August 4, 2018


Na Maulid Kitenge

Wakati Yanga hivi sasa ikipitia kipindi kigumu kiuchumi, lakini tanga­zo la Kaimu Katibu Mkuu, Omar Kaaya kuwa sasa Wanayanga waichangie timu yao kujiandaa na msimu ni aibu.

Ni aibu kwa vile Yanga haikupaswa kufika hatua hiyo, kwa utitiri wa wanachama wa klabu hiyo tu wakilipa ada zao Yanga ilitosha kujiendesha lakini kutokana na mfumo wa wanachama kutolipia ada zao mpaka wakati wa uchaguzi ndiyo maana wamefika hapo.

Kingine Yanga haijaeleweka pesa za Kampuni ya SportPesa ambayo inaidhamini timu hiyo zimeenda wapi? Pesa za udhamini wa Azam na pesa za kuingia hatua ya makundi Kombe la Shirikisho Afrika ziko wapi?

Haya ni maswali ambayo bado majibu yake hayaeleweki lakini badala yake naona tayari wametangaza kapu wana Yanga wachangie. Unajiuliza Yanga ilipaswa kufika hapa? Bila shaka jibu litakuwa hapana.

Badala ya kuhangaikia kutaka kutembeza kapu hilo ili wachangiwe na wanachama na mashabiki wao, nafikiri ni wakati wa Yanga kuharakisha kuelekea kwenye mabadiliko ili timu ipate mbia wa kuiendesha.

Wakati Yanga wanalia njaa, angalia wenzao wa Simba ambao tayari wameonja utamu wa klabu yao kuingia kwenye mabadiliko na sasa hawana tena matatizo ya kifedha baada ya bilionea Mohamed Dewji ‘Mo’ kuwekeza Sh bilioni 20 ndani ya klabu hiyo.

Yanga inapaswa kwenda huko badala ya kuhangaika kutembeza kapu mpango ambao sidhani kama utafanikiwa maana wachangiaji watachoka tu.

Yanga ingeweza kuwa ya kwanza katika mfumo wa kisasa kwani ilikuwa ya kwanza kuanza mchakato wa kampuni na katiba yao kuruhusu kuwa na kampuni ndani ya Yanga ambayo ndio itaendesha timu.

Lakini migogoro baina ya wale wanaopinga na uongozi imewafikisha hapo. Aliyekuwa mwenyekiti wao, Yusuf Manji pia alishataka kuiendesha Yanga kwa kukodi lakini wapingaji walipinga na kukwamisha mchakato huo na Manji kujitoa.

Ukiangalia hayo yote unaona kama Yanga imejitakia yenyewe kupitia hivi sasa katika hali hiyo. Leo tena unasikia mambo ya kutembeza kapu au bakuli! Huko ni kurudi nyuma kabisa sio mpira wa leo.

Je, hapo ndio unaweza kushindana na Simba iliyo kwenye uwekezaji wa bilioni 20? Yanga inapaswa ijitafakari na kufanya haraka kubadili mfumo wa klabu yao kutoka huko iliko sasa na iwe ya mtindo wa hisa.

Mkiendelea kusubiriana hakika mnaweza kuipoteza timu yenu, wanachama ninyi ndiyo wenye maamuzi ya kuamua sasa Yanga iwe katika mfumo gani, mkitaka kubaki hivyo sawa maana naona huko tuendako mtazidi kuumia sana.

Aibu hii kwa timu inayoshiriki michuano ya kimataifa kwa kweli ni mbaya, mkumbuke wenzenu Simba waliamua kubadilika baada ya kupita kipindi kirefu cha mateso na kujikuta wakipotea kabisa kwenye ramani ya mafanikio sasa na nyie Yanga kama mtalala hiki hakiwezi kuwapita.

2 COMMENTS:

  1. Kwanini wabadhirifu simba wapo makorokoroni na watimu nyengine wanaopeta mitaani na mabakuli au ndio timu mpaka ife?

    ReplyDelete
  2. Hapana Kitenge huu utaratibu siyo ndiyo unaotegemewa kuendesha Timu, ni sehemu ya vyanzo vyanzo vya mapato ya Club. Huwezi kutegemea vyanzo kimoja to.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic