DIGRII YAWAKIMBIZA WENGI SIMBA
Kipengele cha Mwenyekiti mpya wa Klabu ya Simba awe na elimu ya shahada ‘digrii’, kimeonyesha kuwatisha wagombea wengi kiasi kwamba hadi juzi Jumapili mchana hakukuwa na mgombea yeyote aliyejitokeza kuchukua fomu ya nafasi hiyo.
Kamati ya Uchaguzi Simba ilitoa siku saba pekee ambapo wagombea walitakiwa kufika makao makuu ya klabu na kuchukua fomu za kugombea nafasi sita zinazogombaniwa ambapo zoezi lilianza Septemba 3 na limefika tamati jana Septemba 10.
Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi wa Simba, Boniface Lihamwike, amesema kuwa bado zoezi la uchukuaji fomu limekuwa la kusuasua licha ya wito kutolewa kwa wanachama kujitokeza kwa wingi katika kusaka nafasi za kuiongoza klabu hiyo, huku nafasi ya uenyekiti ikionekana kuwa ngumu zaidi kutokana na kigezo cha elimu.
“Wanachama bado wanasuasua kuchukua fomu mpaka sasa ni fomu za nafasi ya wajumbe pekee ndizo zimechukuliwa nazo pia zikiwa ni za watu wachache, huku nafasi ya uenyekiti ikionekana watu kuogopana hali inayopelekea mpaka sasa pasiwepo na mgombea hata mmoja,” alisema Lihamwike. Uchaguzi wa Simba umepangwa kufanywa Novemba 3.
Hata hivyo jana kunako makao makuu ya klabu, jumla ya wajumbe 19 walifikia idadi ya kuwa ndiyo waliochukua fomu pamoja na wanaowania nafasi ya Uenyekiti wakiwa wawili.








0 COMMENTS:
Post a Comment