December 3, 2018



NA SALEH ALLY
MARA baada ya kusikia Steven Mguto anawania nafasi ya Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi (TPLB), nikaanza kujipa maswali mengi sana ambayo huenda lengo lilikuwa ni utafakari tu kwa lengo la kutaka au kujiaminisha ipi hasa ni njia sahihi ya mpira wa Tanzania.

Sijawahi kuwa na hofu na Mguto kwamba si kiongozi mzuri, lakini moja kwa moja nikawa nawaza, kama kweli Mguto atashinda uchaguzi, maana yake vyombo viwili vikuu vya soka vitakuwa vinaongozwa na watu kutoka katika klabu moja.

Yaani, Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia ni mmoja wa viongozi wa zamani wa Coastal Union na Mguto ni mwenyekiti wa klabu hiyo. Kwanza kabisa nilianza kujipa maswali kama kutakuwa na usawa.

Jibu ya hilo ni hadi pale Mguto atakapoingia baada ya kushinda na kufanya kazi. Sikuwa nikiamini watu wawili kutoka klabu moja wakiwa viongozi wa TFF na Bodi ya Ligi ni dhambi. Lakini wanaweza kuvumilia na wote wakawa ni sawa wanaowaza maendeleo ya soka la nchi yetu na si maendeleo ya klabu yao.

Baada ya muda, taarifa za mkutano mkuu ambapo ndani yake kungekuwa na huo uchaguzi wa bodi ukawa unafanyika Tanga. Kwao Mguto, Karia na Coastal Union. Bado nikajipendekezea kuwa mtulivu na kutaka kuona.

Mwisho, ameshinda Mguto kutoka Coastal Union, anaungana na Karia wa Coastal Union kwa lengo la kuongoza mpira wa Tanzania kwenda katika maendeleo.

Nikae kimya, nani kasema? Acha niwe wa kwanza kutoa tahadhari na kuzikumbusha pande zote mbili. Upande wa viongozi, yaani Karia na Mguto lakini upande wa wadau ambao wadau wataongozwa na viongozi.

Nianze na viongozi, tunajua sote kwamba kila mwanadamu ana matamanio yake binafsi, kila mwanadamu ni mbinafsi na kama unataka kuwa tofauti lazima upigane na uanadamu ili uwe unayetenda haki na usawa.

Unaweza kujaribu kukata tunda la chungwa katikati, mara zote kunakuwa na kubwa na dogo na utaona, wengi wangependa kuanza kula kubwa ili ikitokea akaombwa atoe dogo. Au kama atakuwa anagawana na mwenzake, basi atachagua kumpa dogo. Lakini kama unataka kujifunza na kupambana na hali ya maumbile ya kawaida ya mwanadamu, basi mpe lile kubwa na wewe baki na dogo. Somo litaanzia hapo.

Hivyo hakuna ubishi, wasipoangalia kwa kuwa wote ni viongozi wa Coastal Union wanaweza wakachotwa na ushawishi wa kupindisha haki katika mambo kadhaa. Maana likitajwa suala la klabu kunakuwa hakuna ushindani na tumeliona hili hata pale TFF pekee kunapokuwa na viongozi wenye ushabiki wa klabu moja, mara nyingi mambo yalikuwa yakienda ndivyo sivyo.

Coastal Union tunaijua, imeshindwa kusimama na kubaki ligi kuu hata misimu minne mfululizo. Panda shuka ndiyo maisha yake, sasa ya huko, yabaki hukohuko.

Kwa wadau, pia nanyi mnapaswa kuwa watenda haki kwa viongozi hao. Kwamba kama tutakuwa tunawaangalia kwa hisia pekee, huenda hatutawatendea haki.

Inawezekana kabisa wakawa wamekosea sehemu kwa maana ya kiongozi naye ni binadamu. Basi kila kitu tusiamini kimetokea kwa kuwa wao ni Coastal Union.

Tuliona Coastal Union ilivyopanda kwa ugumu kurejea Ligi Kuu Bara, lakini wengi tuliamini eti ni kwa sababu tu Karia ni Rais wa TFF.

Tunaweza kuwa na subira na kuangalia mwendelezo ulivyo. Pale tutakapoona kuna matatizo au makosa ambayo yanapaswa kuzungumziwa, basi tuwe huru kwa ajili wote wawili, yaani Karia na Mguto ni watumishi wa umma wa Watanzania katika mpira, vyombo wanavyoongoza ni mali ya sisi Watanzania.

Kikubwa kabisa, tujitahidi kuwaunga mkono na kuepusha lawama hata kama haikutakiwa kuwa hivyo.


1 COMMENTS:

  1. Hakuna tatizo kama watasimamia sheria na kanuni za kazi na uwajibikaji bila ya upendeleo

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic