July 6, 2018







NA SALEH ALLY
KAMA unakumbuka, Agosti mwaka jana, Wallace Karia na timu yake walifanikiwa kuibuka na ushindi na kuingia madarakani.

Sasa Karia ndiye Rais au ‘baba’ wa soka hapa nchini, mchezo ulio na fedha nyingi lakini umejaa madudu kibao.


Asilimia kubwa ya viongozi ambao wamekuwa wakiingia madarakani katika shirikisho hilo, binafsi nimekuwa nikiwaona hawana nia njema na wengi wanaingia kwa ajili ya kujifaidisha wao.

Nasema hivyo kwa kuwa nimekuwa nikiandika na kufuatilia mienendo ya shirikisho tokea lilipoanzishwa. Kabla, tulikuwa tukifuatilia kwa ukaribu kuhusiana na Chama cha Soka Tanzania (Fat).
Fat kilikuwa ni chama kilichooza, chama chenye viongozi wengi wazandiki waliokuwa wakifanya kazi pale kwa ajili ya manufaa yao binafsi na si mpira wa Tanzania.

Wachache sana waliofanya kazi Fat leo wanaweza kusema waliutetea mpira wa Tanzania. Waliobaki walijifaidisha wao na hadi leo wameacha makovu makubwa katika mpira. Bahati mbaya hawajitambui wamekuwa wakitaka kupewa heshima kwa madudu waliyoyafanya.

Leo TFF iko chini ya Karia, ilikuwa ina rundo la ajenda ambazo zinaonyesha wazi zilitokana na uongozi duni wa kipindi kilichopita.

Kipindi ambacho mambo mengi yaliharibika zaidi baada ya kipindi cha Leodegar Tenga ambaye kama rais alijitahidi lakini naye akaangushwa na watendaji wake hasa wale wa kuajiriwa ambao wengi walikuwa tatizo pia.

Tokea ameingia Karia na timu yake kumekuwa na matumaini makubwa. Naweza kusema kuna mambo kadhaa ambayo yamefanyiwa kazi na hasa lile la nidhamu.

TFF inawezekana isiwe tena sehemu ambayo kunaweza kufanyika uchotaji wa waziwazi na ikashindikana kujulikana.

Mfumo umetengenezwa ingawa hauwezi kuwa ndiyo ulinzi wa milele kwa kuwa ili mfumo ufanye kazi vizuri basi unahitaji usimamizi wa uhakika kutoka kwa wale wanaouongoza.

Inawezekana usimamizi pia ukawa bora, lakini nao unahitaji kudumu na kudumishwa ili kufanya mambo yazidi kwenda kwa uhakika ili kuendelea kufanya mambo yasimame.

Lakini katika suala la kuendeleza mpira, sioni kama kuna mipango ya haraka au ya muda mfupi ambayo ingeanza kufanyiwa kazi na kuyaona maendeleo ya mpira yakiwa yanaendelea katika viwanja na si makaratasi pekee.

Sidhani kama kuna kozi za kutosha za makocha, makocha wa makipa na hata ikiwezekana makocha wa watoto kwa ajili ya kuhakikisha wananolewa ili kuja kuwa msaada hapo baadaye.

Hakuna programu bora za watoto ambazo zitaisaidia Tanzania kuwa na vijana bora hapo baadaye na hili linapaswa kuingia katika mipango ya muda mrefu.

Ukiangalia kwa sasa, mambo mengi yanaweza kuwa yanafanyika lakini hayana tofauti kubwa na ya kipindi kilichopita.

Tunataka kuona TFF ya sasa ikibuni vitu, ikiweka wazi mipango yake na utekelezaji na kuchukua au kukopi vile vilivyopo na kusema kuwa kuna mambo yanafanyika.

Inaonekana kila kitu ni kilekile, ila kimeboreshwa, sawa. Sasa ubunifu wa uongozi huu kusaidia na kuboresha mpira wa Tanzania kuanzia mipango ya muda mfupi na mrefu uko wapi?

Kuna kila sababu ya TFF kuamka sasa, lazima wajue wameaminiwa, muda unakwenda na tungependa kuona kuna mabadiliko na vitu vinavyoonyesha tofauti.

Nimelizungumzia suala la nidhamu, nimewapongeza. Ingawa siamini nidhamu pekee inaweza kuwa kila kitu katika maendeleo ya mpira. Programu za vijana zipewe nguvu ili kutengeneza nguvu ya baadaye.

Wakati wa utawala uliopita, viongozi wengi wa sasa wa TFF walikuwa madarakani. Kama ni kasoro na walipojikwaa wanapajua, hivyo wapafanyie kazi.

SOURCE: CHAMPIONI

3 COMMENTS:

  1. Hana lolote kabisa kwa uongozi huu watanzania tusitarajie mabadiliko yeyote ya maana katika maendeleo ya soka nchini.

    ReplyDelete
  2. Matunda ya kufanya mambo kwa minajili ya kukomoana na kulipizana visasi huishia kwenye majuto

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic