Na Saleh Ally
MWAKA 2009 nilifanikiwa kufika katika Mji wa Bouake, mji wa pili kwa ukubwa nchini Ivory Coast. Uko katikati ya nchi hiyo ya Afrika Magharibi.
Kutoka Jiji la Abidjan, Bouake iko takribani kilomita 450 hivi, kwa gari ni mwendo wa saa nne na nusu hivi. Ukiwa njiani kwenda Bouake, unapita mji mkuu wa Ivory Coast uitwao Yamoussokro.
Nilikwenda katika Mji wa Bouake katika kipindi ambacho ulikuwa unaonekana si salama kabisa hasa katika Serikali ya Rais Laurent Gbagbo aliyekuwa madarakani wakati huo huku mpinzani wake mkuu, Alassane Dramane Ouattara.
Kwa sasa Ouatarra ndiye amechukua nchi baada ya mapinduzi ya kijeshi. Lakini hata kabla ya kuchukua nchi, ulikuwa ukifika katika mji huo wenye wakazi takribani 600,000 watu watatu tu ndiyo walikuwa maarufu zaidi na hiyo imeendelea kuwa hivyo.
Watu hao wanaongozwa na Ouatara ambaye alikuwa anaonekana ni shujaa kutoka katika eneo hilo kupambana na serikali (wakati huo) na watu wa Ivory Coast wana tabia ya kujivunia nyota wao kupitia makabila mfano yake ya Baule, Senufo, Dan, Anye na Aowin.
Mashujaa wengine wawili ni Kolo Toure na mdogo wake wake, Yaya Toure. Hawa wawili hawakuwa wamewahi kupigana vita lakini ndiyo mashujaa wa Bouake pamoja na Ivory Coast nzima.
Watu wa Mji wa Bouake, waliamua kuwaruhusu watoto wao kuendelea kucheza soka na kuwasukuma kujifunza zaidi ili kufikia maisha ambayo watoto wa Toure waliyafikia lakini waliona si lazima kufikia huko, kwani hata robo yake bado ingekuwa ni mafanikio makubwa.
Matamanio makubwa ni mafanikio, lakini hata akademi maarufu ya Ivory Coast na Afrika kwa jumla la Asec Mimosas nayo ilijikita kuangalia vipaji vya vijana wengi katika eneo la Bouake na kuachana na kuamini kwamba wachezaji wengi wanaweza wakawa wanapatikana Abidjan pekee ambayo sasa ina wakazi zaidi ya milioni tano.
Uamuzi wa wazazi kuwaruhusu vijana wao kuonyesha vipaji, walioonyesha kuhamasishwa kwa kupewa nafasi na kuungwa mkono, ilisababisha wakati mmoja akademi nyingi za Ivory Coast kuwa na wachezaji wengi kutoka Bouake.
Hata sasa, wachezaji wengi wa Ivory Coast kuanzia wale wanaoshiriki ligi ya nchi hiyo lakini pia wanaocheza nje, wenye asili ya Bouake wanaonekana kuwa ni wengi au wana idadi kubwa ukilinganisha na sehemu nyingine.
Hapo ndiyo naanzia swali langu la leo ni kuhusiana na eneo la Mbagala ambalo liko nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam lakini limeendelea kuwa maarufu sana kwa mambo mengi.
Achana na ule umaarufu wa wimbo wa ‘Mbagala’ ulioimbwa na msanii Diamond kutoka Tandale, lakini kuna mashujaa kadhaa wa Mbagala na mmoja wao ni kijana mtoto wa askari polisi mstaafu.
Huyu ni Mbwana Ally Samatta ambaye sasa anakipiga katika Klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji na ndiye mchezaji Mtanzania anayefanya vizuri zaidi nje ya Bara la Afrika na ikiwezekana kwa wachezaji wote Watanzania wanaocheza nje ya hapa nyumbani.
Kufanya vema kwa Samatta si jambo geni tena kwa kuwa alionyesha tayari anaweza tangu akiwa nchi jirani ya DR Congo ambako aliitumikia TP Mazembe kwa mafanikio makubwa na kuandika rekodi za kutosha.
Alikuwa na haki ya kwenda kucheza Ulaya, tena akachagua Ubelgiji ambayo huenda palionekana hapafai lakini sasa kila kitu kinaonyesha alikuwa sahihi kwa kuwa ni mtu anayejiamini.
Samatta anafanya vizuri kazini kwake. Ameonyesha anajielewa kwa kuwa amejenga nyumba kadhaa, usafiri wa kutosha na amekuwa msaada katika familia yake na hata watu wengine wa karibuni yake, kadiri ya uwezo wake.
Kijana kuwa na ajira, anayejitegemea na shujaa wa taifa ni jambo la kujivunia kwa familia ya askari mstaafu Ally Samatta lakini sasa ni shujaa ya Wanambagala alipotokea.
Watu wa Mbagala wamewahi kumuonea wivu Samatta. Hapa ninazungumzia wivu wa kimaendeleo, kwamba mfano wazazi wamewahi hata kutamani kuona watoto wao wanafikia au kuyapita mafanikio ya Samatta ambaye leo amekuwa msaada wa jamii kwa kuwa amefikia hadi kujenga msikiti.
Kumuonea wivu kwa maendeleo kama walivyofanya watu wa Bouake kwa akina Toure na mwisho wamefikia mafanikio, ni jambo sahihi na muhimu kutokea kwa Mbagala kwa kuwa tukubaliane, Samatta hakucheza peke yake kufikia hapo alipo.
Samatta alicheza na wenzake akaweza kuonekana. Wengi ni wale waliotokea Mbagala. Kweli, Tanzania ina vipaji vingi kutoka sehemu nyingi. Unapopata dhahabu au almasi, basi eneo hilo inabidi uliangalie mara mbili, tatu au zaidi kwa kuwa dhahabu au almasi haiwezi kuwa moja tu katika eneo la mgodi.
Waliocheza na Samatta wapo, hata kama wamechelewa kwa sasa, wako wapi wadogo zao, nani anaanzisha akademi au nani anawahamasisha wajitume na kuendelea kupambana au yupi anautumia mfano wa Samatta kama hamasa kwa watoto na vijana wa Mbagala na maeneo ya jirani na ikiwezekana nchi nzima.
Bado kuna vipaji Mbagala, Samatta awe hamasa ya mabadiliko. Msiamini ni yeye tu baada ya hapo wameisha. Wazazi chunguzeni vipaji vya watoto wenu, wapeni nafasi zaidi. Kweli shule muhimu lakini mambo yakipangiliwa, yote yanawezekana na kwa mafanikio.
Hamasa hiyo inaweza kutembea jirani ya Mbagala, Dar es Salaam yote, mikoa mingine na ikiwezekana Tanzania nzima kwa kuwa tunahitaji akina Samatta wengi kujiondoa hapa katika tope tulipokwama.










Kijana umeandika vizuri. Lakini nadhani hujui kama kuna mtanzania wa kwanza alicheza professional footbal, Sunday Manara enzi hizo. Unashindwa kuelewa kwamba mpira ulikuwepo zamani, lakini baadae ukauawa na serikali ilipoondoa michezo mashuleni. Hujui kama kuna watu walipeleka Tanzania kombe la mataifa huru Africa sikuhizo mnaita AFCON? Na hatukuwa hata na professional player yeyote aliyecheza humo. Wachezaji sana walitoka African sports, Simba, Yanga, Coastal na nyinginezo. Nacho taka kusema ni kwamba vipaji vipo, wao wenyewe vijana wajitambue tu. Samatta na hata Ulimwengu ni mmoja kati ya vijana wachache wanaojitambua. Hawangoji kusukumwa kufanya mazoezi.
ReplyDelete