December 12, 2018



Na Saleh Ally
UNAWEZA kusema inachosha lakini kwa mtu ambaye unalenga kufanya jambo sahihi kamwe hauwezi kuchoka.

Naendelea kulizungumzia suala la beki wa Simba, Juuko Murshid, mchezaji ambaye msaada wake ndani ya Klabu ya Simba ni msaada duni na ule unaopatikana kwa mafungu.

Nitakueleza kwa nini ninasema mafungu. Juuko ni raia wa Uganda ambaye amekuwa akiichezea Simba kwa zaidi ya misimu mitatu sasa na mimi naungana na wote wanaosema ni beki mzuri.

Kinachonivuta mara kwa mara kusema Juuko si mtu sahihi Simba ni zile tabia ambazo nyingi tunazisikia kutoka kwa viongozi wa Simba au makocha wao.

Hizi tabia si za leo wala jana na zimekuwa zikiendelea mara kwa mara bila ya kuwepo kwa ufafanuzi na binafsi ninaona kwa ukubwa wa Simba, unyeyekevu kwa Juuko umetosha.


Kilichoniamsha na kuandika haya leo ni baada ya kusikia kocha Patrick Aussems amemtaka Juuko kupumzika kutokana na kuchelewa kurejea kambini na ilielezwa hakukuwa na taarifa za yeye kukosa mazoezi siku kadhaa huku ikiwa inaelezwa yuko jijini Dar es Salaam na wengine wakisema yuko jijini Kampala.

Kweli Juuko ni beki bora, lakini faida yake kwa Simba ni pale anapoamua. Kama unakumbuka, hivi karibuni wakati Aussems raia wa Ubelgiji akitua kuinoa Simba, beki huyo alikuwa kwao Kampala baada ya kuingia kwenye mgogoro na Kocha Pierre Lechantre ambaye alilalamika tabia ambayo aliamini ni utovu wa nidhamu.

Baada ya Aussems kumuona akiichezea timu ya taifa ya Uganda ‘The Cranes’ pia akiwa hayupo Simba, akataka aitwe kuendelea na majukumu yake. Leo siku chache au baada ya mechi chache, tayari naye amesema apumzike.

Kitaalamu, Aussems anahofia kuvunja morali ya timu yake kabla ya kuwavaa Nkana FC katika ligi ya mabingwa. Mbelgiji huyo anajua athari za kumruhusu mchezaji ambaye ameonyesha utovu wa nidhamu katika kikosi kinachojiandaa kupambana.


Hata kama ni ya kwanza kwa Juuko kufanya hivyo mbele ya Aussems, hii si ya kwanza kwake dhidi ya Simba au makocha kadhaa. Maana yake ameshindikana na hakika kama uongozi ungekuwa imara, basi useme dharau kwa Simba basi!

Haitatokea hata siku moja mchezaji yeyote unayemjua akawa mkubwa dhidi ya klabu kubwa kama Simba. Klabu hiyo ni watu na ukubwa wake unaundwa na mioyo ya watu, hivyo haiwezi kuzidiwa ukubwa na moyo mmoja wa mtu.

Viongozi wa Simba wanapaswa kubadilika kiweledi. Kwamba hofu ya kumuacha Juuko eti kwa kuwa atachukuliwa na Yanga na kule atacheza vizuri halafu wao wataonekana hawana mipango ni mambo ya kizamani yaliyopitwa na wakati. Lakini ni hesabu za kienyeji zisizo na nafasi kwa wakati huu.

Juuko anapaswa kuiheshimu Simba na kama ameshindwa, aachiwe aende ambako anaona sawa na ambao watakuwa tayari kumruhusu. Sidhani kama Yanga wangeweza kumpa nafasi ya uvumilivu huo wa kobe anayekubali kuonewa bila sababu na akaficha kichwa chake.

Juuko ni mchezaji wa kigeni anayepaswa kuwa mfano kiutendaji na mwenye nguvu ya uhamasishaji kuinua morali ya timu kwa maana ya utendaji wake uwanjani lakini maisha sahihi yanayojali nidhamu.

Hakuna haja ya kuwa na wachezaji wa kigeni mfano mbaya, wanaocheza wakitaka, wanaojiunga na timu wakitaka wao na wanaoonyesha dharau kwa kocha, wenzao na viongozi wao.

Tunataka kujenga wachezaji wetu, tunataka kujenga kizazi bora kwa kukipa changamoto sahihi. Huyu Juuko kama kiushabiki, ni mchezaji anayepaswa kubaki Simba na kuendelea kupata anachotaka huku yeye akichagua acheze vipi au aitumikie vipi klabu. Lakini kama ni kwa kufuata weledi, usahihi na nia ya kuifanya Simba kuwa ni yenye nidhamu, inayoheshimika na kubwa, basi hafai na anapaswa kuachiwa aende.

Simba ni kubwa ikiwezekana kuliko timu zote za Uganda anapotokea Juuko. Umaarufu wa Simba umesambaa Afrika kuliko timu zote za Uganda kwa sasa na hii inaweza kuwa sababu moja tu inayoweza kumfanya Juuko naye kuiheshimu klabu hiyo.

Naongeza ushauri wa ziada, kama Juuko ataendelea kupewa nafasi hii ya kuidharau na kufanya anavyotaka ndani ya Simba, basi viongozi mjue mnatengeneza mpasuko taratibu sana lakini mwisho wake, utakuwa mkubwa na kuudhibiti utakuwa ni mtihani mkubwa na mtajuta.

Mawili yatokee, Juuko ambaye anaonekana ameshindikana, abadilike kwa nafasi hii ya mwisho. Ikishindikana, aachwe aende zake.


6 COMMENTS:

  1. Kaongeleee tabia za Yondani...huna lolote na blog yako ya udaku

    ReplyDelete
  2. Yondani ameigomea yanga mara ngapi hatujakusikia ukiandika chochote juu ya tabia yake

    ReplyDelete
    Replies
    1. Umeelewa alichokiandika? Huyo unaemtuhumu ni simba zaidi yako wewe hata kadi Huma.

      Delete
  3. Hukumu ya Juuko itatolewa na kocha mkuu ndie atakaeamua kama Juuko aende au la. Si raisi wa timu au mshabiki wa Simba atakaesema Juuko aondoke kama kocha hajasema kashinda. Mwandidhi au shabiki kazi yake ni kutoa maoni na sio kulazimisha au kushinikiza mchezaji kuachwa kila mtu lazima ajue mipaka yake.

    ReplyDelete
  4. Acha kukariri wewe,sio kila mwenye kadi ya chama au club ukadhani ana mapenzi nayo wengine wanachukua kwa maslahi ya kazi zao,sasa wewe kariri tu uone kitakachokuapata.

    ReplyDelete
  5. Hivi tabia ya mwandishi wa makala za habari kuingilia uhuru wa vilabu na kuwashauri nani afukuzwe nani abakie hili linatoka wapi? Kwani wenyewe Simba hawaoni? Wewe ni nani unataka kuwaamulia? Aliyekwambia akiachwa ataenda Yanga nani? Mimi nakushauri nenda chukua fomu ugombee nafasi za uongozi kwenye vilabu hivi huko sasa utakuwa sahihi kupendekeza haya unayotaka yatokee.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic