October 14, 2018







Na Saleh Ally
NILIWAHI kuzungumza na rafiki yangu mmoja kuhusiana na masuala ya michezo ingawa yeye hapendi michezo pia ni mtu wa masuala ya uzalishaji wa vinywaji baridi katika kiwanda kimoja.


Rafiki huyo ambaye sasa ni injinia, aliniambia hapendi michezo kwa kuwa anaona kama jambo la watu ambao hawako makini na wakati wote wanafanya utani tu.


Aliniambia angependa kuwa sehemu ya familia ya michezo na angeweza kufanya hivyo kama angekuwa anaishi nje ya Tanzania ambako anaona michezo ina tofauti kubwa na hapa nyumbani.


Wakati anazungumza, niliamini alichoniambia nilikuwa ndicho nafikiria. Lakini kwa lengo la kujifunza, nikaona si vibaya kumuuliza kuhusiana na neno lake kuwa angependa michezo kama angekuwa anatokea nje ya Tanzania au angependa michezo kama angekuwa nje ya Tanzania.


Akasema yeye ni mtu anayependa vitu makini, kama ni mjadala basi ni vyenye hoja za msingi. Lakini ameona katika michezo na hasa soka, watu wanapenda kubishana tu bila sababu za msingi.


Akasisitiza, ikiwa ni kwa maandishi, wapenda mpira wengi wanakimbilia maneno makali au matusi badala ya kupita kwenye hoja inayojadiliwa. Akanishangaza zaidi alipokwenda mbali zaidi akisema, kama si kwa maneno, ukiwakuta watu wa soka wanajadiliana, ishu haiishi na hata uzungumzaji wao utafikiri watu waliokunywa pombe imewazidi kwa kuwa wanazungumza kwa sauti ya juu na wakati mwingine hapendi hata kuwa karibu nao. 


“Wakati naanza maisha, nilipanga chumba kimoja Magomeni, niliipenda sana ile sehemu na mwenye nyumba alikuwa mtu mzuri sana. Bugudha kubwa ilikuwa watoto wake wawili, mmoja Yanga na mwingine Simba. Walikuwa wakipayuka, wakati mwingine hata kupigana na wakija marafiki zao ndiyo ilikuwa balaa kabisa,” alinieleza.


Nilijisikia vibaya sana, nilijaribu kumfafanulia mambo kadhaa ikiwemo kumueleza soka wakati mwingine inahitaji watu waelewa kama yeye ili kuwapunguza wasio waelewa ambao wamekuwa tatizo kubwa sana.

Nimemkumbuka rafiki yangu huyo baada ya kuona sehemu mbalimbali, yaani mitaani au kwenye mitandao ya kijamii, baadhi ya watu wakiligeuza suala la kutekwa kwa mwanachama maarufu wa Simba, Mohamed Dewji kama utani wa kawaida.


Mo Dewji alitekwa juzi na watu wasiojulikana. Imezua taharuki kubwa na vyombo vya dola vimekuwa vikipambana kwa kila njia kuhakikisha anapatikana.


Kuna hofu kubwa zaidi baada ya kuelezwa kwamba waliomteka ni raia wa kigeni. Hatujui ni wa nchi gani, wana lengo gani na sababu kuu ni zipi? Hii inazidi kuzuia hofu miongoni mwetu.


Wako wanaotumia kigezo cha kuwa watani wa Simba, lakini wako wanaoona furaha wakiamini matatizo kwa Mo Dewji ni matatizo kwa klabu ya Simba, maumivu kwa wanachama na mashabiki wa klabu hiyo na huenda ni ahueni kwao.


Suala la Mo Dewji halihitaji utani hata chembe kwa kuwa watoto wake wadogo, mkewe, baba yake na familia yake kwa jumla wanaumia sana. Wanapaswa kuliwazwa kwa maneno mazuri na si kuona yale ya utani wa kipuuzi au upuuzi unaofichwa na utani au mjadala wa mchezo wa soka ukiendelea kuwaumiza.


Kama soka inawafurahisha, iko haja ya kutambua umuhimu wa mtu hasa katika mazingira aliyopo Mo Dewji kwa kipindi hiki, hakuna kati yetu anayejua alipo, usalama wale na kadhalika.


Vipi unaweza kuingiza utani katika jambo kama hilo, wewe ni mwanadamu pia. Unapaswa kujiuliza maumivu ya wengine pia hasa binadamu wenzako.


Kuna mtu mmoja nilipomuuliza na kumueleza si sahihi, akaniambia wakati wa matatizo ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji, wako Simba walifurahia.


Nilimueleza tulikemea pia, lakini nikamkumbusha tofauti ya yaliyomtokea Manji aliyekuwa chini ya vyombo vya usalama na Mo Dewji aliye katika hatari na hatujui hatma yake ni ipi hasa.

Kama haitoshi, nikamkumbusha kuhusiana na matatizo kuwa kwa vile yote ni matatizo, suala la mmoja kumjali mwingine ni muhimu sana kuliko kuendelea kupeleka maumivu kwenye maumivu.


Kushangiliana lengo si kupeana maumivu nje ya mchezo wenyewe. Kama ingekuwa timu moja imepoteza mchezo, nyingine inawazodoa, hiyo ndiyo raha yenyewe ya ushangiliaji.


Hapa katika maisha ya mwanadamu, vipi kutakuwa na ushangiliaji wa maumivu ya mwanadamu mwenzako, mwajiri wa wenzako, baba wa watoto, mme wa mke ambaye ni kama dada kwako au mwanafamilia wa watu wanaoumia kutokana na maumivu yake na hofu husika.


Tuwe makini, tubadilike na tujipime na ikiwezekana tuelekeze nguvu nyingi kumuombea Mo Dewji apatikane akiwa salama, halafu baada ya hapo, michezo au utani utaendelea.




9 COMMENTS:

  1. Uandishi mzuri Mr. Saleh, ahsante kwa kutukumbusha hilo na Mwenyezi Mungu akujaalie.

    ReplyDelete
  2. Mapenzi baina yetu yanazidi kupotea ndio maana wengi wetu huruma na upendo vinazidi kuangamia kwa kasi ya ajabu huku chuki na roho mbaya vikichukua nafasi. Ni kwa sababu gani na kwanini watu badala ya kuhurumiana na kupeana moyo katika matatizo na mashaka mbalimbali tunafurahia matatizo ya wenzetu kana kwamba sisi hatutafikwa majanga!? Yapo/Lipo tatizo linahitaji mjadala wa kitaifa ili tuepukane na kuishi maisha yasiyo ya kitanzania. Neno NDUGU linazidi kupotea huku misamiati mipya ikichukua nafasi yake si kiashiria chema katika udugu wetu tuliouenzi. Dalili za kukomaa kwa ubaguzi zinaanza kuota mizizi na hazikemewi ipasavyo. Pasina ubishi wala kuhitaji utafiti mkubwa ubaguzi upo wengi tumejisahaulisha kina nani walitoa michango yao wakati wa uhuru na tunajenga matabaka ambayo yatagharimu vizazi vyetu. Hatujachelewa ikiwa tutataka tunaweza kubadilika na kurudi katika mstari. Tusiokubali kubadilika tukaendelea na kejeli, ubaguzi na kunyanyapaana katika matatizo HAKUNA ANAYEIJUA KESHO YAKE, SOTE TU VIUMBE NA HAKUNA AJUAE NANI NI MSAADA KWAKE NA LINI.

    ReplyDelete
  3. Allah Amjaalie MO huko aliko na Kwa uwezo wake Allah Amrejeshe kwenye maisha yake ya kawaida

    ReplyDelete
  4. Bro nakukubal sana asante kwa hli

    ReplyDelete
  5. Mmekuwa wapole eeee mmesahau eeee mla kunde na mzoa maganda

    ReplyDelete
  6. Saleh ungezungumza wazi bila ya kumumunya) kuwa mashabiki wa Yanga wengi wao ni wajinga ukilinganisha na wale wa Simba. Manji alipopata matatizo hakuna shabiki hata mmoja wa Simba aliefanya dhihaka au kutoa maneno ya kijinga. Manara alitoa wito wa mashabiki wa Simba na Yanga kuwa kitu kimoja timu zetu zinapocheza na timu za nje lakini kilichotokea ni matusi na kejeli kwa Manara hiyo ni mifano michache inabidi lazima tubadilike.

    ReplyDelete
    Replies
    1. Ni akina nani waliokuwa wanamshihaki manji na kumuita mla ngada!? Mkuki kwa nguluwe..

      Delete
  7. Tatizo lako unaansika kuuza badala ya kufanya tafiti!! Binadamu hatufanani, uneajaribu kufanya utafiti ili kuanfalia ni wapenzi wangapi wa Yanga wanaofurahia tukio hili!? Yanga ina uongozi, na viongozi wameshatoa tamko la kulaani! Duniani kote, hakuna sehemu ambayo shabiki wote wanaweza ongea lugha moja. Usiongee na watu wawili ukafanya kuwa mawazo ya watu wote. Tatizo la Champions mnapenda kuandika mawazo yenu wenyewe na kuyafanya taarifa

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic