Kwa taarifa yako shabiki wa Simba popote ulipo, wachezaji wakikanyaga tu Dar es Salaam kesho Jumatatu alfajiri hawataonekana uswahilini. Matajiri wa Simba wameamua watakwenda moja kwa moja kwenye Hoteli ya Serena ambayo wanakaa wageni wa kishuwa tu.
Msemaji wa Simba, Haji Manara alithibitisha kwamba; “Ratiba imebadilika badala ya kutua Jumapili alfajiri itafika Jumatatu alfajiri hapa nchini na kuendelea na maandalizi pamoja na shughuli zile za kijamii ambazo tunafanya kuelekea siku maalum ya Simba day.”
Wachezaji hao ambao walikuwa kambini nchini Uturuki wataonekana mitaani kwa mara ya kwanza baada ya mechi ya Simba Day dhidi ya Asante Kotoko ya Ghana itakayochezwa Jumatano kwenye Uwanja wa Taifa.
Spoti Xtra limedokezwa kwamba viongozi wa Simba chini ya muwekezaji bilionea, Mohammed Dewji ‘MO’ wameamua vijana wafikie kwenye hoteli hiyo iliyoko katikati ya jiji ili kutuliza akili na kujiweka sawa kwa siku hiyo kubwa ya mashabiki wa Simba ambayo itakuwa ni sikukuu ya Nanenane Kitaifa.
Katika vyumba hivyo Simba watalazimika kutoa Sh. Milioni 18 kabla ya kuondoka na kuelekea Sea Scape ambapo wamekuwa wakiweka kambi mara kwa mara ambako nako pia ni ufukweni eneo la Mbezi.
Wachezaji wa Simba wamefurahia hali ya maisha inayoendelea ndani ya klabu hiyo na kusisitiza kwamba sasa ni muda wa kazi tu na mashabiki watafurahia sana msimu ujao.
CHANZO: SPOTI XTRA
0 COMMENTS:
Post a Comment