Na Mwandishi wetu
Klabu ya kuogelea ya Taliss-Ist ya Upanga imefanikiwa kutwaa ubingwa wa mashindano ya wazi ya kuogelea ya taifa yaliyomalizika wikiendi kwenye bwawa la kuogelea la Shule ya Kimataifa ya Tanganyika (IST), Upanga.
Klabu hiyo imetwaa ubingwa huo kwa kupata pointi 2,700 na kuzishinda klabu nyingine saba zilizoshoriki katika mashindano hayo.
Taliss-Ist ilitawala mashindano hayo tokea mwanzo kupitia waogeleaji wake wakiongozwa na nyota mpya ya Tanzania kwa sasa, Natalia Ladha walishinda nafasi ya kwanza kwa upande wa wanawake kwa kukusanya pointi 1,444 na kwa wanaume pia walishika nafasi ya kwanza kwa kupata pointi 1,156.
Pia mwogeaji Nawal Shebe wa Taliss- Ist alifanya vizuri kwa upande wa staili ya Breaststroke kwa kumaliza wa pili katika mita 50 na 100.
Meneja wa Taliss-Ist, Hadija Shebe alisema kuwa moyo wa kujituma, mafunzo mazuri na ushirikiano baina ya shule, klabu na wazazi ndiyo nguzo pekee ya kupata mafanikio hayo yaliyowashirikisha waogeleaji 123 na kupambana katika matukio 121.
“Waogeleaji wetu wamefanya vizuri sana na wanahitaji pongezi, tunajivunia kwa mafanikio haya,ni makubwa kwa upande wa klabu hasa baada ya kuunganika na shule,” alisema Hadija.
Klabu ya Bluefins ya jijini pia ilishika nafasi ya pili kwa kupata pointi 1,339. Klabu hyo ilipata pointi 862 kwa upande wa wavulana na pointi 477 kwa upande wa wasichana.
Muasisi na kocha wa klabu hiyo, Rahim Alidina aliwapongeza waogelaji wote, makocha na wazazi kwa ushirikiano na kuifanya klabu yao kuwa ya pili kitaifa kwa sasa kwa upande wa mashindano ya wazi.
Mabingwa wa Tanzania kwa upande wa klabu, Dar es Salaam Swimming Club (DSC) ilimaliza ya tatu kwa kupata pointi 1,245 ambapo kwa wanawake walipata pointi 799 na kwa wanaume pointi 446.
Nafasi ya nne ilichukuliwa na Mwanza iliyopata pointi 766 wakati nafasi ya tano ilikwenda kwa Mis Piranhas kwa kupata pointi 542 na ya sita ilichukuliwa na klabu mpya kabisa, FK Blue Marlins kwa kupata pointi 202.
Klabu ya Moshi (ISM) ilimaliza katika nafasi ya saba kwa kupata pointi 153 na Champion Rise ilimaliza katika nafasi ya nane kwa kupata pointi 143.
Mwenyekiti wa Chama Cha Kuogelea Tanzania (TSA), Imani Dominick alisema kuwa mashindano hayo yamefanikiwa sana pamoja na kuyandaa wiki tatu tu baada ya wao kuingia madarakani.
“Nwashukuru wadau na wadhamini kwa kufikisha mashindano hayo ikiwa ni muda mfupi tokea kuingia madarakani, hivyo, Pepsi, Azam, Subway, IST, Food Lover’s Market na wengineo wanastahili pongezi kubwa,” alisema Dominick.
0 COMMENTS:
Post a Comment