UTARATBU WA MAPINGAMIZI SIMBA HUU HAPA, YATASIKILIZWA LEO SERENA HOTEL
Utaratibu wa kusikiliza mapingamizi ya wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi wa Simba unatarajiwa kufanyika leo Jumatatu kuanzia saa 10:30 jioni Serena Hotel jijini Dar huku mpaka kufikia jana jioni kulikuwa na mtu mmoja pekee aliyepeleka pingamizi kwa baadhi ya wagombea wa nafasi za ujumbe.
Klabu ya Simba hivi karibuni ilitangaza rasmi kuanza mchakato wa uchaguzi kwa nafasi mbalimbali za uongozi katika klabu hiyo. Uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika Novemba 3, mwaka huu.
Mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi huo, Boniface Lihamwike, amesema kuwa mchakato wa kupeleka mapingamizi kwa wagombea umefikia kikomo na kwamba kilichobaki ni kusikiliza mapingamizi ambapo shughuli hiyo itafanyika leo.
Ni mtu mmoja tu mpaka sasa ambaye amepeleka mapingamizi yake kwa wagombea wanne, mmoja akiwa ni mwanamke akidai wamekosa sifa ya kuiongoza Simba kutokana na kuvunja katiba, lakini Lihamwike ameshindwa kuwataja majina yao, hata hivyo alisema waliowekewa mapingamizi ni wale watu waliokuwa wajumbe wa kamati ya utendaji iliyopita.
“Kesho (leo) ratiba ya kusikiliza mapingamizi ipo kama kawaida na itafanyika Serena Hotel kuanzia saa 10:30, na mpaka kufikia jana (juzi) kulikuwa na mtu mmoja ambaye ameweka mapingamizi kwa wagombea wanne,” alisema Lihamwike.
Mwenyekiti huyo pia alipuuza taarifa kwamba uchaguzi wao umepigwa stop na Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), akisisitiza kwamba siyo za kweli kwa kuwa hawajapokea taarifa rasmi juu ya uamuzi huo.
“Hamna kitu cha namna hiyo, taarifa hizo zilitafsiriwa tofauti lakini siyo kupigwa stop. Mpaka leo sisi kama kamati hatujawahi kupokea taarifa hizo,” alisema.
Alipotafutwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Revocatus Kuuli, kuzungumzia suala hilo, alisema ni kweli waliusimamisha uchaguzi wa Simba, lakini baada ya kurekebisha dosari waliruhusu uendelee.
“Bahati mbaya ile barua tuliyoandika sekretarieti ya TFF haikuipeleka kwa Simba, ikabidi tuwape (Simba) nakala ambayo waliitumia kurekebisha dosari na tukaamua uchaguzi uendelee,” alisema Kuuli.
0 COMMENTS:
Post a Comment