KUMEKUCHA!! MANJI KUREJEA KWA KISHINDO YANGA
KUMEKUCHA Yanga! Hivyo ndivyo unavyoweza kusema baada ya taarifa mpya kuibuka klabuni hapo mara tu baada ya uchaguzi wa kuziba nafasi za viongozi zilizoachwa wazi ikiwemo ile ya mwenyekiti kusitishwa Ijumaa iliyopita kutokana na baadhi ya wanachama wa klabu hiyo kukimbilia mahakamani kupinga zoezi hilo ambalo lilitakiwa kufanyika jana Jumapili.
Hata hivyo wakati ufumbuzi wa suala hilo ukitarajiwa kupatikana leo hii, taarifa mpya ambazo sasa zipo ndani ya Yanga ni juu ya kurejea klabuni hapo kwa aliyekuwa mwenyekiti wa klabu hiyo, Yusuf Manji.
Ikumbukwe kuwa kabla ya kufikiwa uamuzi huo wa kuziba nafasi hizo uliofikiwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambalo pia limekuwa likisimamia mchakato mzima wa uchaguzi huo, Novemba 11, mwaka jana.
Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la Yanga ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, alisema kuwa Manji ataanza kwenda ofisini kwa ajili ya kazi zake za uenyekiti wa klabu hiyo kuanzia Januari 15, mwaka huu ambayo ni kesho Jumanne.
Mkuchika alisema kuwa, Manji aliliambia baraza hilo la wadhamini wa Yanga kuwa tarehe hiyo ndipo ataanza kwenda ofisini kwake Yanga.
Baadhi ya wanachama wa Yanga wamejiandaa kumpokea kiongozi wao hiyo kama atatokea klabu hapo hiyo kesho kama alivyowaahidi kupitia barua yake hiyo aliyokuwa akilijibu baraza hilo la wadhamini la Yanga kuridhia maombi ya wanachama hao.
Kwa mujibu wa Championi, mmoja kati ya wajumbe wa kamati ya utendaji wa klabu hiyo alisema: “Wanachama wengi wamejiandaa kuona hiyo Jumanne itakuwaje, je kiongozi wao huyo wanayempenda kweli ataanza kuja ofisini kama alivyokuwa ameahidi?
“Lakini pia wanasubiria kuona ni maamuzi gani yatakayotolewa na mahakama hii leo baada ya baadhi ya wanachama kwenda kufungua kesi ya kuzuia uchaguzi huo wa kuziba nafasi za viongozi zilizo wazi ikiwemo ile ya mwenyekiti ambayo TFF wanadai kuwa nayo ipo wazi wakati wanachana wao wanajua kuwa mwenye nafasi hiyo yupo.”
Alipotafutwa Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Omary Kaya simu yake ya mkononi iliita tu bila ya kupokelewa lakini Ofisa Habari wa timu hiyo, Dismas Ten alipoulizwa kuhusiana na hilo alisema: “Sina taarifa yoyote kuhusiana na hilo mezani kwangu.”
Tunazidi kuchelewesha tu maendeleo ya club.
ReplyDelete