Kuna vizazi vitatu vya utangazaji; cha kwanza ni kizazi cha wakongwe. Hiki kinawajumuisha kina Rainfred Masako, Julius Nyaisangah (marehemu), Halima Mchuka (marehemu), Charles Hillary ‘Tishio’, Deogratius Rweyunga, Juma Nkamia ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Chemba (CCM) na wengineo. Kizazi hiki ni kile cha mwanzo kabisa, kikianzia Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD).
Kuna kizazi kipya, hiki kiliibuliwa na Redio za FM, miaka ya mwishoni mwa 90’ na mwanzoni mwa mwaka 2000 hadi 2010. Hapa wapo watangazaji kama Taji Liundi, Saleh Jabir, Misanya Bingi (marehemu), Godwin Gondwe (sasa Mkuu wa Wilaya ya Handeni), Rose Chitala, Sebastian Ndege, Regina Mwalekwa, Abdallah Mwaipaya, Fina Mango, Fred Fidelis ‘Fredwaa’, Neema Diwani na wengine.
Kizazi cha mwisho ni hiki cha sasa cha Bongo Fleva; hiki kimekuta tayari muziki wa Bongo Fleva una heshima na kukubalika na watu wa rika zote. Hapo utakutana na kina Adam Mchomvu, Sam Misago, Salama Jabir na wengineo. Katika makala haya, nakupa listi ya watangazaji wa kizazi kipya ambao nyota zao zinawaka muda wote. Yaani tangu wamechomoza, wameendelea kuwa ‘hot’ mpaka leo.
MAULID KITENGE
Huyu ni habari nyingine unapozungumzia watangazaji wakali katika vipindi vya michezo. Alianza kupata jina akiwa Radio One na ITV alipotumikia kwa miaka 14, kabla ya kujiunga na Radio E FM, Agosti, 2014 ambapo yupo mpaka leo. Vipindi anavyotangaza kwa sasa ni pamoja na Sport Headquarters, E-Sports na Joto la Asubuhi. Pia anasoma taarifa za habari.
MASOUD KIPANYA
Jina lake halisi ni Ali Masoud ambaye anatamba kwenye vipindi vya asubuhi. Ni miongoni mwa waasisi wa Kipindi cha Power Breakfast, akiwa na wenzake Gerald Hando na Fina Mango.
Aliondoka Clouds mwaka 2008 yeye na Fina, ambapo alikwenda kujishughulisha na program ya kipindi maarufu cha runinga kiitwacho Maisha Plus na baadaye kingine cha Inawezekana. Alirejea tena Clouds mwaka 2016 na kujiunga na watangazaji Babra Hassan, Fredwaa na Said Bonge a.k.a Bonge katika kipindi hicho, baada ya Hando na Paul James ‘PJ’ kutimkia Radio E – FM. Hata hivyo, baadaye PJ alirejea tena Clouds.
GARDNER G. HABASH
Huyu ni mwamba wa vipindi vya jioni, ingawa awali alianzia vipindi vya asubuhi. Ndiye muasisi wa Kipindi cha Jahazi kinachorushwa na Radio Clouds FM.
Alianzia katika kituo hicho, baadaye akaondoka na kwenda kujiunga na Radio Times FM alipokuwa akitangaza kipindi cha Maskani kabla ya kuchukuliwa na Radio E FM akisimama na kipindi cha Ubaoni. Aprili, mwaka huu, Gardner aliamua kurejea tena mjengoni Clouds FM kuungana na swahiba wake Ephrahim Kibonde na George Bantu katika kuendeleza kusongesha Jahazi.
SALAMA JABIR
Aliibuliwa na Kipindi cha Planet Bongo katika Radio East Africa ambapo alikuwa akiwachana wasanii wa Bongo Fleva wanaofanya vibaya.
Baadaye mwaka 2008 aliondoka kituoni hapo, mikoba yake akamwachia Abdallah Ambua ‘Dulla’. Anatambulika kama mmoja wa majaji wa shindano maarufu la muziki – Bongo Star Search ‘BSS’ na mtangazaji wa kipindi cha Mkasi ambacho huwahoji mastaa wa fani mbalimbali Bongo. Aina ya utangazaji wake, akitumia maswali ya kichokozi ndiyo hasa iliyompaisha na kumuacha kileleni hadi sasa.
MILLARD AYO
Ana historia ndefu katika safari yake ya utangazaji, akianzia TV Z visiwani Zanzibar, Wapo Radio ambayo ni ya dini, baadaye ITV na Radio One ambapo alitangaza habari za michezo katika Runinga ya ITV na kipindi cha burudani cha ‘Milazo 101’. Baadaye alijiunga na Radio Clouds FM ambapo aliasisi Kipindi cha Amplifaya, pia anatangaza kipindi cha Clouds FM Top 20. Kinachomuweka Millard pazuri ni namna yake ya kuzungumza kwa vituo, utani na kuchambua mambo.
ABOUBAKAR SADICK
Kama angekuwa ni mcheza soka, ningeweza kusema Abou ‘Kwafujo’ anacheza miguu yote. Ana kipaji cha kipekee katika utangazaji.
Ni kati ya waasisi wa vipindi vya muziki wa Bongo Fleva kama The Heat na Dj Show katika kituo cha Radio One Sterio anachotumikia hadi sasa. Ana zaidi ya miaka 15 kituoni hapo. Vipindi vingine alivyopata kuwika navyo ni Nani Zaidi na Chombeza Time. Alijiunga na kituo hicho tangu mwaka 1999 akitokea Radio Tanzanite ya jijini Arusha. Abou ni Dj mkali na anasoma habari. Kwa sasa anatangaza vipindi vya Midundo Motomoto na Nani Zaidi.
WENGINE
Watangazaji wengine ambao bado wapo hot na vituo wanavyofanyia kazi kwa sasa kwenye mabano ni pamoja na Khadija Shaibu (Times FM), Fredrick Bundala (Dizim TV), Ephrahim Kibonde (Clouds FM) na Dina Marios (E FM).
Naona mewasahau wakongwe kama Ahmed kipozi Amina Mungi Faudhia Taabud, Betty mkwasa na Hata Ephraim Kibonde alikua mwingi kuliko Kitenge
ReplyDelete