KAMPUNI ya MultiChoice Tanzania kupitia king’amuzi chake cha DSTV, imeamua kuwawezesha kiuchumi mawakala wake wa viunga tisa vya Dar es Salaam, kwa kuwapatia Pikipiki 27 za magurudumu matatu (maarufu kama Bajaj), pamoja na ofisi za kufanyia kazi ikiwa pamoja na vitendea kazi vyake kama kompyuta.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo Mkuu wa mauzo wa kampuni hiyo Salum Salum, yaliyofanyika katika Ofisi zao Kinondoni jijini Dar es Salaam jana, alisema hii ni awamu ya kwanza ya mradi huo ambapo wametoa Bajaj 27 kwa viunga tisa Dar, na baada ya awamu hii watafanya tathmini yao na kisha kuupanua zaidi.
“Tumekuwa tukifanya kazi na vijana wengi wa Kitanzania wakiwa kama mawakala wa mauzo wa kujitegemea, jambo ambalo kwa sasa tumeamua kuwawezesha na kufanya nao kama wabia wetu wa kibiashara hivyo tutaendesha nao mauzo rasmi ya uwakala wa DSTV.
“Bajaj hizi ni maalum kabisa kwa kuhakikisha wanatoa huduma kwa haraka na wakati kwenye maeneo yao ili kuendeleaza hali ya ubora wa DSTV katika kutoa huduma za haraka kwa wateja wake wote, kwani tutahakikisha na wao wanakuwa na mtandao wa vijana wengine wengi wa mauzo na mafundi wa kufunga DSTV ambao wamepata mafunzo maalum na kuthibitishwa.
“Tumelazimika kufanya hivi kwani hapo mwanzo tulikuwa tunafanya mauzo kwa tabu sana kutokana na kutokuwa na mawakala wetu ambao wengi hawakuwa na ofisi maalumu jambo lililokuwa likiwafanya wateja wapate kwa tabu, lakini pia mawakala hawakuwa na vyombo vya kubebea vifaa pindi wanapokwenda kuwafungia wateja wetu jambo ambalo sasa limetatuliwa”, alisema Salum.
0 COMMENTS:
Post a Comment