Na Saleh Ally aliyekuwa Sudan
HALI ya hewa na jiji la Khartoum ni joto sana. Kwa wale ambao wamekuwa wakiamini Dar es Salaam au Tanga kuna joto sana, wanaweza kushangazwa wanapokuwa hapa.
Katika maisha ya kawaida, wakazi wengi wa jiji la Khartoum hupenda kuingia mitaani kuanzia saa 11 jioni, jua limepoa.
Unapopita katika maeneo mengi ya jiji hili katika nyakati za mchana. Utakutana na zile feni zinazotumia maji, wakijipoza.
Hata katika mabanda ya wachuuza bidhaa kama vile nguo au viatu kama ukienda katika soko la Karume pale jijini Dar es Salaam, huku wanatumia feni.
Wakati wa jiji la Khartoum pamoja na kuwa ni wachuuzi wanaopambana na hali ya hewa hadi nyuzi joto 45, furaha yao kubwa ni mchezo wa soka.
Timu mbili za Al Hilal na El Merreikh ndiyo zinachukua watu wengi zaidi kama inavyokuwa kwa Simba na Yanga nyumbani Tanzania.
Wana wazimu hasa wa soka na wengine wako tayari kumuumiza ambaye wanamuona ni tatizo mbele yao au anaonyesha kuwa kero dhidi ya timu yao.
Mtanzania Thomas Ulimwengu ambaye amewahi kung’ara na TP Mazembe, yeye sasa ni nyota wa klabu ya Al Hilal.
Al Hilal ndiyo timu kubwa na kongwe pia maarufu na tajiri zaidi ya nyingine zote za hapa Sudan.
Huenda wengi waliamini Ulimwengu alikosea kujiunga na Al Hilal lakini ukweli Al Hilal Omdurman ni klabu yenye fedha nyingi sana.
Inamiliki hoteli kubwa ndani ya uwanja wake wa Al Hilal ambao una uwezo wa kuingiza zaidi ya watu 40,000.
Uwanja huo uko katika eneo la Omdurman, eneo ambalo unalazimika kuvuka mto Naili kutoka upande wa Khartoum kwenda ulipo uwanja huo.
Katika jiji la Khartoum na mingine, Ulimwengu ni mtu maarufu sana. Championi ambalo lilisafiri hadi Khartoum kufuatilia kinachoendelea katika maisha ya Ulimwengu, limejifunza mengi sana.
Moja kuu ni heshima kubwa aliyojijenge Ulimwengu ndani ya miezi takribani mitano ambayo amejiunga na kufanya kazi na klabu hiyo.
Katika mitaa ya jiji la Khartoum ni kazi ngumu kutembea na Ulimwengu. Iwe mitaani, sehemu za wachuuzi au kwenye majumba makubwa ya kibiashara kama Mlimani City ya dar es Salaam au Rocky City Mall ya Mwanza.
Wakati fulani, ililazimika baadhi ya walinzi kusogea na kumuondoa Ulimwengu baada ya mashabiki kuvamia na kutaka wapige picha na mshambuliaji huyo.
Pamoja na kukubali kupiga na mmoja au wawili, waliendelea kuongezeka mmoja baada ya mwingine. Mmoja baada ya mwingine ili mradi kila mmoja alichotaka ni kuona anapata picha hiyo.
Kutokana na idadi ya watu kuzidi kuwa kubwa, ililazimika walinzi kuingilia na kuokoa Ulimwengu ambaye alionekana kuzidiwa na mzigo wa mashabiki hao.
Kawaida wanamuita kwa jina la Thomas kwa kuwa lile la Ulimwengu linaonekana kuwatatiza. Lakini wakati mwingine, Ulimwengu anapokuwa mitaani analazimika kuvaa kofia ili kuficha kiduku chake kuogopa kutambuliwa.
SALEHJEMBE: Haya ni kama maisha magumu, maana unagombewa na watu hadi hauna amani?
Ulimwengu: Ni kweli unaweza ukaona kama unakosa uhuru, lakini kama ni mtumishi wa watu, unakuwa hauna ujanja. Unavumilia.
SALEHJEMBE: Umeweza vipi kuishi hivi bila ya mzozo, maana wengine walikuwa wakikurukia kwa nguvu?
Ulimwengu: Unajua hawa watu wanaonyesha mapenzi. Katika kikosi cha Al Hilal kuna wageni wawili, Mbrazil na mimi, tena yeye kachukua uraia wa Sudan. Lakini bado mimi naonekana kipenzi chao kwa muda mfupi, nalazimika kuvumilia.
SALEHJEMBE: Tulikuwa tumeongozana na dreva wako, mara nyingi nimesikia akiwaambia wewe ni John na si Thomas, kwanini?
Ulimwengu: Nafikiri ni suala la kuwakwepa mashabiki. Unajua kabla lazima waulize huyo ni Thomas. Sasa yeye anawaambia hapana, ni John, ndugu yake Thomas. Lengo ni kuwaepusha wasinivamie.
SALEHJEMBE: Nini kimewafanya wakuone wewe ni mtu muhimu kwao?
Ulimwengu: Nafikiri ni juhudi zangu uwanjani, nimefunga mabao sita katika uwanja wa nyumbani na mengine manne nje ya nyumbani. Ndani ya miezi minne na kidogo, kufanya hivyo lazima mashabiki wakupende.
SALEHJEMBE: Unafikiri ni hayo mabao pekee?
Ulimwengu: Mabao ni kitu cha kwanza, ukiwa mshambuliaji mashabiki wanapenda ufunge. Lakini pia namna ninavyojituma na kuisaidia timu, ni jambo linalowavutia sana.
SALEHJEMBE: Mara ngapi unaingia mtaani kwa wiki na kukutana na mashabiki?
Ulimwengu: Mara chache sana, hata hii kutoka kwa kuwa nilitaka kukuonyesha mji. Lakini nashinda ndani zaidi. Baada ya mazoezi nakuwa naangalia ‘muvi’ na kujifunza mambo mengine.
SALEHJEMBE: Ukiachana na mashabiki wanaokufanya uishi kama mfalme, unaweza kuvumilia hali hii ya joto hadi nyuzi joto 45?
Ulimwengu: Kweli ni kazi, lakini nimekuja kufanya kazi katika mazingira haya lazima niwe tayari.
SALEHJEMBE: Wakati wa mechi unawezaje kuvumilia, au unafanya mazoezi mchana?
Ulimwengu: Mara moja moja tunacheza mechi mchana. Mara nyingi sana mechi ni usiku na huku ndiyo wanapenda hivyo. Hivyo inapunguza ukali wa joto.
SALEHJEMBE: Ushindani wa ligi ya huku ni Al Hilal na El Merreikh pekee, au kuna timu nyingine?
Ulimwengu: Zipo, kuna Shandy na nyingine nyingi. Ligi yao ni ngumu sababu ya ushindani na wakati mwingine fitna za kimchezo nazo ni shida.
SALEHJEMBE: Fitna zipi?
Ulimwengu: Kuna wakati waamuzi wanafanya mambo unaweza kushangaa. Lakini kw akuwa ni mchezaji ninayefuata weledi, najikita zaidi katika kazi.
SALEHJEMBE: Mashabiki wa huku kwa ujumla wakoje?
Ulimwengu: Wanazipenda sana timu zao, mfano hao wa Al Hilal, hata kama timu ndogo wanajua mtashinda lakini wanajitokeza kwa wingi sana na wanajaza uwanja. Wanashangilia mwanzo mwisho kwa kuwa wanapenda timu yao na wanapenda mpira.
SALEHJEMBE: Unawezaje kuufananisha ugumu wa ligi ya hapa na DR Congo?
Ulimwengu: Nafikiri hapa kuna ugumu zaidi kiuchezaji. Watu wako makini zaidi na wananuia ushindi. Congo pia si kwamba wako chini, sema shida zaidi ilikuwa ni viwanja.
SALEHJEMBE: Viwanja vilikuwa na nini?
Ulimwengu: Viwanja vya Congo vingi vilikuwa vibaya hasa vile vya mikoani. Lakini tulikuwa tunapambana vilivyo kuhakikisha tunafanya vema.
SALEHJEMBE: Tumeona mazoezi unakwenda kufanya umbali wa zaidi ya kilomija 20 hivi, haikusumbui?
Ulimwengu: Ndiyo kazi zaidi, naishi Sudan nakwenda Omdurman. Lakini ni kawaida kwa kuwa nina usafiri wangu.
SALEHJEMBE: Yaani unaendesha mwenyewe?
Ulimwengu: Hapana, bado sijaanza kuendesha huku. Ila kuna dereva maalum na gari ambayo ananisubiri kuanzia asubuhi hadi jioni na ndiye ananipeleka mazoezini na kadhalika.
SALEHJEMBE: Malipo hakoje hapa?
Ulimwengu: Malipo ni mazuri lakini viongozi wanaunga mkono wachezaji.
SALEHJEMBE: Wanaunga vipi mkono?
Ulimwengu: Wanapenda kuona watu wanasonga mbele. Ukifanya vizuri zaidi hapa kuna nafasi ya kwenda mbele na mbali.
SALEHJEMBE: Umekuwa ukisumbuliwa na majeraha mfululizo. Uliweza vipi kujikwamua na unaendeleaje?
Ulimwengu:…
USIKOSE KESHO JUMAMOSI kujua namna Ulimwengu anavyoishi kwake, suala la chakula na maslahi katika soka la Sudan.
Interesting
ReplyDelete