November 19, 2018


Wakati sakata la Yusuf Manji likiendelea kuwaumiza vichwa wengi juu ya nafasi yake ndani ya klabu hiyo, hatimaye mwenyewe amewajibu Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa staili ambayo unaweza kuiita ni ya kibabe.

Kwa muda mrefu tangu Yanga itakiwe kufanya uchaguzi mkuu, TFF iliagiza zijazwe nafasi zote kuanzia mwenyekiti, makamu mwenyekiti na wajumbe jambo ambalo Yanga wamekuwa wakilipinga muda wote.

Baada ya sarakasi zote hizo, bado Kamati ya Uchaguzi ya TFF, imeendelea kushikilia msimamo wake kwa kusema lazima nafasi ya mwenyekiti ijazwe kama ilivyo kwa nafasi nyingine katika uchaguzi huo utakaofanyika Januari 13, mwakani.

Jana Ijumaa, Kamati ya Utendaji ya Yanga na Kamati ya Uchaguzi ya TFF zilikutana ambapo Yanga iliwakilishwa na Hussein Nyika, Samuel Lukumay, Thobias Lingalangala na Siza Lyimo.

Lakini katika hali ya kushangaza, baada ya kumalizika kwa kikao hicho cha pande mbili, Nyika, alikuwa mtu wa kwanza kutoka ndani na kutokomea kusikojulikana, akifuatiwa na Lukumay, huku Lingalangala akiingia kwenye gari na kushindwa kuingia kwenye mkutano wa waandishi wa habari.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumalizika kwa kikao hicho, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Malangwe Mchungahela, alisema walisikiliza hoja za Yanga, lakini wamebaki na msimamo wao uleule.

“Hoja za Yanga tumezisikiliza lakini uchaguzi utabaki kuwa palepale na nafasi ya mwenyekiti lazima mtu agombee, kama Manji atataka kugombea nafasi ipo na mwisho wa kuchukua fomu ukifika tutafunga tu bila tatizo.

“Hatumtambui Manji kama mwenyekiti sababu aliwahi kuandika barua ya kujiuzulu, ni muda mrefu na suala hilo kwenye katiba lipo wazi kabisa.

“Na Yanga kwa muda mrefu walikuwa wanaelezwa suala la kufanya uchaguzi lakini walikuwa kimya, kuna wakati kwenye mkutano mkuu tulitegemea kuwa ni suala la uchaguzi kumbe wameenda kumpitisha Manji kuwa bado ni mwenyekiti wakati hakuna mkutano mkuu ambao unaweza kumrudisha kikatiba.



“Safari hii baada ya kusikia Manji amerudi Yanga, Agosti 9, mwaka huu TFF ilimuandika barua Manji kujua kama kweli yupo Yanga, lakini alikaa kimya na barua yake tumepokea Novemba 12, mwaka huu ambayo inaonyesha iliandikwa Oktoba 9, 2018.

“Katika barua yake hiyo, Manji alisema TFF wakitaka kujua cheo chake wawaulize Baraza la Wadhamini la Yanga.

“Lakini kwa nyakati tofauti tumekuwa tukimtafuta kiungwana kujua hatma yake ndani ya Yanga na hata Waziri Mwakyembe alikutana naye na akamwambia harudi tena Yanga.

“Hivyo, tutaendelea na uchaguzi kama kawaida na Yanga wamesema katika mkutano mkuu wa dharura watakaofanya hivi karibuni Manji atahudhuria kama mwanachama na siyo mwenyekiti,” alisema Mchungahela.

Kutokana na sintofahamu hiyo, Championi Jumamosi likamtafuta Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Hussein Nyika ili kuzungumzia walichojadili kwenye kikao hicho kama kweli wameridhia au la.

Alipopatikana, Nyika alisema: “Kweli tumeenda kwenye kikao hicho na hatukuafikiana vizuri kwa sababu sisi bado tunamtambua Manji ni mwenyekiti wetu, TFF wao hawataki kuelewa.

“Kama uchaguzi tutafanya bila ya shida yoyote, lakini kwa nafasi nyingine za makamu mwenyekiti na wajumbe wengine, lakini ile ya mwenyekiti mwenyewe yupo.

“Tunashangaa TFF sijui wanataka nini, kwanza ukiangalia hapa Yanga kuna ofisi zetu, lakini kwa nini fomu za uchaguzi zichukuliwe katika ofisi za TFF.”

CHANZO: CHAMPIONI

2 COMMENTS:

  1. Mbona kichwa Cha habari ni tofauti na contents zake?

    ReplyDelete
    Replies
    1. Kinachowasumbua Gazeti la Champion ni kujua tofauti yao na magazeti mengine kama Risasi. Mwisho wa sk nao wanaandika kama habari zile zinazopatikana kwenye magazeti yale mengine

      Delete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic