October 8, 2018



NA SALEH ALLY
SITAKI kuficha hata kidogo kwamba inaonekana wazi baadaye kunaweza kuwa na mgogoro mkubwa hasa mwishoni mwa Ligi Kuu Bara.

Nasema kutakuwa na mgogoro mkubwa kwa kuwa kama mwendo ndiyo huu tunaokwenda nao, hali ya kuwa na malalamiko mengi sana itazidi.

Kuzidi kwa malalamiko, kutafanya badala ya gumzo kubwa mpira na mambo ya kiujuzi au kifundi, mijadala itakuwa ni kazi mbovu ya waamuzi.

Hamtaki kukubali kwa kuwa ushabiki umekuwa ni miwani migumu inayowazuia kufumbua macho yenu lakini joto kali linalozuia mioyo yenu kuwa huru na kuangalia kilicho sahihi.

Waamuzi wamekuwa wakichezesha mechi nyingi za Ligi Kuu Bara katika kiwango cha chini ambacho kinasikitisha kwa kiasi kikubwa.

Nimeangalia mechi takribani nne, zote naona ziko katika kiwango duni na kinachonishangaza, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB) ni kama wanaona mambo hayo ni sahihi.

Adhabu kwa waamuzi hazichukuliwi mara moja kwa wakati, hakuna taarifa kuwa walionywa ndiyo maana hakukuwa na adhabu na ukimya umekuwa juu.

Kuendelea hivi maana yake hata wao wanaridhika na hii hali au wanaona kawaida, jambo ambalo litakuwa na matatizo mengi mwishoni.

Matatizo yatakuwa mengi kwa kuwa tu, ligi hii ni tofauti na ile ya msimu uliopita kwa maana mbili ambazo zinapaswa kuangaliwa sana.

Msimu uliopita ulikuwa na timu 16, kila moja ilicheza mechi 30 kwa mgawanyo wa 15 kwa 15. Lakini msimu huu kuna timu 20, maana yake kila timu itacheza mechi nane zaidi kwa kuwa ni 38 ikiwa ni 19 kila mzunguko na ipo miwili.

Ongezeko la mechi nane, si dogo katika ligi maana unazungumzia pointi 18 ambazo kila timu ingependa izipate na hakutakuwa na ulaini.

Sasa jiulize, uchezeshaji wa waamuzi hao tayari umeshaanza kuonyesha uchovu mapema kabisa. Kama wamechoka mwanzoni, mwishoni itakuwa vipi.

Uamuzi ambao wamekuwa wakitoa katika mechi za ligi unashangaza sana. Wanakataa penalti za timu, sehemu ya kutoa kadi, hawatoi, isiyo ya kutoa wanatoa. Wamekuwa na kiwango cha mchangani badala ya ligi kuu.

Kinachonishangaza zaidi aina ya makosa yamekuwa yakizidi kutokea mechi moja baada ya nyingine na yakajirudia halafu hakuna marekebisho wala anayekemea.

Waamuzi hawa wa ligi kuu wanafanya hivi, jiulize wale wa Ligi Daraja la Kwanza na ligi kuu ambazo hazionekani kwenye runinga kwa kiwango kama hiki inakuwaje kule.

Awali niliwahi kuandika kwamba waamuzi hawapaswi kushawishika na rushwa kwa kuwa tu sasa hakuna mdhamini wa ligi kuu. Ila safari hii ninajiuliza, ni uwezo duni au ndiyo wameanza kushawishika?

Mechi ya Simba ya Yanga, madudu yalikuwa mengi. Nimeangalia ile ya African Lyon na Simba, nayo kero kabisa. Lakini zaidi ya mechi nne sasa mabao halali yameshakataliwa na waamuzi ambao unawaona ni kama watu wasiojitambua au unapata hisia huenda wanafanya makusudi kwa kuwa wana faida binafsi!

Uamuzi mbovu wa waamuzi, ni hatari sana kwa kuwa soka linashirikisha mashabiki ambao wakati mwingine wanaweza kuzidiwa na jazba kutokana na mlolongo mrefu wa madudu yasiyoisha.

Hakuna mjadala katika hili, TFF na TPLB wanapaswa kulifanyia kazi kwa muda mwafaka kabla mambo hayajaharibika zaidi.

Ninaamini wana watu wanaofanya tathmini ya mwenendo. Hawapaswi kuwa wale wanaopingana na ukweli, badala yake wakubali na kufanyia kazi ili kuweka usahihi.

Hatuwezi kuwa na ligi bora wakati tuna waamuzi wa kubahatisha.

2 COMMENTS:

  1. Umeongea siasa, ulitakiwa utaje moja kwa moja game unazolalamikia na madudu gani yaliyofanyika ili iwe rahisi kufanya reference!! Issue ya kadi hata ulaya kumekuwa na malalamiko kwakuwa muda mwingi inategemea refa amelionaje tukio na analipa uzito gani!!

    ReplyDelete
  2. Mimi nasema goli la SIMBA lilokataliwa zidi ya yanga kwa madai ya offside ni goli halali kabisa.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic