa mechi laini kama wengi wanavyoiona na ubora katika umakini kwa kila upande unaweza kuwa dawa ingawa kasi ya ushambuliaji wa Brazil inaweza kuwapa wakati mgumu Wabelgiji na wasipokuwa makini basi wataanguka.

Kama Ubelgiji watacheza 4-3-3 na kubaki wengi nyuma wanaweza kufanya vizuri na kuizuia Brazil kukosa nafasi  ya kufanya mashambulizi “mkimbio” ambayo wameonekana kuyatumia katika mechi zote zilizopita.

Mechi hii ni tamu zaidi kuangalia kwa kuwa hakuna aliye salama tokea inapoanza hadi inafikia ukingoni.

Lakini bado itakuwa na ufundi mwingi na uamuzi wa matokeo utatengenezwa na mambo mawili makubwa. Kwanza ubora wa mfumo lakini ubora wa wachezaji hasa wale ambao wanaweza kuamua matokeo kupitia uwezo wao binafsi, nje ya mfumo.




0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic