Ndoto za kucheza fainali za mwakani za michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) zitakazofanyika Cameroon zinaweza kutimia iwapo tutapata ushindi leo ugenini dhidi ya Visiwa vya Cape Verde.
Wachezaji wa Taifa Stars wanapaswa wajue kuwa wana jukumu zito leo chini ya kocha wake Mnigeria Emmanuel Amunike na jukumu lenyewe ni kupata ushindi leo ugenini. Katika soka hilo linawezekana.
Hii itakuwa mechi ya kwanza kabla ya marudiano tarehe 16, mwezi huu hapa jijini Dar es Salaam. Cha muhimu ni kwa wachezaji wenyewe kupambana na kuweka utaifa mbele.
Tumezikosa fainali za mataifa ya Afrika tangu tulipofuzu kwa mara ya kwanza mwaka 1980 na tangu hapo tumekuwa hatufiki mbali katika hatua ya kufuzu. Fainali za mwakani kila kundi linatoa timu mbili hivi na hatua hiyo kweli tushindwe kufuzu?
Huu ni wakati wetu na sisi kuona tunakwenda katika fainali hizo za mwakani kwani mazingira yanaonekana meupe kwetu, hakika unaweza kusema hii ni zamu yetu.
Kama karata zetu tutazichanga vizuri leo, tunaweza kuanza kuona mwanga wa kuikaribia Cameroon hapo mwakani kwenye fainali hizo.
Wachezaji wa Stars wanapaswa kucheza kwa kujituma leo na wahakikishe wanafunguka na kushambulia muda wote. Mfumo wa timu zetu nyingi Afrika ugenini tumekuwa tukijihami lakini kwa vile tunahitaji matokeo ni lazima tufunguke.
Licha ya idadi ndogo ya mashabiki waliokwenda, siye tuliobaki tunapaswa kuomba dua sana kwa vijana wetu ili wapeperushe bendera. La kushauri kwa TFF hii, mechi ilipaswa ihamasishe Watanzania kwa muda mrefu wajipange waende na Stars. Kumbuka shabiki siku zote ni mchezaji wa 12 sasa kama unacheza bila shabiki hamasa inakosekana.
TFF iwe na kitengo kitakachoshughulika na masuala ya hamasa na hicho ndicho kitakachokuwa kinahamasisha watu wasafiri na Stars katika mechi za ugenini kama hii ya leo. Wenzetu kote wamekuwa wakisafiri na mashabiki wao kuifuata timu ya taifa.
Hili linapaswa kuwa somo wakati mwingine, kwamba mechi za namna hii inabidi zipewe hamasa ya kutosha na kuwawezesha Watanzania kuamka zaidi.
Najua Watanzania wengi wataifuatilia mechi hii, lakini ilipaswa kuwepo hamasa ya kuwawezesha wengi kwenda kuishuhudia ili kuwapa nguvu wachezaji ambao bila shaka wangeona Watanzania wenzao wamejitokeza kwa wingi uwanjani, basi wangejituma zaidi na zaidi.
Tukiachana na hilo, niwasisitize Watanzania kuendelea kuomba dua zao na wale watakaofanikiwa kuwa uwanjani, basi washangilie kwa nguvu kubwa na kuhakikisha hawatulii kwa muda wote wa mchezo ili kuwawezesha wachezaji kupambana kwa morali ya juu.
0 COMMENTS:
Post a Comment