MultiChoice yawawezesha vijana
· Yawafungulia ofisi za uwakala wa DStv
· Yawadhamini vitendea kazi – Bajaji
· Mradi huo kusambaa nchi nzima
Dar es Salaam Alhamisi Agosti 16, 2018: Kampuni ya MultiChoice Tanzania imeimarisha mkakati wake wa kuwawezesha vijana wa Kitanzania kibiashara na kiuchumi kwa kuwafungulia ofisi za uwakala wa DStv na kuwadhamini vitendea kazi mbalimbali ikiwemo kompyuta na pikipiki za magurudumu matatu (Bajaj).
Katika kutimiza hilo kampuni hiyo imekabidhi ofisi na bajaji tisa kwa vijana wa mkoa wa Dar es Salaam na inatarajia kupanua mradi huo kwenda mikoa mingine ikiwemo Mwanza, Arusha, Mbeya na Dodoma.
Akizungumza katika makabidhiano ya Bajaji hizo yaliyofanyika leo Alhamisi Agosti 16 katika makao makuu ya MultiChoice Tanzania jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Mauzo wa kampuni hiyo Salum Salum, amesema hii ni awamu ya kwanza ya mradi huo ambapo wametoa jumla ya Bajaji 27 kwa viunga 9 vya Dar es salaam na kwamba baada ya awamu hii watafanya tathmini na kisha kuupanua hapa Dar es Salaam ni mikoa mingine.
Amesema katika mradi huo, MultiChoice inawafadhili vijana hao ofisi za uwakala wa DStv na pia inawadhamini vitendea kazi muhimu kama vile Kompyuta na Bajaji ili
“Tumekuwa tukifanya kazi na vijana wengi ambao ni mawakala wa mauzo wa kujitegemea (direct sales) lakini sasa tumeamua tuwafanye wabia wetu wa kibiashara na kuwawezesha kuendesha biashara rasmi ya uwakala wa DStv” alisema Salum na kuongeza kuwa vijana hao watakuwa wakitoa huduma katika maeneo maalum yajulikanayo kama ‘viunga’. Kila wakala atakuwa na kiunga chake, na atakuwa na jukumu la kuhakikisha wateja wa eneo lake wanahudumiwa kwa haraka
“Vijana hawa watakuwa na mtandao wa vijana wengine wa mauzo na mafundi wa kufunga DStv ambao wamepata mafunzo maalum na kuthibitishwa. Kwa hiyo, kama mteja yuko Mbagala, atahudumiwa na wakala wa kiunga cha Mbagala, hivyo hivyo aliyeko Tabata atahudumiwa na kiunga cha Tabata na hii itakuwa kwa viunga vyote ambavyo ni Mbagala, Tabata, Kigamboni, Ilala, Chang’ombe, Mbezi beach, Mbezi Kimara, Manzese na Ukonga.
Amesema kwa kuwarasimisha vijana hawa, sasa watakuwa wanafanya biashara rasmi, wakiwa na leseni na ofisi na hivyo kuweza pia kulipa kodi stahiki kwa serikali na hivyo kuongeza mchango wao kwa uchumi wa nchi.
Wakizungumza bara baada ya kukabidhiwa bajaji hizo sambamba na laptop, wakuu wa viunga hivyo wamesema wamekuwa wakifanya kazi kama mawakala wadogo wa kujitegemea kwa muda sasa lakini walikuwa wakifanya kazi katika mazingira magumu kutokana na kutokuwa na ofisi rasmi na pia vitendea kazi hususan usafiri.
“Tulikuwa tunafanya mauzo kwa tabu sana kwani kwanza kutokuwa na ofisi ilikuwa ni vigumu kwa wateja kutupata. Pia hata ukipata mteja unalazimika kubeka vifaa kwenye usafiri usio wa uhakika kwenda kwa mteja na hii ilikuwa inapoteza muda na kuongeza gharama” alisema Rose Haule mkuu wa kiunga cha Temeke.
Naye Yusuph Migeto wa kiunga cha Mbagala amesema kuwa kuwepo kwa ofisi na usafiri wa uhakika kutawahakikishia wateja wao huduma ya haraka na yenye ufanisi. “wakati mwingine wateja walikuwa wanalalamika kwa kucheleweshewa huduma kwani ukipata mteja inabidi ufuate vifaa DStv kisha uende kumfungia mteja. Hii ilikuwa inachelewesha sana. Lakini kwa sasa tutakuwa na uwezo wa kuwa na vifaa karibu na pia kuwepo kwa usafiri wa uhakika kutatufanya kufanya kazi kwa haraka zaidi”
0 COMMENTS:
Post a Comment