Sasa ni rasmi kwamba dakika yoyote kuanzia sasa linaweza kutoka tangazo la Simba kuachana na kocha wao msaidizi, Mrundi Masoud Djuma.
Championi ambalo ni gazeti dada la Spoti Xtra ndilo lilikuwa la kwanza kuripoti habari ya Simba kufikia uamuzi wa kutemana na kocha huyo kipenzi cha mashabiki na wanachama kutokana na mbwembwe zake mazoezini na kwenye mechi mbalimbali pamoja na rekodi zake ndani ya Msimbazi.
Habari za uhakika ambazo Spoti Xtra imezipata jana Jumatano jioni ni kwamba Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems ameusisitizia uongozi kwamba hayuko tayari kufanya kazi na kocha huyo na akaiambia bodi ya klabu hiyo sababu zake.
Habari zaidi zinasema kwamba Mbelgiji huyo alianza kuzinguana na Masoud tangu timu hiyo ikiwa kambini nchini Uturuki na waliporejea Dar es Salaam wakapatanishwa yakaisha lakini baadaye yakaibuka tena.
Habari zinasema kwamba Masoud alipoitwa kwenye uongozi alikiri kuna mambo kati yao hayakuwa sawa lakini akawa tayari kuomba radhi ndipo baadhi ya viongozi wakaafikiana kwamba kama wakiendelea kumuacha, misimamo ya kocha mkuu huenda ikaleta mikwaruzano baina yao na kazi ikaharibika na wakakosa kutimiza malengo yao.
Habari zinasema kwamba kocha mkuu anadai kwamba Masoud amekuwa akimsema vibaya pembeni ingawa Mrundi huyo alipotafutwa na Spoti Xtra hakupatikana kutoa ufafanuzi.
Msemaji wa Simba, Haji Manara hivi karibuni alinukuliwa baada ya kipigo cha Mbao kwamba kuna maamuzi magumu watayafanya punde.
Manara aliwahi kulalama kwenye vyombo vya habari kwamba Masoud amekuwa akiwasiliana na wanachama ambao wamekuwa hawaelewi mambo yalivyo na badala yake kuishia kuulaumu uongozi.
CHANZO: SPOTI XTRA
0 COMMENTS:
Post a Comment