Na George Mganga
Wakati Simba wakitarajiwa kuwasili jijini Mwanza leo kwa usafiri wa anga, uongozi wa Mtibwa Sugar umesema hautishwi na kambi ya Uturuk ambayo iliwekwa na wapinzani wao kwa muda wa wiki mbili.
Mtibwa watakutana na Simba kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii jijini Mwanza kesho majira ya saa 10 kamili jioni ukiwa ni mwanzo wa kuikaribisha Ligi Kuu Bara 2018/19.
Msemaji Mkuu wa Mtibwa, Thobias Kifaru, amefunguka na kusema kambi ya Simba ambayo waliweka Uturuki haina jipya na akitamba kuwa lazima wawaoneshe kuwa wao ni chuo cha soka.
Kifaru ameeleza kuwa kikosi chao kilikuwa katika maandalizi mazito hapa hapa nchini na akiwaambia Simba watarajie upinzani mzito kuelekea mechi hiyo kubwa inayosubiriwa kwa hamu na wadau wa michezo nchini.
"Unajua wenzetu waliamua kwenda Uturuki kuweka kambi ya wiki mbili, lakini wakae wakijua sisi haitupi presha na tuliamua kujichimbia hapa hapa nchini ili tuandae dawa yao, tutawaonesha upinzani mkali" alisema.
0 COMMENTS:
Post a Comment