July 2, 2018





NA SALEH ALLY
MICHUANO ya Kombe la Kagame imeanza na timu nyingi za hapa nyumbani zinazoshiriki zimeamua kutumia vikosi tofauti na vile vinavyotumika katika Ligi Kuu Bara.

Utumiaji wa vikosi tofauti unaonekana kuwa na faida yake. Faida mbili zinaweza kupatikana wakati wa michuano hiyo ya Kagame ambayo tayari imeanza jijini Dar es Salaam.

Kwanza ni kwa klabu, zitapata nafasi ya kuwajaribu wachezaji wengine kwa kuwa zimeamua kuwajaribu wachezaji wapya kwa ajili ya kuona kama itaongeza ukubwa wa vikosi.

Sababu zinaweza kuwa nyingi sana, mfano kuna wachezaji majeruhi au wengine wamepumzishwa. Faida itaongezeka kwani hadi mwisho wa michuano hiyo hata kama timu itacheza mechi tatu, basi itakuwa imeona kuna vipaji vipya vimejificha.

Vipaji hivyo vilikuwa vimejificha kwa kuwa hakukuwa na nafasi ya kutosha kwa wachezaji kucheza katika mechi za Ligi Kuu Bara au michuano mingine.

Nafasi ilikuwa inakosekana si kwa kuwa klabu inapenda. Badala yake kutokana na matakwa ya mwalimu ambayo yanazalishwa na utendaji wa wachezaji wenyewe. Kawaida mwalimu asingependa kubadili kikosi kinachoshinda kwa zaidi ya asilimia 20.

Hii inawafanya wachezaji wengi kukosa nafasi, lakini kupitia michuano ya Kagame, watapata nafasi ya kuonekana na raha zaidi watakuwa wakicheza mechi nyingi dhidi ya timu kutoka katika nchi jirani.

Kama mchezaji atafanya vizuri katika mechi dhidi ya timu inayotokea nje ya Tanzania. Hali ya kujiamini inapanda kwa zaidi ya asilimia 35 na kama atacheza mechi tatu na kufanya vizuri, bila shaka ana nafasi ya kufanya vizuri sana atakapopewa nafasi katika mechi za ligi.

Upande wa wachezaji hii ni bahati kwao, bahati njema ambayo huenda wangeweza kulalama kwamba hawakuwa wakipewa nafasi. Sasa nafasi na kama ni dodo basi liko mikononi mwao.

Kazi yao ni kulila tu, mchezaji anayepewa nafasi katika michuano kama ya Kagame, akashindwa kufanya vizuri, basi anakuwa hana wa kumlaumu. Kama atalaumu basi atakuwa ni mtu asiyejitambua na mpenda majungu.

Tumeona mchezaji kama Mohamed Ibrahim, hakupata nafasi ya kutosha kutoka kwa Kocha Pierre Lechantre ambaye alianza kulaumu kwamba hakuwa makini, hakuwa akihudhuria mazoezi kama inavyotakiwa na alipotokea mazoezini hakuwa ‘siriaz’.

Lakini kwa kuwa wachezaji wengi walipumzishwa katika michuano ya SportPesa Super Cup nchini Kenya akapata nafasi.

Huko nako alishindwa kuonyesha cheche ambazo zingeweza kuwafanya makocha kuona kweli alistahili nafasi ambayo alikuwa hapewi. Kutofanya kwake vizuri katika SportPesa Super Cup kumewafanya makocha waamini kwamba walikuwa sahihi kumuweka nje na huenda wanaweza wakaendelea vizuri bila yeye.

Maana yake, Mo Ibrahim kwa Simba, si tegemeo tena na hili amelichagua yeye. Huenda hataipata nafasi hiyo kwa mara nyingine na inawezekana ndiyo ikawa basi tena mambo yasiwe mazuri kwake.

Ndiyo maana nikasema michuano hii ya Kagame ina faida kwa klabu ambayo itagundua vipaji vilivyojificha vilivyokuwa havina nafasi. Kwa wachezaji wao wana nafasi ya kusimama na kuonyesha walichonacho.

Wachezaji washindane na wachezaji wasio katika kikosi kwa sasa. Kama unacheza namba ya Emmanuel Okwi, John Bocco au wengine ambao hawatakuwepo, huu ndiyo mwafaka kumuonyesha kocha na benchi la ufundi kwamba nafasi ipo kwako kufanya vizuri hata kama wasipokuwepo wale waliokuwa wakiaminika ni tegemeo.

Hii itamsaidia mchezaji kuingia katika akili ya kocha na wakati mwingine ataweza kumpa nafasi hata katika mechi ambayo watu wanaamini anastahili kucheza ni Bocco au Okwi tu.

Ushindani huu unapaswa uwe ule wa nia njema lakini nao hauwezi kufanikiwa kama wachezaji hawatajituma bila ya kuchoka wakiwa na nia ya kufanya vizuri.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic