DIAMOND AANDIKA HISTORIA TANDALE
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ameziagiza mamlaka husika za aradhi jijini hapo kufanya mchakato wa kumpatia ardhi msanii wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz kwa ajili ya kujenga uwanja wa michezo na chuo cha sanaa.
Makonda alitoa agizo hilo wakati alipokuwa mgeni rasmi katika tafrija ya msanii huyo aliyoifanya mitaa ya Tandale Sokoni katika kusherehekea siku yake ya kuzaliwa ambapo aliitumia kugawa misaada mbalimbali kwa wananchi wa Tandale.
Awali, Diamond alitoa pendekezo hilo alipokuwa akihutubia mbele ya umati wa watu ulihudhuria tafrija hiyo ya wazi na ndipo Makonda akaagiza mamlaka zikutanane na Diamond ili kufanya mchakato wa kumpatia ardhi kwa lengo hilo mitaa ya Tandale.
Staa huyo ambaye sherehe yake ya kuzaliwa rasmi ilikuwa Oktoba 2, 2018 aliamua kuitumia siku hiyo ya jana kutoa misaada Tandale kwa kuwa ni eneo ambalo alizaliwa na kukulia.
Diamond alitoa bima ya afya kwa watu 1,000 kupitia Kampuni ya Resolution, bodaboda 20 kwa vijana ambao hawana ajira pamoja, matenki manne kwa Shule ya Msingi ya Hekima na mitaji kwa wanawake.
Naye, Mkurugenzi wa Global Group, Eric Shingongo ambaye alikuwa mmoja wa wageni alitoa pikipiki tatu na kufanya idadi ya pikipiki zilizotolewa kuwa 23.
Akizungumza alipopewa nafasi, Shigongo ambaye ndiye mtu wa kwanza kumlipa fedha nyingi Diamond kwa ajili ya shoo, alisema inawezekana vijana wa Tandale kuwa kama Diamond ikiwa wataamua kujituma na kukwepa tabia ovu.
“Jiepushe na tabia mbaya, ulevi, kila mmoja anaweza kufanikiwa, Tanzania ni nchi nzuri, hapa kuna mawaziri na rais, mnao uwezo wa kununua nyumba za Masaki,” alisema Shigongo.
Baadhi ya wageni maarufu waliohudhuria ni Meya wa Kinondoni, Benjamin Sitta, Rayvanny, Lavalava, Chid Benz, Mboso, Asha Baraka, Katibu wa Basata, Jaqueline Mengi, Haji Manara, Queen Darleen na Mama Diamond.
0 COMMENTS:
Post a Comment