October 5, 2018


Mwanachama wa Klabu ya Simba ambaye anaelekea kuwa mwekezaji klabuni hapo, Mohamed Dewji ‘Mo’ ameonekana kupania kufanya kweli baada ya kukamilisha ahadi yake ya kutengeneza uwanja wa kuchezea wa klabu hiyo uliopo Bunju jijini Dar.

Simba inamiliki uwanja huo wenye ukubwa zaidi ya ekari nane uliopo Wilaya ya Kinondoni nje kidogo ya Dar ambapo ulinunuliwa enzi za aliyekuwa mwenyekiti wa klabu hiyo, Hassan Dalali lakini umekuwa na mchakato wa kusuasua katika ujenzi wake.

Championi Ijumaa lilifika eneo hilo jana Alhamisi na kushuhudia ujenzi ukiendelea ambapo lilifanya mazungumzo na mkandarasi, Daniel Matiko kutoka Kampuni ya Masasi Construction Co. Ltd ambayo ndiyo inayojenga uwanja huo.

“Tumeanza ujenzi huu wiki mbili zilizopita kwa kusafisha kisha kumwaga vifusi, hadi sasa udongo mwingi tumemwaga na kufikia levo hii, tunahitaji kuongeza udongo mwingine wa mwisho ili uwanja uwe juu kwa ajili ya kukwepa maji.

“Tunatarajia kujenga uwanja wa kisasa wenye viwango vya kimataifa, tutatandaza mabomba chini kwa ajili ya kupitishia maji pindi mvua itakaponyesha ili maji yaweze kwenda chini kwa kutoathiri uwanja, tutakamilisha kazi hii Februari mwakani.

“Tutakapokamilisha hatua ya awali, uwanja utakaguliwa na vyombo husika ikiwemo TFF ili tuweze kuendelea na hatua nyingine, kwani tunahitaji kutengeneza pichi ya viwango vya kimataifa.

“Tutaweka nyasi bandia katika uwanja huu ambazo kwa sasa tayari zimeshaandaliwa, pia tutazungushia ukuta wakati tukiwa tunaendelea na shughuli nyingine za ujenzi.

“Hadi sasa tuna wafanyakazi 15 wanaoshughulikia uwanja na tutaendelea kuwaongeza kadiri muda unavyokwenda kulingana na mahitaji.

“Ukubwa wa uwanja upo mita 109 kwa urefu na upana mita 70, tutakapokamilisha ujenzi katika eneo la kuchezea watakuja wataalamu wa viwanja kwa ajili ya kuweka magoli na kupima urefu wa uwanja wanaouhitaji kwa kuwa sisi tumeweka viwango vya kimataifa,” alisema Matiko.

CHANZO: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic