HAWATUWEZI, KICHUYA AKABIDHIWA KWA BOXER
Hawatuwezi! Ndivyo ambavyo tambo za mashabiki wa Simba na Yanga zinasikika kwa sasa kila mmoja akijitapa kwamba mpinzani wake hawezi kumfunga katika mchezo wao wa ligi kuu utakaopigwa kesho Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa.
Mchezo huu namba 72, umepangwa kuanza saa 11 jioni kwa saa za Tanzania na Jonesia Rukyaa anatarajiwa kupuliza kipyenga ikiwa ni mechi yake ya nne ya watani wa jadi huku akisaidiwa na Ferdinand Chacha wa Tanga na Mohammed Mkono kutoka Mwanza huku Elly Sasii wa Dar akitarajiwa kuwa mwamuzi wa akiba.
Yanga wenyewe walienda kuweka kambi mjini Morogoro tangu Jumatatu na jana jioni walitarajiwa kurejea jijini Dar wakati Simba wao walibaki Dar na kuendelea na mazoezi yao kama kawaida.
Makocha wa timu zote, Patrick Aussems wa Simba na Mwinyi Zahera wa Yanga wanaonekana kutokuwa na hofu sana kama ambavyo mashabiki wa timu zote waliyonayo huku kila mmoja akisisitiza kuwa anataka pointi tatu kwa maana hiyo unaweza kusema kila mmoja anaona mwenzake hawezi kumfunga.
Hata hivyo, katika mazoezi ya timu zote, makocha hao walionekana kusimamia zaidi kwenye suala la ufungaji. Katika mazoezi yaliyofanyika jana kwa upande wa Simba, Viwanja vya Gymkhana, Posta, Dar Championi lilimshuhudia kocha Aussems raia wa Ubelgiji akitoa maelekezo namna ya kushambulia goli la wapinzani wakati timu yao ikiwa imepata mipira ya faulo na kona.
Mbelgiji alionekana akiwapa mbinu Pascal Wawa na Erasto Nyoni na kuwataka kwenda kushambulia kwa kupiga mipira ya vichwa pale inapotokea faulo na kona kwenye goli la wapinzani huku lengo lake likiwa ni kucheza mipira ya vichwa huku akiwataka kufunga.
Hiyo, ni baada ya kukosekana John Bocco ambaye ana sifa kubwa ya kufunga mipira ya vichwa inayotokana na krosi, kona na faulo ambazo wanazipata wakiwa uwanjani.
Kocha huyo, mara kadhaa alikuwa akionekana akiwapa maelekezo na wakati mwingine kurudia mipira ya kona na faulo kupigwa kwa lengo la kutoa maelekezo wakati mazoezi hayo yakiendelea wakicheza muundo wa mechi baada ya kuvipanga vikosi viwili.
Wakati mazoezi hayo yakiendelea, Wawa na Nyoni walionekana wakifuata maelekezo ya kocha huyo kwa kwenda kushambulia goli la wapinzani kila timu yao inapopata kona au faulo huku wakiwaacha golini kwao kulinda mabeki wa pembeni, Shomari Kapombe na Hussein Mohamed ‘Tshabalala’. Akizungumzia hilo, Aussems alisema: “Najaribu kuboresha baadhi ya sehemu nilizoziona zina upungufu ambazo niliziona kwenye michezo iliyopita kwa lengo la kupata ushindi.”
Kwa upande wa Yanga ambayo ilifanya mazoezi yake ya mwisho mkoani Morogoro jana Ijumaa kwenye Uwanja wa Chuo cha Biblia, Kocha Zahera alionekana akiwapa mazoezi ya kawaida wachezaji wake huku mara nyingi wakichezea mpira.
Lakini katika mazoezi waliyofanya tangu watue hapo ukiachana na ya jana, Zahera alionekana kuwatumia zaidi wachezaji Deus Kaseke, Mrisho Ngassa, Gadiel Michael na Ibrahim Ajibu katika kupiga krosi ambapo langoni kulikuwa na washambuliaji kadhaa wakiwemo Amissi Tambwe, Heritier Makambo na Yusuf Mhilu.
Washambuliaji walitakiwa kumalizia mipira hiyo langoni kwa kichwa na miguu huku wengi wakionekana kumuelewa kocha kwani walifanya vyema. Lakini pia, wachezaji wote walijifua kupiga mashuti makali hali inayoonekana kuwa huenda mchezo wa kesho ukawa na krosi na mashuti ya mbali kwa sana.
Hata hivyo kulingana na mazoezi ya timu zote, kikosi cha Simba kitakachoanza kesho Jumapili kinaweza kupangwa hivi; Aishi Manula, Shomary Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Pascal Wawa, Erasto Nyoni, James Kotei, Shiza Kichuya, Jonas Mkude, Meddie Kagere, Emmanuel Okwi, Claytous Chama.
Kwa upande wa Yanga, kikosi kinaweza kuwa hivi kesho; Beno Kakolanya, Paul Godfrey, Gadiel Michael, Andrew Vincent ‘Dante’, Kelvin Yondani, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Ibrahim Ajibu, Papy Tshishimbi, Heritier Makambo, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Deus Kaseke.
Kocha wa Yanga, Zahera amezungumza na Championi kuhusiana na mchezo huo ambapo alisema: “Mechi ni ya kawaida sana kwangu kwani Simba nimewaona na aina ya mchezo wao pia ni uleule ambao walicheza na Asante Kotoko wala haujabadilika, kwa hiyo kwangu mimi hawanitishi.
“Tatizo ambalo naliona ni kwa wachezaji wa timu zote kuuchukulia mchezo huo kuwa ni mkubwa sana jambo ambalo siyo zuri.
“Hata hivyo nimewaambia wachezaji wangu kuuchukulia kama mchezo wa kawaida kama ilivyokuwa Mtibwa Sugar, Coastal Union, Stand pamoja na Singida United.” Kocha wa Simba, Aussems alisema: “Tumejiandaa vyema kwa ajili ya mchezo wetu dhidi ya Yanga siku zote ukikutana na mpinzani wako lengo lako ni kuona unashinda na ndivyo ilivyo kwa upande wetu, tunachokihitaji ni kupata pointi tatu. “Mchezo hautakuwa mrahisi hivyo tunatumia siku zilizobakia kuhakikisha tunafanikiwa kufanya vyema ili kushinda.”
SIMBA wapo wenye uwezo wengi hata Yanga lakini kichuya kama atakuwa mzima wa afya timamu basi Yanga wajue wanashida. Na hata wale walombeza kuachwa kuitwa timu ya Taifa basi kesho wanaweza kujisikia vibaya. Uzuri wa kichuya licha ya udogo wake wa kimo lakini ni mpambanaji kwa hivyo katika hii mechi kichuya anaweza kuwa mwiba kwa safu ya ulinzi wa Yanga.
ReplyDelete