DIRISHA DOGO SIMBA NI MZIKI MNENE, MAMBO YAKO HIVI
Wakati usajili umefunguliwa Novemba 15, mwaka huu, tayari Simba wameshajiweka mguu sawa kuhakikisha wanasajili majembe yanayoweza kuwasaidia kufanya vizuri kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika na Ligi Kuu Tanzania Bara.
Simba watacheza michuano ya kimataifa mwaka huu na mechi yao ya kwanza itakuwa Novemba 28, dhidi ya Mbabane Swallows ya Swaziland, ili washinde mechi hiyo Simba wanatakiwa kuwa na kikosi kamili.
Tayari vigogo wa Simba wametajwa kuanza mazungumzo ya usajili na Thomas Ulimwengu, ambaye kwa sasa hana timu, Francis Kahata ambaye ni staa kwenye kikosi cha Gor Mahia, Salum Kimenya akitokea Prisons na beki Abdul Rwatubyaye na winga Caleb Bimenyimana wakitokea Rayon Sports ya Rwanda.
Mastaa wote hawa wanatakiwa na timu hiyo, ingawa kila mmoja amekuwa akisema lake, lakini wakipatikana wote watabadili kabisa sura ya kikosi hicho cha Msimbazi . Ulimwengu ambaye amekuwa akicheza kama mshambuliaji wa pili au winga ametajwa kuwa anaweza
kusaini Simba kwa miezi sita na tayari jina lake limekabidhiwa kwa kocha wa timu hiyo, Patrick Aussems ambaye amesema alishamuona Taifa Stars.
Mshambuliaji huyo wa timu ya taifa ambaye alivunja mkataba na timu yake ya Al Hilal ya Sudan hivi karibuni, anaweza kukamilisha mazungumzo na Simba baada ya timu ya taifa kurejea kutokea Lesotho inakokipiga jioni hii na wenyeji. Kama akisajiliwa kuna
uwezekano mkubwa akaingia kwenye kikosi moja kwa moja kutokana na uwezo wake na uzoefu wa michuano ya kimataifa alionao. Ulimwengu aliwahi kuitumikia, TP Mazembe na kuiongoza kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini pia alishiriki michuano ya Klabu Bingwa Dunia akiwa na
timu hiyo na akitua Simba atakuwa ndiye mchezaji aliyecheza michuano mikubwa kuliko wengine wote. Ishu ya Kahata na Simba inaonekana kufanyika kwa siri kubwa, ingawa mara kwa mara wamekanusha kuwa hawana mpango naye, lakini kwenye usajili hilo ni jambo la kawaida.
Staa huyo wa Gor Mahia ndiye mchezaji bora zaidi kwenye kikosi hicho ambaye aliiongoza hivi karibuni kuvaana na Everton wakalala kwa mabao 4-0, amekiri kwamba kuna kitu kinaendelea kati yake na Simba.
Kabla Meddie Kagere hajatua Simba, Kahata ambaye anaweza kucheza nafasi mbili, winga wa kushoto au kiungo mshambuliaji alifanya mazungumzo na Simba, lakini dau lake likawa kubwa.
Hivi karibuni alinukuliwa akisema kuwa yupo tayari kutua kwenye timu hiyo kwa kuwa anataka kucheza pamoja na Meddie Kagere, Simba hawajawa wazi lakini ukweli ni kwamba wanataka huduma ya mchezaji huyo raia wa Kenya.
Inavyoonekana ni kwamba akiingia kwenye timu hiyo atabadilisha kabisa kikosi cha Simba, lakini kasi yake na pasi zenye macho inaweza kuisaidia timu hiyo kuwika Afrika.
Hata hivyo, pamoja na Simba kusema kuwa sasa wanataka kufungia kazi sehemu mbili, mbadala wa Shomari Kapombe na Jonas Mkude, wanaonekana kuwa wanaweza kurudi fasta kwa Kimenya.
Hivi karibuni Simba walimwita Kimenya wa Prisons jijini Dar na kukaa naye kuweka mipango ya beki huyo kuhakikisha anatua Simba ili akawe mbadala wa Kapombe, lakini pamoja na kumweka dau nono mezani bado askari huyo aligoma kusaini.
Sasa kitendo cha Kapombe kuumia kwenye mazoezi ya timu ya Taifa, Taifa Stars, inaonekana kuwa Simba lazima wafanye juhudi nyingine kubwa kumpata beki huyo mwenye kasi na krosi matata ili aweze kuisaidia timu hiyo.
Hata hivyo, bado Simba wanaonekana kuwa wanaweza kumsajili beki Abdul wa Rayon siku chache zijazo, huyu naye anaonekana kuwa anaweza kuanza moja kwa moja au akaanzia benchi, huyu ameshasema kuwa Simba wamemfuata.
Winga wa Rayon, Caleb ambaye kwasasa yupo kwao Burundi, aliliambia Spoti Xtra wiki hii kwamba amezungumza na Simba na anachosubiri ni wao wamtumie mkataba wa awali aje Dar es Salaam kukamilisha dili.
Ni dhahiri kuwa zimebaki siku 26 za Simba kuhakikisha wanakuwa na kikosi tishio kama hicho hapo mbele ili waweze kuwika kimataifa na kutwaa ubingwa wa ligi kuu.
CHANZO: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment