October 3, 2018



NA SALEH ALLY, KHARTOUM
NENO Al Hilal maana yake ni mwezi, hili ni jina la timu nyingi sana duniani hasa zile zinazotokea katika nchi mbalimbali za Kiarabu au zenye asili hiyo.


Licha ya rundo la timu zinazotumia jina hilo, Al Hilal Omdurman ya Sudan ndiyo timu ya kwanza kuanza kuitwa jina hilo mwaka 1930, sasa ni miaka 88 iliyopita.

Klabu hiyo ni maarufu zaidi nchini hapa na inashindana na wapinzani wao wakubwa El Merreikh ambao pia ni maarufu na moja ya timu tajiri barani Afrika.

Omdurman ni eneo linalojitegemea likiwa ni upande wa pili wa Khartoum baada ya kuvuka Mto Nile. Ndiyo maana klabu hiyo ikapewa jina la Al Hilal kutoka Omdurman ambako pia wanatokea wapinzani wake, El Merreikh na viwanja vya klabu hiyo mbili, viko jirani kabisa.

Al Hilal inamiliki uwanja unaojulikana kwa jina la Al Hilal Stadium, uwanja huu unakadiriwa kufikisha hadi watu 65,000 wanaoingia lakini kitaalamu kwa uwanja ambao una viti na watu kuingia kwa nafasi, angalau watu 40,000.

Klabu ya Al Hilal inatajwa kuwa moja ya klabu tajiri barani Afrika na Mtanzania, Thomas Ulimwengu anaitumikia kupitia timu yake.

Timu inayomilikiwa na klabu hiyo ndiyo inayoongoza kwa mashabiki hapa Sudan na ukubwa wake unaifanya iwe gumzo zaidi kuliko nyingine zote.

Mashabiki wa Al Hilal ni wale wenye wazimu hasa wa soka ambao wanapokasirika huwa ni hatari sana kwa kuwa wana uamuzi mgumu na wanaweza kudhuru wakati wowote.

Wakati wa mechi za Al Hilal kumekuwa na ulinzi mkali hasa inapocheza na timu ambazo zinaaminika zina upinzani mkali dhidi yake.

Kikundi chake cha ushangiliaji cha Al Hilal Utras, ndicho kinaaminika kuwa na mashabiki watukutu zaidi barani Afrika kikifananishwa na kile cha Al Ahly ya Misri au Club African ya Tunisia kwa kuwa wao kuumiza si jambo gumu kwao na wamekuwa wakipambana na askari inapoonekana wamekerwa.

Mwenyekiti wake ni bilionea Ashraf Seed Ahmed, mmoja wa watu maarufu nchini hapa na hivi karibuni alikubali Thomas aongezwe katika kikosi chake bila ya kujali hakuwa amepona sawasawa.

Ulimwengu alisajiliwa na Ah Hilal huku mwenyekiti huyo akiunga mkono kwa kuwa tayari alishamuona Ulimwengu akiitumikia TP Mazembe ya DR Congo na kufanya vizuri.

Wakati Ulimwengu ametua kwa takribani miezi miwili, Al Hilal ilimuajiri kocha wake wa zamani Lamine N’Diaye raia wa Senegal ambaye alifanya naye kazi wote wakiwa TP Mazembe na kufanya vizuri.

Kwa hadithi, unaweza kuamini Ulimwengu amepotea kwenda Sudan lakini kama utazungumza suala la mafanikio kwa kuangalia yuko, Ulimwengu ambaye alikaa nje na kushindwa kucheza kwa takribani miezi sita kutokana na kuandamwa na majeraha, unaweza kusema ni mchezaji mwenye bahati.

Wachezaji wengi ambao wako fiti na wanategemewa na klabu zao, wangetamani kupata nafasi ya kucheza Al Hilal lakini inashindikana licha ya juhudi za dhati kwa na hata mawakala wao.

Ulimwengu alikubalika tangu akiwa bado mgonjwa, jambo ambalo lilikuwa ni kuonyesha imani ya kiwango cha juu sana.

Klabu hiyo imezaliwa mwaka 1930, miaka mitano baadaye ikazaliwa Yanga na ulipoongezeka mmoja na kuwa sita, ikazaliwa Simba.

Pamoja na kupishana miaka mitano na sita, utakapoamua kuzifananisha, utakuwa unazungumzia mfano tofauti sawa na mbingu na ardhi.

Uwanja mkubwa kama wa Al Hilal, si jambo dogo tena ni uwanja ambao ndani yake kuna hoteli kubwa ya kisasa ambayo wachezaji huweka kambi.

Hoteli hiyo iko ndani ya uzio wa Al Hilal Stadium na ina vyumba takribani 50 vya kisasa kabisa na ina sehemu tatu za kupumzikia zikiwa na makochi ya kisasa na mapokezi pia.

Upande huo wa mapokezi unaambatana na sehemu ya chini ya kupumzikia lakini kuna sehemu nyingine juu na zote zinatumika kwa ajili ya wageni wachache maalum wa klabu hiyo lakini hasa ni mahsusi kwa ajili ya wachezaji wanapoweka kambi.

Wachezaji wa Al Hilal wanapokuwa kambini angalau kwa siku mbili, wanaweka kambi katika hoteli hiyo ya kisasa ambayo mbele yake kuna sehemu maalum ya kupumzikia yenye majani.
Al Hilal ni kati ya klabu chache kabisa za Ukanda wa Afrika Mashariki zinazojitambua. Maana inamiliki redio yake, runinga yake na pia gazeti lake. Hivyo ina timu kubwa ya vyombo vya habari.


Vyombo hivyo vya habari vimekuwa vikifanya kazi ya kuitangaza na kuisaidia Al Hilal kuongeza mashabiki na kwa ushirikiano mkubwa na vyombo vingine vya habari.

Tofauti na nyumbani, timu hata ikianzisha gazeti tu, tayari inatengeneza uadui na vyombo vingine vya Tanzania kama vile kuvikomoa na kadhalika. Al Hilal imekuwa ikisisitiza suala la umoja na vyombo vya habari hauwezi kuvunjwa.

Meneja wa Al Hilal, Mohamed Haroun amezungumza na na blog yako pendwa ya SALEHJEMBE katika eneo la Omdurman na kusisitiza kwamba wanajitambua na kikubwa kwao ni ndoto ya ubingwa Afrika.

“Tunataka kuwa mabingwa, tumelikosa kombe mara zote lakini tunataka kuwa mabingwa wa Afrika ili kutimiza ndoto zetu,” anasema.

“Tunajua tuna mafanikio makubwa katika suala la biashara na uendeshaji, lakini kuitwa mabingwa wa Afrika ni jambo tunalolipa kipaumbele kweli,” anasisitiza.

Ukiachana na meneja huyo, Ulimwengu yeye anasema alipajua Sudan kabla hajatua Al Hilal.

“Nilikuja hapa mara mbili na TP Mazembe. Mara moja nilifunga dhidi yao na wakati mwingine dhidi ya Merreikh. Hivyo walikuwa wakinijua vizuri, hii ilinisaidia hata kuzoea hapa mapema,” anasema.


“Kwa maana ya klabu kweli mambo yanafuata weledi, utaratibu sahihi na kila kitu kimepangwa. Hii ni klabu kubwa sana tofauti na wengi wanavyofikiria. Huenda kwa kuwa iko Sudan, wengi kuichukulia poa.

“Kwa maisha hapa, kila mtu ana yake. Pia watu wanapenda sana mpira hivyo kuheshimika kama unafanya vizuri ni jambo la sekunde tu.”

Al Hilal inamiliki uwanja huo mkubwa, inamiliki mali nyingi hadi hoteli na hapa ndiyo unagundua ukubwa wake huku ikiwa moja ya timu inayoheshimika sana kisoka barani Afrika ingawa bado hawajatimiza  ndoto ya kuwa mabingwa wa Afrika.

Ulimwengu ameamua kutua Sudan na kufanya kazi na sasa kwa wale waliokuwa hawajui au waliona amekosea, wanaweza kuelewa kuhusiana na Al Hilal.

Kama hiyo haitoshi, Jumatano tutakuletea kugusiana na namna Ulimwengu ambavyo amekuwa gumzo katika soka la Sudan lakini anavyoishi kwa kukwepa usumbufu wa mashabiki barabarani au kila anapotembea.



2 COMMENTS:

  1. Aya ndio yanayotakiwa kufanywa na timu zetu

    ReplyDelete
    Replies
    1. Itawezekena tu watakapoondoka akina mzee Akilimali na wazee wenzake akina Hamisi Kilomoni na Bi.Chau

      Delete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic