MASKINI DIMPOZ!! HOI TENA, AKIMBIZWA UJERUMANI
Tumuombee! Hiyo ndiyo kauli fupi na yenye ujumbe mzito aliyoitamka baba mzazi wa msanii wa Bongo Fleva, Omary Nyembo ‘Ommy Dimpoz’, Faraji Nyembo ‘Baba Dimpoz’ akizungumzia hali ya mwanaye.
AMEKIMBIZWA UJERUMANI
Awali, mtu wa karibu na familia ya Dimpoz ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini, alilieleza Ijumaa Wikienda kuwa, hivi karibuni Dimpoz alikuwa hoi kwa mara nyingine tena hivyo kulazimika kukimbizwa nchini Ujerumani kwa ajili ya matibabu.
Alisema baada ya kufanyiwa upasuaji wa awali wa koo hadi tumboni, staa huyo wa Wimbo wa Wanje, alipata tatizo la kujaa usaha ambalo ndilo lililomfanya azidiwe na familia ikalazimika kumpeleka Ujerumani baada ya kushauriwa kuwa kuna wataalam wazuri wa tatizo lake.
“Kama unakumbuka baada ya kufanyiwa upasuaji ule wa awali, Dimpoz alikwenda kupumzika Mombasa (Kenya). Baadaye alipokwenda kuchekiwa baada ya miezi mitatu kupita, alikutwa na tatizo hili la usaha, akapatiwa matibabu kisha kurejea nchini,” alisema mtu huyo.
TATIZO LAREJEA
Alisema baada ya kushughulikiwa tatizo hilo kisha kurejea nchini, tatizo hilo la usaha kujaa lilimrudia na ndipo walipoamua kumpeleka nchini Ujerumani. “Tuliamini sasa Dimpoz anarudi kwenye hali yake maana alionekana kupata ahueni kubwa, lakini ndiyo hivyo tena, hali ilibadilika ghafla,” kilisema chanzo hicho.
Hata hivyo, picha kubwa kwenye ukurasa wa mbele wa gazeti hili ni ya kipindi ambacho Dimpoz alilazwa nchini Afrika Kusini akisumbuliwa na tatizo hilohilo lilifanya akimbizwe nchini Ujerumani.
BABA ATHIBITISHA
Baada ya kuzungumza na mtu huyo wa karibu na familia, Ijumaa Wikienda lilimvutia waya baba mzazi wa Dimpoz aliyeko Sumbawanga mkaoni Rukwa ambapo alipopatikana alithibitisha mwanaye kuzidiwa hivi karibuni na kwamba amepelekwa nchini Ujerumani kwa matibabu zaidi.
“Ni kweli walinijulisha kwamba mwanangu amezidiwa tena, wakampeleka Ujerumani kwa ajili ya matibabu zaidi kisha kufanyiwa operesheni kwa mara nyingine na nimekuwa nikiwasiliana nao kujua hali yake,” alisema baba Dimpoz.
Baba Dimpoz alipoulizwa kuhusu hali ya mwanaye kwa sasa, alisema anamshukuru Mungu anaendelea vizuri, lakini bado anaendelea na matibabu nchini humo na anaomba Watanzania wazidi kumuombea ili arejee kwenye hali yake ya kawaida na aweze kuwaburudisha kama zamani. “Kikubwa kabisa niwaombe Watanzania wenzangu tumuombee Dimpoz, bado anaumwa yupo hospitalini, tumuombee aweze kuwa na afya njema,” alisema Baba Dimpoz.
MENEJA WAKE ANASEMAJE?
Ijumaa Wikienda lilimtafuta meneja wa msanii huyo, Christina Mosha ‘Seven’ ili kujua anaendeleaje kwa sasa, lakini jitihada hizo hazikuzaa matunda kufuatia simu yake ya mkononi kutopokelewa.
Hata hivyo, mmoja wa watu wa karibu kabisa na Dimpoz ambaye hakupenda jina lake lichorwe gazetini alieleza kuwa Dimpoz kwa sasa anaendelea vizuri baada ya kupatiwa matibabu nchini humo na kwamba hali aliyokuwa nayo awali na sasa, ni vitu viwili tofauti, afya yake imeimarika maradufu na sasa anaweza kuongea vizuri kwani sauti inatoka.
“Kwa sasa kwa kweli tunamshukuru Mungu yupo vizuri. Alivyoenda kule na alivyo sasa kwa kweli tuna kila sababu ya kumshukuru Mungu, amepata ahueni kubwa,” alisema mtu huyo.
UGONJWA WA DIMPOZ
Dimpoz alianza kuumwa mapema mwaka huu ambapo kwa mujibu wa taarifa za madaktari wa Afrika Kusini alipokwenda kufanyiwa upasuaji wa awali, msanii huyo alikunywa sumu iliyowekwa kwenye kinywaji na kumsababishia tatizo kwenye koo kuziba.
Kabla ya kupelekwa Afrika Kusini, alianza kupatiwa matibabu nchini Kenya, lakini hata hivyo, madaktari walishauri aende kufanyiwa upasuaji Afrika Kusini kutokana na uzito wa tatizo lake. Upasuaji wa awali ulifanyika vizuri, akarejea nchini, lakini hali ilibadilika na sasa yupo Ujerumani kwa ajili ya matibabu zaidi.
MHARIRI
Ijumaa Wikienda linatoa pole kwa Dimpoz na familia yake na kumuombea kwa Mungu ili aweze kupona na kurejea kwenye majukumu yake ya kila siku.
Kutoka GPL
0 COMMENTS:
Post a Comment