KOCHA SIMBA AJA NA MFUMO MPYA UTURUKI
Mambo ni moto katika kikosi cha Simba huko nchini Uturuki ambako kikosi hicho kinachoendelea kujifua kwa ajili ya msimu ujao, ambapo moja ya mabadiliko yaliyopitishwa na kocha mkuu wa timu hiyo, Mbelgiji, Patrick Aussems ni katika mfumo wa mawasiliano.
Unaambiwa kuwa mawasiliano yoyote ya kiofisi kuhusiana na timu kutoka kwa viongozi kwenda kwake ni lazima yawe kwa maandishi na yatumwe kwake kwa njia ya barua pepe (email) lakini pia nakala zitumwe kwa viongozi wengine wa juu yake.
Habari za kuaminika kutoka ndani ya Simba ambazo Championi Ijumaa limezipata zimedai kuwa utaratibu huo wa Aussems unaonekana kuwa mpya kwa baadhi ya viongozi kutokana na kuonekana kuwatesa.
“Huo ndiyo utaratibu mpya wa mawasiliano ya ndani ya timu yetu ambao kocha amependekeza utumike, kwa hiyo na sisi hivi sasa tunajitahidi kuufanya, hivyo japokuwa unatusumbua kidogo kwa sababu tulikuwa hatujauzoea.
“Kwa mfano tunapotoka mazoezini, daktari anatakiwa kuandika ripoti yake inayoonyesha afya za wachezaji na maendeleo ya wachezaji ambao ni majeruhi kisha amtumie kwa njia ya email huku nakala akituma kwa viongozi wengine ambao wanastahili kupata ripoti hiyo.
“Kwa hiyo na viongozi wengine wote wanatakiwa kufanya hivyo kwa ajili ya kulinda maslahi ya timu na kuondoa hali ya kuingiliana katika kufanya maamuzi,” kilisema chanzo hicho cha habari na kukiri kuwa mfumo huo umekuwa ukiwapa wakati mgumu watendaji kwa kuwa hayakuwa mazoea yao.
Alipoulizwa kuhusiana na hilo Meneja wa Simba, Richard Robart ambaye yupo na kikosi hicho nchini Uturuki hakuwa tayari kusema chochote zaidi ya kudai kuwa hayo ni mambo ya ndani ya timu kwa hiyo hawezi kuyazungumzia.
Simba inaendana na kauli ya hapa kazi tu. Yaani yanayoendelea kutokea pale Simba ni ya kushangaza. Na kama wataendelea hivi hivi wanavyokwenda sasa basi SIMBA lazima iwe klabu ya mfano kwenye ukanda wetu.
ReplyDelete