October 19, 2018




 
Na Saleh Ally,

KOCHA Emmanuel Amunike amefikisha mechi tatu za mashindano akiwa na kikosi cha Taifa Stars na takwimu zinaonyesha ameishaonja matokeo yote matatu.

Amunike ameonja matokeo ya sare, kushinda na kufungwa. Alianza na sare ya 0-0 dhidi ya Uganda maarufu kama The Cranes ambao walikuwa nyumbani.

Akakumbana na kipigo akiwa ugenini dhidi ya Cape Verde, Taifa Stars ikalala kwa mabao 3-0. Aliporejea Dar es Salaam, Stars ikaitwanga Cape Verde 2-0 na kulipa kisasi.

Ushindi dhidi ya Cape Verde, umeamsha matumaini ya Stars kwamba safari ya kucheza Afcon nchini Cameroon, mwakani bado ipo na kinachotakiwa ni kushinda mechi zote mbili, ya ugenini dhidi ya Lesotho halafu nyumbani dhidi ya Waganda ambao unaweza kusema ‘wameishatusua’.

 
Wakati anapitia matokeo yote hayo, Amunike, mchezaji wa zamani wa FC Barcelona ya Hispania na timu ya taifa ya Nigeria ‘Super Eagle’ amekumbana na mambo mengi kwa wakati mmoja lakini ameonyesha vitu ambavyo vinaonyesha ni kocha mzuri anayepaswa kuungwa mkono kwa kuwa anaweza kutufikisha mbali.

Amunike ni msikifu, mbunifu na asiye muoga kwa maana anataka kufanya kile anachoona sahihi na huyu ni kocha mwenye akili ya mipango sahihi na kazi yake na yule ambaye angetaka ushindani au majibizano.

Mwendo wa Amunike unaonyesha ni mtu aliyepania maendeleo au mafanikio ya kikosi chake na yeye kujitengenezea CV ya uhakika baada ya kufanikiwa. Ndiyo maana utaona karibu kila maoni ameyafanyia kazi na tumeona kilichokuwa sahihi kimefanya kazi, kile ambacho hakuona ni sahihi, ameachana nacho bila ya kujali nani amesema nini.

Suala la wachezaji wa Simba kuchelewa kambini, alichukua hatua na hakukuwa na mambo ya siasa tena kama ambavyo tumezoea Simba na Yanga kutaka waonekane ni wakubwa sana na hata wakiharibu waangaliwe tu.

Pamoja na kelele nyingi za mashabiki wachache ambao waliamini wana nguvu sana kuliko taifa zima la Tanzania, Amunike hakutetereka ameendelea kufanya kazi yake, hakuonyesha kinyongo na wachezaji wa Simba na badala yake kaangalia kila anayefaaa kulingana na anachohitaji kama kocha na amemtumia au kumuita.

Kikosi alichokitumia Uganda kilifanya vizuri, kikacheza jihadi na kupata sare ngumu dhidi ya Uganda ambao unawaona wako vizuri wakiongozwa na Emmanuel Okwi lakini hawakufurukuta kwao.

Baada ya mechi hiyo, wengi waliona mambo kadhaa yalipaswa kufanyiwa mabadiliko. 


Yeye kama kocha na wenzake wa benchi la ufundi, kuna yale waliona, kuna maoni wakachukua na mabadiliko yakafanyika. Mechi ya Cape Verde wakati tunapoteza utaona kuna wachezaji kama Gadiel Michael, Hassan Kessy na hata David Mwantika aliyefanya vizuri sana Uganda, iliwashinda. Soka liko hivyo kwa kuwa si kila siku ni Ijumaa.

Baada ya hapo, maoni yametolewa, kocha mwenyewe na wenzake wameangalia na mwisho akafanya mabadiliko ambayo inaonyesha wazi yalihitajika na kufanya kazi.

Amemuita Erasto Nyoni, licha ya kwamba wako waliolaumu mfululizo kuhusu Jonas Mkude huku wakijua hakutumiwa sababu ni majeruhi. Nyoni kaitwa na kucheza na kafanya vizuri sana. Hapa Amunike hakutaka kushindana kuonyesha inawezekana bila yule aliyetajwa.

Alichoangalia ni uhalisia na nia ya kuona timu yake inafanya vizuri. Amefanikiwa kwa kuwa Nyoni alicheza vizuri dhidi ya Cape Verde.

Mwantika alifanya vizuri Uganda, ndiyo maana alimtumia Cape Verde ambako alifanya vibaya. Haraka amebadilisha, amempa nafasi Yondani ambaye alikaa benchi Cape Verde baada ya kubaki Dar es Salaam na kushindwa kwenda Kampala.

Kweli Yondani amecheza vizuri na kuwa msaada mkubwa. Usisahau, kulikuwa na maoni kidogo kuhusiana na Fei Toto, aliporejea kutoka Cape Verde, kidogo tu kampa nafasi tena katika mipango sahihi baada ya Taifa Stars kuwa inaongoza kwa mabao 2-0.

Kinda huyo ameingia na kupiga zile pasi zake ndefu na fupi zinazofika, akasaidia kutimiza malengo aliyotaka kocha huyo.

Bila shaka, Amunike kaonyesha si kocha anayelenga kuzozana, kuonyeshana au kutaka kulumbana akionyesha yeye ni kocha anajua na hasikilizi mtu. Badala yake anaangalia maoni ya ukweli wa mambo kwa usahihi.

Kocha huyu anapaswa kuungwa mkono huku tukiangalia na kukumbuka kuhusiana na ukweli wa soka, kwamba halina uhakika wa ushindi hadi baada ya dakika 90 na pia tuachane na kuwa mashabiki wa timu yetu ya taifa hadi inaposhinda tu, ikitoka sare au kupoteza tunahamia kwingine. Huo ni utumwa wa fikra kwa kuwa hakuna timu inashinda mechi zote na haijawahi kutokea.


4 COMMENTS:

  1. Mwendelee kujipamba ivyo mpaka mwisho maana timu yetu kwa magazeti ijambo tuje kupigwa 7 kama aligeria ndio mtaipatapata

    ReplyDelete
  2. Ifahamike tu hakuna binaadamu aliekamilika kila mtu anamapungufu yake na ni vigumu sana mtu kuyaona mapungufu yake yeye mwenyewe binafsi na ndio maana mchezo wa mpira unakupa picha halisi kuwa binaadamu anahitaji kukosolewa au kuelekezwa na mtu mwengine ili awe bora zaidi kwani licha ya umahiri wa Mesi katika kusakata kandanda lakini kuna kocha anaemsimamia,kuna marefaree,kuna hata wapenzi pengine kuguna kwao anapofanya vibaya ni msaada kwake wa kujirekebisha. Watanzania sio wapumbavu. kwa kiasi fulani ni wafuatiliaji wazuri wa soka na timu yao ya taifa isipokuwa vizuri wanajua na ni vizuri kuwa hawakai kimya wanasema na kusema kwao sio kwamba itafsiriwe kuwa wanachuki na timu yao au viongozi wake la hasha ni kutaka kuona wahusika wanarekebisha mangufu yaliyopo. Hakuna haja tena kurejesha au kukumbusha maigizo ya kuondolewa kwa wachezaji wa Simba kambini kwa madai ya utonvu wa nidhmu baada ya kuchelewa kuingia kambini kwa masaa au siku moja ilihali kuna wachezaji wengine waliingia kambini siku nne baadae kilichofanyika ni wa kuwatoa kafara wachezaji wa Simba pasipo na sababu za msingi na kuwajaza wachezaji pressure wakiwa karibu na mechi muhimu kabisa zidi ya Uganda. kama aliechukua uamuzi ule awe kocha mwenyewe au uongozi wa TFF walifanya maamuzi yale kibabe bila ya kufuata kanuni na taratibu za FIFA na sio kitu kizuri hata kidogo. Hatutaki kuwa wa kweli ila kama Taifa stars ingesafiri na wachezaji wake pamoja na wale wa Simba katika mechi ya Uganda basi uwezekano wa kuondoka na ushindi siku ile ungekuwa mkubwa.Mfano watu walihoji kwanini Nyoni kaachwa hawakuwa wakihoji kwa upenzi au ushabiki bali wanaujua uwezo wake na angeweza kuwa mchango mkubwa kwa timu. Na bado tutaendelea kuwashangaa wale wanaoisimamia timu hiyo kama wataendelea kuwaacha wachezaji amabao tayari walishashiriki mashindano ya Africa kwa ngazi za vilabu na bado wapo fiti mfano akina kichuya, Ibrahimu Ajibu,Mohamed Husein na wengineo ili kuwa na wachezaji sahii na wanastahiki nadini ya Taifa Stars.

    ReplyDelete
  3. Kwani wachezaji waliokaitwa tena hawakufanya vizuri Uganda?
    Hao unaosema waliingia siku 4 ilikuwa baada ya kuondolewa wale wa simba na yanga na wale wanaocheza nje.
    Narudia tena acha ushabiki wa umbumbumbu.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic