NA SALEH ALLY
HAKUNA watu wanaojua kila kitu na wasiotaka kujifunza kitu kama mashabiki wa soka Tanzania ukiwemo wewe unayesoma makala niliyoandika!
Inawezekana nitaanza kwa kukuudhi sana, lakini naona jambo zuri kusema ukweli kuliko kuendelea kuwapamba ili nionekane mzuri sana.
Utaguswa na makala niliyoandika kama utakuwa umewahi kufanya mambo nitakayoyazungumzia. Lakini unaweza kuguswa pia na ukaona kuna haya ya kutofanya mambo hayo hasa kama utaona kweli hayafai.
Unajua, sisi sote ni binadamu na tunakuwa na nafasi ya kukosea na baadaye kujirekebisha. Mwanadamu akipita katika njia hizi mbili, basi anapata nafasi ya kukua.
Unakumbuka ule msemo, “Kukua, kuona mengi.” Unaweza vipi kukua bila kuyaona mengi, unapoyaona unajifunza na ndani ya kujifunza kuna makosa mengi.
Niliwahi kusema mengi kuhusiana na Haruna Moshi, nikijua namuudhi. Kwamba yeye ni almasi iliyo mavumbini na yeye ndiye aliamua kuifanya almasi hiyo yenye thamani zaidi ya dhahabu iendelee kubaki katika hayo mavumbi.
Haruna, maarufu kama Boban angeweza kuwa tajiri mkubwa kama angetaka kuwa ni mtu mwenye mwendelezo na kujitambua uwanjani. Wako wengi wanaocheza soka leo hawafikii ubora wake lakini wamepata bahati ya kujitambua nje ya uwanja na kwamba wanataka nini.
Unapojitambua nje ya uwanja unakuwa na mipango ya maendeleo, sehemu unayotaka kufikia na unakuwa na subira na uvumilivu. Haya aliyakosa Boban ambaye alikuwa bora na mipango dhabiti uwanjani, nje ikawa tofauti akaanguka.
Unakumbuka akiwa Simba tegemeo na namna ilivyofikia akaondoka, ndani yake kulikuwa na neno “ametuchosha”. Lakini kumbuka pia alikuwa Sweden katika timu ya Gefle IF, iliyokuwa inamtaka sana abaki lakini mwisho ikaamua kumuachia na neno lilelile “ametuchosha”.
Mwisho ameamua kuamka, amekumbuka shuka kunakaribia kukucha lakini kupitia mfano ule wa kukosea na kujirekebisha, anakuwa sahihi kwa kuwa bado ana muda wa kucheza soka kwa miaka kadhaa na bado akafanya vizuri.
Hauwezi kuwa na hofu na Boban uwanjani. Kama mpira utamkataa siku moja lakini siku nyingine nyingi atakuonyesha namna anavyoweza kufanya vema na mambo yakawa safi sana kuliko hata ulivyoyatarajia.
Swali litabaki anaweza kuwa mvumilivu kwa kuwa anaofanya nao kazi Yanga si malaika, ni wanadamu na watamkosea. Je, ataweza kuvumilia kusubiri kile anachokipata kama kitakuwa kinachelewa, mambo ambayo alishindwa kuyafanya.
Boban ni mwanadamu kama mimi na wewe na anapaswa kupewa nafasi ya kutuonyesha kama ni yuleyule au amebadilika. Na hapa ndiyo ninaingia kwenye kundi la mashabiki wale wanaoamini wanajua kila kitu hata vile ambavyo hawajawahi kujifunza hata kwa kufuatilia au kusoma kwenye mtandao.
Nimeona mashabiki wengi sana wamemshambulia Boban na wakati mwingine hata Yanga waliomsajili wakitaka kuonyesha wamesajili “mzee” na kadhalika.
Wako hadi waliomshambulia Boban kwa maneno makali na kadhalika. Inawezekana ni ushabiki, sawa, inawezekana ni wivu, si vibaya lakini inawezekana ni kutotambua au kujua mambo lakini bado ukaendelea kujiona unajua.
Huna haja ya kumshambulia Boban ambaye ameonyesha amejifunza, ameonyesha ameumizwa na makosa na sasa anataka kuamka na kujirekebisha.
Kwani wewe shabiki umefanya makosa mangapi katika maisha, ukayajutia na kurejea baadaye ukajirekebisha na kufanya vema? Nani alikusakana, hakuna waliokutia moyo?
Je, unaamini Boban ana familia? Je, amefanya kosa kurejea na kucheza na sasa ametoka African Lyon na kwenda Yanga, hii ni hatua ya kusifiwa au kulaumiwa?
Wakati amekosea tulimsema bila ya hofu, ni jambo jema kwa kuwa tulionyesha hatupendi akosee. Sasa vipi ameamua kujirekebisha bado tunamlazimisha alale upande wa makosa!
Inaonekana mashabiki wengi wanaamini kusema vibaya pekee ndio jambo linaloweza kumfanya mtu aonekana ana uwezo, akili au ubora mbele ya wengine.
Kwa hali ilivyo, inaonekana anayesifia, au kupongeza ataonekana si mkosoaji au anayeweza kusikilizwa. Nafikiri kuna sababu ya kujifunza na kukubali kutoa nafasi kwa waliokosea nao kama wanadamu wapate nafasi ya kuonyesha wamebadilika na wamejutia makosa yao.
Tumpe nafasi Boban kwa kuwa hii ni fainali yake. Kama atafeli tena hapa na Yanga wakasema “ametuchosha” basi ndiyo itakuwa safari ya mwisho. Lakini kama mwanadamu ameona na kujutia makosa yake, sote tunaweza kutamani kumrudisha umri nyuma kwa kuwa suala la uwezo wa mpira kwake ni sawa na kuuliza makofi makali ya kushtukiza kituo cha polisi.
Tuache kusakama kabla ya kutoa nafasi. Na inapofikia wakati wa kukosoa, basi upendo utangulie. Unapokosoa kwa chuki, mara nyingi utajikuta unazungumza pumba kwa kuwa hakuna muunganiko kati ya moyo ya ubongo uliozama kwenye ukosoaji wenye mashiko.
Umechemka kikokotoo ulichotumia kuwahukumu wasomaji kinatia kinyaa.unatukana halafu unatoa tafsiri ya matusi umechemka
ReplyDeleteWasomaji always mnapenda kulaumu kila kitu.
ReplyDeleteNa ndiyo maana akaandika hapo juu kwenye aya za mwanzo.
Mhh ndugu yetu Saleh sasa sisi washabiki kosa letu nini? Umezunguka sana halafu unarudi palepale.Timu zote alizochezea na maana ya Simba, Coastal Union,Mbeya City, Lyon na hiyo ya Sweden aliondoka mwenyewe na hakufukuzwa licha ya vituko lukuki aliyowafanyia Simba na Gefle.Kama Boban amekumbuka shuka asubuhi basi tusubiri matokeo na sio kutuhukumu wakati asubuhi hakujakucha.
ReplyDelete